Jumatatu, 24 Februari 2025

WATUMISHI MANYARA WAFANYA UTALII NGORONGORO

Na Christopher Msagati – Mahakama, Manyara

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Manyara Mhe. John Rugalema Kahyoza, amewaongoza watumishi wa Mahakama Kanda hiyo, kufanya ziara ya utalii iliyofanyika mnamo tarehe 22 Februari, 2025 katika Hifadhi ya Bonde la Ngorongoro (Ngorongroro Crater) mkoani Arusha.

Akizungumza na watumishi kwa nyakati tofauti wakati wa maandalizi na hitimisho la ziara hiyo, Mhe. Kahyoza alieleleza lengo la ziara hiyo ni kutambua maeneo mapya ambayo watumishi wengi hawajawahi kuyafikia, kupata furaha na kuimarisha afya ya akili.

“Muda mrefu tunakaa ofisini tukiwa tunashughulika na majukumu ya usikilizwaji wa mashauri bila kupata fursa ya kufahamu masuala mengine mengi ambayo tunapaswa kuyafahamu. Hili jambo linaweza kupunguza ufanisi wa utendaji kazi kama tunakosa muda wa kuwaza masuala mengine nje ya kazi, ziara hii ya Ngorongoro ituwezeshe kuwa na mtazamo mpya lakini pia kuyafahamu maeneo ambayo yanatuzunguka,” alisema Mhe. Kahyoza.

Kwa upande wake, Jaji wa Mahakama Kuu, Kanda ya Manyara Mhe. Devotha Kamuzora aliwapongeza watumishi wote waliofanikiwa kushiriki ziara hiyo na kuwashauri watumishi kuendelea kushirikiana katika masuala kama hayo yanapojitokeza kwa kuwa pia yanaongeza upeo wa ufahamu ambao unaimarisha utendaji kazi.

“Nawapongeza watumishi wote (Watalii wenzangu) waliofanikiwa kusafiri kwa ajili ya utalii na nawashauri siku nyingine ziara kama hii ikitokea tuungane sote kwa pamoja kwa kuwa tutakuwa tumeongeza kitu kikubwa sana katika upeo na ufahamu wetu na kuboresha ufanisi wa kazi pia,” alisema Mhe. Kamuzora.

Vilevile, Mhe. Kahyoza aliwashukuru watumishi wa Mahakama ya Wilaya ya Karatu kwa kushirikiana nao bega kwa bega katika maandalizi ya safari hiyo ya kuelekea Ngorongoro.

Watumishi 66 wa Kada tofauti kutoka Mahakama za ngazi mbalimbali wakiwemo Mahakimu Wakazi wafawidhi wa Wilaya zilizopo katika Kanda ya Manyara, Mahakimu wengine na Mtendaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Manyara walishiriki ziara hiyo ikiwa ni muendelezo wa kuendelea kutambua vivutio vya asili vilivyo ndani na nje ya Mkoa wa Manyara pamoja na kuwafanya watumishi kuendelea kuishi kwa umoja na kwa ushirikiano.

Watumishi wa Mahakama Kuu Kanda ya Manyara wakiwa katika picha ya Pamoja katika ziara ya Hifadhi ya Taifa ya Ngorongoro.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Kanda ya Manyara Mhe. John Kahyoza (wa kwanza kulia) akiwa katika picha ya Pamoja na baadhi ya watumishi wa Mahakama Kuu, Kanda ya Manyara katika ziara ya Hifadhi ya Taifa Ngorongoro.

Jaji wa Mahakama Kuu, Kanda ya Manyara Mhe. Devotha Kamuzora akifurahia jambo wakati wa ziara ya Utalii iliyofanywa na watumishi wa Mahakama Kuu Manyara katika Hifadhi ya Taifa ya Ngorongoro.

Moja wapo ya Mabwawa ambayo wanaishi viboko katika Hifadhi ya Taifa ya Ngorongoro.

Pundamilia wakionekana katika Eneo la Ngorongoro Crater wakati wa ziara ya Hifadhi ya Taifa Ngorongoro iliyofanywa na watumishi wa Mahakama Kuu Kanda ya Manyara.

Tembo akionekana katika Eneo la Ngorongoro Crater wakati wa ziara ya Hifadhi ya Taifa Ngorongoro iliyofanywa na watumishi wa Mahakama Kuu Kanda ya Manyara.





 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni