Ijumaa, 21 Februari 2025

MAHAKAMA KUU DODOMA YAMUAGA JAJI KAKOLAKI

Na ARAPHA RUSHEKE-Mahakama Kuu, Dodoma

Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dodoma imefanya hafla fupi  ya kumuaga aliyekuwa Jaji wa Mahakama Kuu Dodoma, Mhe. Edwin Eliasi Kakolaki, ambaye amehamishiwa Mahakama Kuu Kanda ya Mtwara kuwa Jaji Mfawidhi.

Hafla hiyo ilifanyika jana tarehe 20 Februari, 2025 katika Ukumbi wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki Dodoma na kuhudhuriwa na Majaji, Viongozi na Watumishi wengine.

Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Mhe. Kakolaki aliwashukuru Watumishi wa Mahakama Dodoma kwa ushirikiano na upendo mkubwa waliompatia wakati akiwa katika Kanda hiyo.

Aliongeza kwamba alikuwa na furaha ya kufanya kazi na timu imara na yenye ufanisi wa hali ya juu ambao ulimwezesha kutekeleza majukumu yake bila kikwazo chochote.

"Nimefurahi sana kufanya kazi na timu hii ya Mahakama Kuu Dodoma, ushirikiano wenu na upendo mkubwa mlionionyesha umenisaidia kutekeleza majukumu yangu bila kikwazo chochote…

“…kwa kweli Dodoma ni eneo nililoishi kwa amani sana, ni eneo ambalo watu wana upendo, ninawashukuru kila mmoja kwa nafasi yake kwa sababu mmekuwa mchango mkubwa katika maisha yangu, nawapenda sana asanteni," alisema Mhe. Kakolaki.

Kwa upande wake, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dodoma, Mhe. Dkt. Juliana Masabo, kwa niaba ya Watumishi wote, alimpongeza Jaji Kakolaki kwa kuaminiwa na kukasimiwa mamlaka ya kusimamia Kanda ya Mahakama Mtwara.

“Hongera sana, tunaungana na wewe kumshukuru Mungu kwa namna ambavyo amekulinda, amekutunza na kwa mema yote ambayo amekutendea, lakini zaidi kwa namna ambavyo amekuona kama unafaa na kutoa kibali ili uweze kusimamia Kanda ya Mtwara,” alisema.

Mhe. Dkt. Masabo alitumia fursa hiyo kumshukuru Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahimu Hamis Juma na Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Mustapher Mohamed Siyani kwa imani waliyoionesha na kumteua Mhe. Kakolaki kuwa Jaji Mfawidhi katika Mahakama Kanda ya Mtwara.


 Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Mtwara, Mhe. Edwin Eliasi Kakolaki akiwa katika uso wa bashasha katika hafla fupi ya kumuaga iliyofanyika katika Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki Dodoma.


Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Mtwara, Mhe Edwin Eliasi Kakolaki (katikati) akikata keki aliyoandaliwa katika hafla hiyo. Kulia kwake ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dodoma, Mhe. Dkt. Juliana Masabo na kushoto kwake ni Jaji wa Mahakama Kuu Dodoma, Mhe. Dkt. Fatma Khalfan.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Mtwara, Mhe. Edwin Eliasi Kakolaki akiwa katika uso wa bashasha mara baada ya kupokea moja ya zawadi kutoka kwa Watumishi wa Mahakama Kuu Dodoma. Picha chini akipokea zawadi nyingine kutoka kwa Watumishi.



Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dodoma, Mhe. Dkt. Juliana Masabo (kulia) akimpatia zawadi Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Mtwara, Mhe. Edwin Eliasi Kakolaki kama ishara ya shukrani na heshima kwa mchango wake mkubwa alioutoa akiwa Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Dodoma.

 

Baadhi ya Watumishi wa Mahakama Kuu Dodoma wakiwa katika picha ya pamoja wakati wa hafla hiyo.

Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dar es Salaam.

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni