Na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Mustapher Mohamed Siyani amewaongoza watumishi wa Mahakama Kuu Masjala Kuu kumuaga aliyekuwa Jaji wa Masjala hiyo, Mhe. Frederick Manyanda ambaye ameteuliwa kuwa Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Sumbawanga.
Akizungumza wakati wa hafla fupi ya kumuaga Jaji Manyanda leo tarehe 25 Februari, 2025 katika ukumbi wa mikutano wa Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma, Mhe. Dkt. Siyani amesema kuwa, ana imani na utendaji kazi wa Mhe. Manyanda.
“Mtu anapoteuliwa kuwa Mfawidhi anabeba majukumu ya ziada ya kazi yake na wale wanaoteua huwa kuna majina mengi lakini Mungu akasema sasa ni zamu ya Jaji Manyanda kwa sababu ninaamini kuwa uteuzi wowote ule huwa unaanza na Mungu halafu binadamu anakuja tu kugonga muhuri kile ambacho Mungu ameshakifanya,” amesema Jaji Kiongozi.
Amesema kuwa, hana wasiwasi na juu ya uwezo wa Jaji Manyanda katika kushirikiana na wengine, ukarimu wake, lugha nzuri sambamba na uchapakazi na kuongeza kuwa hizo ni baadhi ya sifa za Kiongozi.
Amemtaka kusimamia uondoshaji wa mashauri, kusikiliza malalamiko ya wananchi, kutatua migogoro kwa haki na kuhakikisha kuwa wananchi wa Sumbawanga wanapata huduma ya haki kwa wakati.
“Nikutakie heri sana Mheshimiwa, kule kuna mashauri mengi kuliko uliyokuwa nayo hapa nenda ukayasimamie, kahakikishe kwamba Watanzania waliopo katika Kanda ile kwa maana ya Rukwa na Katavi wanapata huduma ya haki kwa wakati,” amesisitiza Mhe. Dkt. Siyani.
Mhe. Dkt. Siyani amemtoa wasiwasi Jaji Manyanda kuwa, Sumbawanga pia ni sehemu nzuri ya kufanyia kazi na kueleza kuwa naye amewahi kufanya kazi katika Kanda hiyo miaka 14 iliyopita.
Kadhalika, Jaji Kiongozi ametoa rai kwa watumishi wengine kuwa tayari kufanya kazi mahali popote wanapopangiwa kwakuwa wote.
Naye Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Sumbawanga, Mhe. Frederick Manyanda amemshukuru Jaji Kiongozi pamoja na watumishi kwa tukio la kumuaga.
"Kwanza kabisa nimeshtushwa na 'surprise' hii kwa kuwa nilifuata mizigo yangu na tayari gari lilikuwa limeshawashwa kwa ajili ya kuanza safari kuelekea Masjala ndogo Sumbawanga," amesema Jaji Manyanda.
Mhe. Manyanda amemshukuru Jaji Kiongozi kwa kuacha majukumu yake na kuja kujumuika na watumishi wengine kwa lengo la kumuaga. Aidha, amekiri kufurahi kufanya kazi Masjala Kuu kwa kuwa ndio sehemu aliyojifunza kufanya kazi bila karatasi yaani (paperless) na kuhaidi kuchukua ujuzi huo na kuwapelekea Masjala ndogo Sumbawanga waweze kufanya kazi bila kutumia karatasi.
Mhe. Frederick Manyanda anachukua nafasi ya Mhe. Dkt. Deo John Nangela aliyeteuliwa hivi karibuni kuwa Jaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania.
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Mustapher Mohamed Siyani (kulia) akimpatia zawadi Jaji Mfawidhi mpya wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Sumbawanga, Mhe. Frederick ambaye ameagwa leo tarehe 25 Februari, 2025 na Watumishi wa Masjala Kuu baada ya kuhamishiwa katika Kanda hiyo.
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Mustapher Mohamed Siyani (aliyesimama) akizungumza jambo wakati wa hafla fupi ya kumuga Jaji Frederick Manyanda (wa pili kushoto) aliyehamishiwa Mahakama Kuu Kanda ya Sumbawanga. Wa pili kulia ni Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Kuu, Mhe. Upendo Madeha na wa kwanza kulia ni Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Kuu, Mhe. Abdi Kagomba.
Aliyekuwa Msaidizi wa Ofisi wa Jaji Manyanda, Bi. Sinahila akizungumza jambo wakati wa hafla hiyo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni