Na BAKARI MTAULLAH-Dar es Salaam
Viongozi wa Mahakama Kanda ya Dar es Salaam tarehe 22 Februari, 2025
walikutana kufanya tathmini ya malengo na mipango ya utendaji kazi
waliyojiwekea kwa mwaka 2024 na kuweka malengo mapya ya mwaka 2025.
Kikao hicho ambacho ni cha tatu kutoka kuanzishwa utaratibu huo,
kilifanyika katika ukumbi wa White Sand Hotel Jijini Dar-es-salaam
kikihudhuriwa na Majaji nane, Naibu Wasajili wanne, Mtendaji wa Mahakama na Maofisa wa kada za utumishi na Teknolojia
ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) kutoka Kanda hiyo.
Akizungumza wakati anafungua kikao hicho, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya
Tanzania, Kanda ya Dar-es-Salaam, Mhe. Salma Mussa Maghimbi aliwashukuru
wajumbe kwa kuhudhuria na kuwasihi kushiriki kikamilifu kufanya tathmini katika
mipango waliyojiwekea na kujiuliza nini cha kufanya kwa yale ambayo
hawakufanikiwa.
“Sote tulikuwepo mwaka jana 2024 na bahati nzuri sote tupo kwenye kikao
hiki, tumekuja kujitathimini katika mipango tuliyojiwekea na kupanga jinsi gani
tunatoka hapa kwenda mbele zaidi…
“…Tufanye tathmini katika yale ambayo hayakufanyika vizuri na lazima
tujiulize kwa nini. Tumefanyaje kazi na kama malengo yetu tumeyafikia, na kama
yamefikiwa ni kwa kiasi gani, na kama hayakufikiwa ni kwa kiasi gani,” alisema.
Jaji Mfawidhi aliwapongeza wajumbe wa kikao hicho kwa mafanikio makubwa
yaliyopatikana kwani wameweza kuvuka malengo waliyokuwa wamejiwekea kwa mwaka
2024. Alitaja mafanikio hayo kubwa ikiwa ni kuvuka mwaka 2024 na mashauri tisa
tu ya mlundikano, sawa na asilimia 0.7, ikilinganishwa na mwaka 2023 ambapo
mashauri 48 ya mlundikano, sawa na asilimia 3 ndio yaliyovuka mwaka.
Alieleza kuwa mwelekeo uliopo kwa sasa katika Kanda hiyo ni sawa na kushuka
mlima, akitolea mfano upande wa mlundikano wa mashauri ambao umeendelea
kuporomoka.
Ingawa alitahadharisha kwamba kama hakutakuwepo na usimamizi bora wa
mashauri, upo uwezekano wa kurudi nyuma jambo ambalo hatapenda kuona hali hiyo
ikitokea.
“Changamoto yetu ilikuwa kwenye mashauri ya mlundikano, lakini kwa kazi
mliyoifanya, mwaka 2025 hautakuwa na
mashauri kama hayo. Tunachotaka kwa sasa mashauri yanayoamuliwa yawe mengi
zaidi kuliko yanayosajiliwa, na kwamba tuzuie uwezekano wa mashauri kufikia
hatua ya mlundikano” alisema.
Viongozi hao wa Kanda walijadiliana kuhusu usimamizi bora wa mashauri ikiwa ni pamoja na utekelezaji wa Waraka Na.1
/2025 wa Jaji Mkuu wa Tanzania kuhusu matumizi ya TEHAMA katika usimamizi wa
mashauri, mpango wa vikao vya mashauri ya jinai na mashauri ya madai kwa mwaka
2025.
Kadhalika, walijadiliana kuhusu mpango wa Ukaguzi wa Mahakama na Magereza
na pia tathmini ya utekelezaji wa bajeti
ya mwaka 2024/2025 pamoja na maoteo ya mwaka 2025/2026.
Pamoja na mambo mengine, kikao hicho kilitoka na maazimio yakiwemo kuongeza kasi ya matumizi ya mifumo mbalimbali ya TEHAMA ili kuboresha utendaji kazi na kuzuia uzalishaji wa mashauri mlundikano.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Salma Maghimbi (katikati-akisisitiza jambo alipokuwa anazungumza kwenye kikao hicho.
Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania kutoka Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Butamo Philip akisisitiza jambo kwenye mkutano huo.
Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania kutoka Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Elizabeth Mkwizu akieleza jambo kwenye mkutano huo.
Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania kutoka Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Arnold Kirekiano akichangua hoja kwenye mkutano huo.
Majaji wa Mahakama Kuu na Naibu Wasajili wakifuatilia yaliyokuwa yanajiri katika mkutano.
Naibu Wasajili na Mtendaji wa Mahakama Kanda ya Dar es Salaam wakiwa kwenye
mkutano huo.
(Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dar es Salaam)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni