Na JOVINE BISHANGA -Mahakama, Kigali
Mkutano wa Tatu wa
Mwaka wa Mahakama ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (the East African Court of
Justice) unaowaleta viongozi mbalimbali wa Mahakama katika nchi hizo umeanza
leo tarehe 18 Februari, 2025 nchini Rwanda kujadili mada mbalimbali zinazolenga kuimarisha huduma
za utoaji haki kwenye ukanda huo.
Viongozi wa Mahakama
ya Tanzania wanaoongozwa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya
Dar es Salaam, Mhe. Salma Maghimbi, ambaye amemwakilisha Jaji Mkuu wa Tanzania,
Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma, wamehudhuria ufunguzi wa Mkutano huo wa siku
mbili unaofanyika katika hoteli ya Marriott iliyopo jijini hapa.
Viongozi wengine wa
Mahakama ya Tanzania wanaoshiriki Mkutano huo ni Jaji Mfawidhi wa
Mahakama Kuu ya Tanzania, Kituo cha Usuluhishi Dar es Salaam, Mhe. Zahra Abdallah
Maruma, ambaye atamwakilisha Mhe. Prof. Juma katika jopo la Majaji Wakuu watakaojadili
na kuhimiza namna bora ya kutatua migogoro kwa njia mbadala (Alternative Dispute Resolution).
Kwa upande mwingine, Jaji wa Mahakama ya Rufani ya
Tanzania, Mhe. Omar Othman Makungu, ambaye pia ni Jaji wa Mahakama ya Jumuiya
ya Afrika Mashariki pamoja na Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, ambaye pia ni
Jaji Kiongozi wa Mahakama ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, Mhe. Yohane Bokobora
Masara, wanashiriki pia katika Mkutano huo muhimu.
Kadhalika, Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Eva
Kiaki Nkya na Katibu wa Msajili Mkuu, Mhe. Dkt. Jovine
Costantine Bishanga ni miongoni mwa Viongozi wa Mahakama kutoka Tanzania
wanaohudhuria Mkutano huo.
Mkutano huo wenye kauli mbiu “Justice, Ethics and Enforcement
of Decisions: A Judicial Pathway for Regional Development” umefunguliwa na
Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Rwanda, Mhe. Mukantaganzwa kwa niaba ya Rais wa Jamhuri
ya Rwanda, Mhe. Paul Kagame, ambaye amehimiza wanachama wa Jumuiya ya Afrika
Mashariki kuendelea kutekeleza maamuzi yanayotolewa na Mahakama ya Afrika
Mashariki pamoja na kutatua changamoto mbalimbali zinazoikabili.
Mbali na kuhimiza utatuzi wa migogoro kwa njia
mbadala, Mkutano huo pia utajadili mada mbalimbali ikiwa ni pamoja na matumizi
ya Akili Mnemba “Artificial Intelligent” katika shughuli za Mahakama,
sambamba na wajibu wa Mahakama ya Jumuiya ya Afrika Mashariki katika kushughulikia
mashauri ya haki za binadamu na kuimarisha utangamano wa Jumuiya ya Afrika
Mashariki.
Wadau mbalimbali wa Mahakama ya Jumuiya ya Afrika
Mashariki ikiwa ni pamoja na Viongozi wa Serikali kutoka Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, akiwemo Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
anayeshughulikia masuala ya Afrika Mashariki, Mhe. Dennis Lazaro Londo, pamoja na
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
anayeshughulikia masuala ya Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Stephen Mbundi, nao
wanahudhuria Mkutano huo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni