Christopher Msagati - Mahakama, Manyara
Mahakimu
wa Mahakama Kuu Kanda ya Manyara wameelekezwa kuzingatia utekelezaji wa malengo
yanayowekwa na Viongozi wa Mahakama Kitaifa pamoja na Kanda ili kuhakikisha
jukumu la Utoaji Haki kwa wakati linatimia ipasavyo.
Hayo
yamesemwa jana tarehe 24 Februari, 2025 na Kaimu Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu,
Kanda ya Manyara Mhe. Devotha Kamuzora wakati wa kikao kazi kilichofanyika katika
Ukumbi wa mikutano Mahakama Kuu Manyara. Lengo la kikao kazi hicho lilikuwa
kufanya tathmini ya Utendaji kazi wa mwaka 2024 na kuweka mipango na matarajio
mapya kwa mwaka 2025.
Aidha,
Mhe. Kamuzora alisisitiza kwa Mahakimu wote kuhakikisha kwamba, wanazingatia
muda wa kumaliza mashauri ambao umewekwa na Uongozi wa Kanda.
“Sote
tunajua kuwa Mahakama Kuu Kanda ya Manyara tumejiwekea malengo ya kumaliza
mashauri yanayofunguliwa Mahakama Kuu, Mahakama ya Hakimu Mkazi Pamoja na
Mahakama za Wilaya ndani ya miezi sita, aidha kwa Mahakama za Mwanzo tumeweka
Malengo ya kumaliza mashauri hayo ndani ya miezi mitatu. Ni wajibu wa kila
mmoja wetu kuhakikisha kuwa anajitahidi kufanikisha malengo hayo ili wananchi
hawa tunaowahudumia wazidi kuwa na imani na Mahakama yetu” alisema Mhe.
Kamuzora.
Akichangia
katika taarifa iliyosomwa na Naibu Msajili wa Mahakama Kuu, Kanda ya Manyara
Mhe. Bernard Mpepo. Jaji wa Mahakama Kuu, Kanda ya Manyara Mhe. Nenelwa
Mwihambi alipongeza juhudi zilizofanywa katika mwaka 2024 kwa kuwa hapakuwa na
mashauri ya mlundikano katika Mahakama Kuu Kanda ya Manyara, Mahakama ya Hakimu
Mkazi, Mahakama zote za Wilaya pamoja na Mahakama zote za Mwanzo zilizopo.
“Waheshimiwa
Majaji na Mahakimu kwa kweli mnastahili pongezi kwa kuwa tumemaliza mwaka 2024
pasipo kuwa na mashauri ya mlundikano, nawasihi tuendelee na moyo huu kwa mwaka
2025,” alisema Mhe. Mwihambi.
Naye,
Mtendaji wa Mahakama Kuu, Kanda ya Manyara Bi. Nyanzobe Magambo Hemedi,
ameahidi kuendelea kutoa ushirikiano wake kwa Maafisa Mahakama hao Kanda ya
Manyara kwa kuhakikisha anafuatilia upatikanaji wa watumishi, ukamilishaji wa
miradi ya ujenzi pamoja na upatikanaji wa vitendea kazi ili kufanikisha kazi
zinafanyika bila usumbufu wowote.
Katika
upande mwingine, Majaji, Naibu Msajili, Mahakimu wa Ngazi zote, Mtendaji wa
Mahakama, Mafisa Utumishi na Tawala, Wakuu wa Vitengo kutoka Mahakama Kuu,
Kanda ya Manyara na Watumishi wengine waliopo katika jengo la Mahakama Kuu
Manyara walipata fursa ya kupata Elimu inayohusu Afya ya Akili kutoka kwa
wataalamu wa Hospitali ya Mkoa wa Manyara Dkt. Karim Mbonde na Dkt. Noel
Nywelo. Zoezi hili la utoaji elimu hiyo lilifanyika kabla ya kufanyika kikao
kazi hicho.
Kaimu
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Kanda ya Manyara Mhe. Devotha Kamuzora akizungumza
jambo wakati wa Kikao kazi kilichofanyika Mahakama Kuu Manyara tarehe
24/02/2025.
Jaji
wa Mahakama Kuu, Kanda ya Manyara Mhe. Nenelwa Mwihambi akichangia mada wakati wa
kikao kazi cha Mahakimu na viongozi wengine wa Mahakama Kuu, Kanda ya Manyara.
Naibu
Msajili wa Mahakama Kuu, Kanda ya Manyara Mhe. Bernard Mpepo akitoa taarifa ya
Utendaji kazi kwa Mwaka 2024 katika kikao kazi cha Mahakimu na viongozi wengine
wa Mahakama Kuu Kanda ya Manyara.
Hakimu
Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Manyara Mhe. Mariam Lusewa (wa kwanza kulia) pamoja Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya
Mbulu Mhe. Johari Kijuwile wakifuatilia matukio katika kikao kazi cha Mahakimu na viongozi wengine wa
Mahakama Kuu, Kanda ya Manyara.
Sehemu ya watumishi wa Mahakama Kuu, Kanda ya Manyara wakifuatilia mafunzo ya Elimu ya
Afya ya akili kabla ya kuanza kwa kikao kazi cha Mahakimu na viongozi wengine
wa Mahakama Kuu, Kanda ya Manyara.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni