- Msajili Mkuu akiri Maonesho ya mwaka huu yameleta tija
- Maadhimisho ya kilele cha Siku ya Sheria kufanyika tarehe 03 Februari mwaka huu
Na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma
Maonesho ya Wiki ya Sheria yaliyokuwa yakifanyika nchi nzima yamefikia tamati leo tarehe 01 Februari, 2025 ambapo Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Eva Kiaki Nkya ameeleza kuwa, maonesho hayo yamekuwa ya tija na yamewafikia wanachi wengi zaidi.
Akizungumza leo wakati akifunga Maonesho hayo yaliyofanyika Kitaifa katika Viwanja vya Nyerere ‘Square’ jijini Dodoma, Mhe. Nkya amesema utaratibu mpya wa maadhimisho ya wiki ya sheria kwa mwaka huu uliwezesha watumishi wa Mahakama pamoja na wadau kuwatembelea wananchi katika maeneo yao ya kazi na kuwapa elimu.
“Tathmini yetu, imeonesha kwamba utaratibu wa kuwafuata wananchi katika maeneo yao ya kazi unaleta tija na tumeweza kufikia wanachi wengi zaidi,” amesema Mhe. Nkya.
Ameeleza zaidi kuwa, Mahakama na wadau si tu kwamba walitoa elimu katika viwanja vya maonesho pekee, bali pia walifanikisha utoaji wa elimu katika maeneo mengine ambako Mahakama iliwafuata wananchi moja kwa moja. Maeneo yaliyotembelewa ni pamoja na Machinga Complex, Mnada Mpya, Sabasaba, na Stendi ya Mabasi Nanenane.
Mhe. Nkya amebainisha pia kuwa, wakati maonesho hayo yakiendelea timu ya Mahakama kwa kushirikiana na wadau walitoa elimu kwa wanafunzi wa Shule za Msingi Kilimani, Makole, Chimwanio, Kizota, Chang’ombe, Amani, Mbwanga, Kendege na Chinangali na Shule za Sekondari za Dodoma, Lukundo, Ntyuka, Nzunguni, Viwandani, Michese, Jhon Merlin, Al Qaem Seminary, na Shule ya Wasichana Huruma, ambapo wanafunzi hao walipata fursa ya kujifunza kuhusu Mahakama pamoja na huduma zinazotolewa na Mahakama.
Ameongeza kuwa, hatua hiyo ni utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Mahakama wa mwaka 2020/2021-2024/2025, hususani nguzo ya tatu ya kurejesha imani ya wananchi na ushirikishwaji wa wadau.
Aidha, Msajili Mkuu amesema kwamba, kwa upande wa Mahakama, ilitolewa elimu ya jinsi ambavyo Mhimili huo unavyotumia Teknolojia ya Habari na Mawasilano (TEHAMA) katika kuboresha huduma zake, jinsi ya kupata maoni, mirejesho na malalamiko na namna ambavyo yanashughulikiwa kupitia Kituo cha Huduma kwa Mteja cha Mahakama.
Amebainisha kuwa, jumla ya malalamiko 64 yameshughulikiwa kwa ukamilifu katika ngazi zote za Mahakama nchini, ameongeza kwa kueleza kuwa, “tumetoa pia elimu kuhusu utaratibu wa ufunguaji na uendeshaji wa mashauri mbalimbali kama mirathi, ndoa, talaka na kuasili, maboresho ya Mahakama, mchango wa Mahakama katika kuboresha au kurekebisha sheria na kanuni, na utekelezaji wa amri na tuzo za Mahakama.
Ameeleza kwamba, Mahakama ya Tanzania inaendelea na maboresho ya huduma zake kwa kushirikiana na wadau ili kufikia Dira yake ya kutoa haki sawa kwa wote na kwa wakati. Amesisitiza kuwa, “lengo letu ni kuendelea kuongeza ufanisi na pia kusogeza huduma karibu na wananchi na kuchangia katika ustawi wa kiuchumi, kijamii na kisiasa katika taifa letu.”
Amewashukuru wananchi pamoja na wadau walioshirikiana pamoja na Mahakama ya Tanzania kwa kufanikisha kufanyika kwa Maonesho hayo.
Akitoa taarifa fupi ya Maonesho ya Wiki ya Sheria kwa mwaka huu, Naibu Msajili wa Mahakama ya Rufani na Katibu wa Kamati ya Maandalizi ya Wiki ya Sheria, Mhe. Charles Magesa amesema hadi kufikia tarehe 01 Februari, 2025 jumla ya wananchi 3,394 wametembelea mabanda mbalimbali ya maonesho hayo.
“Kwa upande wa elimu mashuleni, elimu ilitolewa katika shule mbalimbali za mkoa wa Dodoma ikiwa ni pamoja na shule ya msingi ya Kilimani, Makole, Chamwino, Kizota, Chang’ombe, Amani, Kiwanja cha Ndege, Mbwanga, Mlimwa na Chinangali. Katika shule hizo jumla ya wanafunzi na walimu 13,979 wamenufaika na elimu ya sheria kwa mwaka huu,” amesema Mhe. Magesa.
Katika Maonesho hayo jumla ya wadau 39 wameshiriki pamoja na Mahakama, Wadau hao ni pamoja na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Madawa ya Kulevya, Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Tume ya Kurekebisha Sheria, Tume ya Utumishi ya Mahakama, Mamlaka ya Mkemia Mkuu Wa Serikali, Tume ya Usuluhishi na Uamuzi, Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu, Chama cha Wanasheria Wanawake Tanzania (TAWLA), Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Wizara ya Katiba na Sheria na nyingine.
Maonesho ya Wiki ya Sheria nchini mwaka 2025 yalizunduliwa mnamo tarehe 25 Januari, 2025 na Rais Mstaafu, Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete kwa matembezi na mbio maalumu za kilometa 5 na Kilometa 10.
Maadhimisho ya Kilele cha Siku ya Sheria yatafanyika tarehe 03 Februari, 2025 ambapo Mgeni Rasmi anatarajiwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Maadhimisho hayo ambayo yatafanyika kitaifa katika Viwanja vya Chinangali jijini Dodoma.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni