Jumatatu, 24 Februari 2025

MFUMO WA e-JOPRAS WAWAFIKIA MAHAKIMU SUMBAWANGA

Na Fredrick Mahava – Mahakama, Sumbawanga

Mahakimu Kanda ya Sumbawanga wamepata mafunzo ya mfumo wa kidigitali wa tathimini na mapitio ya utendaji (e-JOPRAS) ikiwa ni jitihada za kuongeza utendaji kazi.

Mafunzo hayo yalifunguliwa na Kaimu Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu, Kanda ya Sumbawangu Mhe. Dkt. Thadeo Mwenempazi tarehe 21 Februari, 2025 ambayo yalifanyika katika Ukumbi wa Mahakama Kuu.

Mafunzo hayo yaliendeshwa na Afisa TEHAMA wa Mahakama Kuu Sumbawanga Bw. Mayanga Someke aliyewajengea uwezo wa namna  ya kutumia mfumo wa  e-JOPRAS katika majukumu yao ya kila siku na namna ya kujaza taarifa zao kwenye mfumo huo kwa ufanisi. Mahakimu hao walipata uelewa wa namna mfumo huo unavyofanya kazi kwa vitendo.

Aidha, kabla ya mafunzo hayo, yalitanguliwa na kikao cha watumishi wa Mahakama Kuu, Kanda ya Sumbawanga na Katavi ambao walipewa mrejesho wa mambo mbalimbali ambayo yalitokana na kikao cha mapitio ya utekelezaji wa bajeti ya mwaka 2024/2025 kwa kipindi cha nusu mwaka na maandalizi ya bajeti ya mwaka 2025/2026 kilichofanyika Dodoma.

Akizungumza wakati wa kikao hicho Mtendaji wa Mahakama Kuu, Kanda ya Sumbawanga Bw. Machumu Essaba  alitoa taarifa  ya  bajeti ya mwaka fedha 2025/2026 kwa Mahakama  zilizopo mkoa wa Rukwa na pia alitoa mrejesho wa maelekezo kutoka kwa Mtendaji Mkuu  kuhusu utekelezaji.

Vilevile, Naibu Msajili wa Mahakama Kuu, Kanda ya Sumbawanga Mhe. Joseph Luambano alitoa msisitizo juu ya matumizi ya TEHAMA katika usikilizaji wa mashauri na kuzingatia nyaraka mbalimbali zilizotelewa na Jaji Mkuu, Jaji Kiongozi na Msajili Mkuu. Pia aliwaomba watumishi kuendelea kusimamia mikakati iliyowekwa ambayo ilisaidia kupunguza mlundikano wa mashauri.

Naye, Kaimu Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu, Kanda ya Sumbawanga Mhe. Dkt. Thadeo Mwenempazi pamoja Jaji wa Mahakama Kuu, Kanda ya Sumbawanga Mhe. Abubakar Mrisha, Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Sumbawanga Mhe. Joseph Luambano na Mtendaji wa Mahakama Kuu, Kanda ya Sumbawanga Bw. Machumu Essaba waliungana na Mahakimu kupata mafunzo hayo.

Kaimu Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu, Kanda ya Sumbawanga Mhe. Dkt. Thadeo Mwenempazi akifungua mafunzo ya e-JOPRAS kwa Mahakimu katika Ukumbi wa Mahakama Kuu Sumbawanga

Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Sumbawanga Mhe. Joseph Luambano akisisitiza jambo kwa Mahakimu hao wakati wa mafunzo.

Mtendaji wa Mahakama Kuu, Kanda ya Sumbawanga Bw. Machumu Essaba akitoa mrejesho wa kikao cha Bajeti kilichofanyika jijini Dodoma hivi karibuni

Mahakaimu wakifuatilia kwa makini Mafunzo ya Mfumo wa e-JOPRAS

Majaji na Mahakaimu wakifuatilia kwa makini Mafunzo ya Mfumo wa e-JOPRAS


Afisa TEHAMA wa Mahakama Kuu Kanda ya Sumbawanga Bw. Mayanga Someke akiendesha Mafunzo hayo kwa Mahakimu.


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni