Jumamosi, 22 Februari 2025

MAJAJI, MAHAKIMU KANDA YA DODOMA WAPIGWA MSASA MATUMIZI YA MIFUMO

Na ARAPHA RUSHEKE- Mahakama, Dodoma.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dodoma, Mhe. Dkt. Juliana Masabo amefungua mafunzo kuwajengea uelewa Majaji na Mahakimu wa Mahakama katika Kanda ya Dodoma program maalumu ya ushauri wa kitaaluma na mfumo wa upimaji na kutathimini utendaji kazi.

Akizungumza wakati wa kufungua mafunzo hayo ya siku moja yaliyofanyika jana tarehe 21 Februari, 2025 katika Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki Dodoma, Mhe Dkt Masabo alisema kuwa programu hiyo (mentarship program) ambayo imeanzishwa ina malengo mengi, ikiwemo kuwajengea uwezo Majaji na Mahakimu katika kazi.

“Kama Viongozi tunajukumu la kuwasaidia watu wetu wa chini na kuwajengea uwezo, kwa muktadha huo tukitumia vizuri mafunzo haya yatatujengea uwezo na ufanisi mkubwa katika kazi zetu,” alisema Dkt. Masabo.

Jaji Mfawidhi aliwasisitiza Mahakimu kuzingatia maadili ya kazi zao ili waweze kutekeleza majukumu yao ya utoaji haki kwa ufanisi unaotakiwa bila kufanya upendeleo wa aina yeyote kwa wateja wao.

Akizungumza wakati wa mafunzo hayo, Mwezeshaji wa eneo la kitaaluma (mentorship) ambaye pia ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanaania, Kanda ya Mtwara, Mhe. Edwin Kakolaki aliwataka washiriki kuhakikisha wanatoka na ujuzi na uwelewa utakaowasaidia kuongeza ufanisi katika uotaji wa huduma kwa Wadau na umma kwa ujumla.

Naye Ofisa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) wa Mahakama Kuu Kanda ya Dodoma, Bw. Omary Mkadama alitoa elimu ya mifumo ya kielektroniki namna ya utumiaji wa mifumo kama eJOPRAS, eCMS na Data Hub kwa Mahakimu na kueleza umuhimu katika kutathimini utendaji kazi wao wa kazi na kupata mrejesho wa kile wanafanyia kazi kila siku.

Aidha, Mahakimu hao walishauriwa kushirikiana kwa ukaribu na Wadau wengine wa mfumo wa haki ili kuimarisha utoaji wa haki kwa Wananchi kwa njia endelevu na yenye uwazi zaidi.

Katika maboresho ya utendaji kazi kwa watumishi wa Mahakama, Mahakama Kuu Kanda ya Dodoma ililazimika kuendesha mafunzo maalumu kwa Majaji na Mahakimu katika matumizi mbalimbali ya mifumo ya kielektroniki ikiwa ni jitihada za kuongeza ufanisi kwenye kazi.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dodoma(katikati) Mhe. Dkt. Juliana Masabo na kushoto kwake  ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Mtwara, Mhe. Edwin Eliasi Kakolaki ambaye ni Mwezeshaji wa Mafunzo hayo na kulia kwake ni Jaji wa Mahakama Kuu Dodoma, Mhe. Dkt. Fatma Khalfan.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Mtwara, Mhe. Edwin Eliasi Kakolaki akiwasilisha mada wakati wa mafunzo hayo.

Ofisa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) wa Mahakama Kuu Dodoma, Bw.Omari Mkadama ambaye ni mwezeshaji akiwasilisha mada wakati wa mafunzo hayo.

 

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dodoma, Mhe. Dkt. Juliana Masabo (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na washiriki wa mafunzo hayo waliowakilisha Mkoa wa Dodoma.

 

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dodoma, Mhe. Dkt. Juliana Masabo (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na washiriki wa mafunzo hayo waliowakilisha Mkoa wa Singida.

(Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dar es Salaam)

 

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni