-Wadau walioshirikiana na Mahakama katika maadhimisho wapewa vyeti vya ushiriki
-Kanda ya Musoma yang’ara katika Bonanza la Mahakama za Kanda ya Ziwa kuashiria kuhitimishwa kwa maonesho ya Wiki ya Sheria
Na KANDANA LUCAS -Mahakama, Musoma
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Musoma, Mhe. Fahamu Hamidu Mtulya, amehitimisha Maonesho ya Wiki ya Sheria katika Kanda ya Musoma kwa kutoa vyeti vya ushiriki kwa wadau wa Mahakama walioshiriki kutoa elimu katika maeneo mbalimbali.
Akizungumza na wadau hao wakati wa kikao cha majumuisho, Mhe. Mtulya aliwapongeza kwa ushiriki wao katika Maonesho ya Wiki ya Sheria ambapo elimu kwa umma kuhusu masuala mbalimbali ya kisheria ilitolewa katika maeneo ya wazi (viwanja), taasisi za elimu na kupitia vyombo vya habari kuanzia tarehe 25. Januari hadi tarehe 01Februari, 2025.
“Nichukue nafasi hii kuwapongeza sana wadau wetu wote mlioshirikiana na sisi Mahakama kutoa elimu kwa umma katika Maonesho ya Wiki ya Sheria 2025. Kwa kutambua ushiriki wenu, Mahakama Kuu Kanda ya Musoma, imeandaa utaratibu wa kutoa vyeti vya ushiriki ambavyo vitakabidhiwa kwa wawakilishi wa taasisi zilizoshiriki,” alisema Mhe. Mtulya.
Kwa upande mwingine, Kanda ya Musoma imeng’ara katika Bonanza la michezo kwa ajili ya kuhitimisha maonesho hayo, lililofanyika tarehe 01Februari.2025 jijini Mwanza likihusisha Kanda tatu za Mahakama ambazo ni Mwanza, Musoma na Shinyanga.
Katika michezo yote, Kanda ya Musoma iliibuka mshindi wa jumla kwa kutwaa makombe matatu kati ya manne yaliyokuwa yameandaliwa pamoja na zawadi za mchezaji mmoja mmoja.
Michezo ambayo Musoma waliibuka washindi wa kwanza ni pamoja na mchezo wa kamba wanaume na wanawake, Mpira wa pete, mchezo wa karata, kukimbiza kuku,kete/draft(wanaume), mchezo wa kukimbia na yai kwenye kijiko (wanaume na wanawake) na kukimbia kwenye magunia (wanaume na wanawake).
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, Majaji Wafawidhi wa Mahakama zilizoshiriki ambao ni Mhe. Dkt Ntemi Kilekamajenga (Kanda ya Mwanza), Mhe. Mtulya (Kanda ya Musoma) na Mhe. Frank Mahimbali (Kanda ya Shinyanga), walipongeza ushirikiano uliofanikisha bonanza hilo na kuahidi kuendeleza utaratibu wa kufanya michezo ya pamoja ili kujenga afya na kupunguza msongo wa mawazo kwa watumishi.
8. Timu ya kamba wanaume kutoka Musoma (wazee wa kichuri) wakichuana vikali na timu ya kamba wanaume kutoka Shinyanga (hawapo pichani).
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Mwanza, Mhe. Ntemi Kilekamajenga akitoa neno kwa washiriki wa bonanza katika Viwanja vya Nyamagana.
Mshindi wa mchezo wa kete (draft) Bw. Rukojo Magara Torokoko kutoka Kanda ya Musoma akionesha ufundi wake
Washindi wa mchezo kukimbiza kuku kutoka Kanda ya Musoma wakifurahia.
(Habari hii imehaririwa na MAGRETH KINABO-Mahakama Dodoma)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni