Jumatatu, 3 Februari 2025

RAIS SAMIA AONGOZA WATANZANIA KUADHIMISHA SIKU YA SHERIA 2025

Na FAUSTINE KAPAMA -Mahakama, Dodoma

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan leo tarehe 3 Februari, 2025 amewaongoza Watanzania kuadhimisha Siku ya Sheria na kuipongeza Mahakama ya Tanzania kwa kwa mafanikio makubwa ambayo imeendelea kuyapata chini ya Uongozi wa Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma.

Mhe. Dkt. Samia amesema Mahakama ya Tanzania imekuwa kinara kwenye matumizi bora ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) barani Afrika na kuendelea kuwa mfano wa kuigwa kwa uchapaji na upandishaji wa hukumu kwa haraka kwenye Mfumo wa Taarifa za Maamuzi, Sheria na Kanuni za Tanzania (TanzLII).

Rais Samia aliwasili katika Viwanja vya Chinangali majira ya saa 3:40 hivi asubuhi na kupokelewa na mwenyeji wake, Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma pamoja na Viongozi wa Mahakama na Serikali.

Baada ya kufika jukwaa kuu, Wimbo wa Taifa na ule wa Afrika Mashariki ulipigwa kabla ya Mshereheshaji Mkuu kwenye maadhimisho hayo, Hakimu Mkazi, Mhe. Mutandzi Akiza Matovelo kuwakaribisha Viongozi wa Dini kuyaweka maadhimisho hayo mbele za Mungu.

Kabla ya Jaji Mkuu wa Tanzania kupanda jukwaani kuongea na Watanzania, Mshereheshaji Mkuu katika maadhimisho hayo alikaribisha kikundi cha Kwaya ya Mahakama, maarufu Ng’aring’ari ambacho kilikonga nyoyo za Rais na wananchi waliokuwa wamefurika katika Viwanja vya Chinangali.

Baadhi ya Viongozi na wananchi wengine walishindwa kujizuia, wakaamua kuachia viti vyao na kuwatunza waimbaji hao kufuatia burudani safi ya nyimbo iliyokuwa inatolewa na kwaya hiyo.

Nyimbo za Kwaya ya Mahakama, hususan zinazoelezea kauli mbiu ya maadhimisho ya Siku ya Sheria mwaka 2025 na mambo mengine ya kimahakama, zimewaacha Wananchi, akiwemo Mkuu wa Nchi wakitabasamu muda wote kutokana na ujumbe bora na burudani safi iliyokuwa inatolewa.

Wakati anazungumza na Taifa kwenye maadhimisho hayo yaliyokuwa yanarushwa mubashara na vituo mbalimbali vya runinga, Rais Samia alisema, “Kwa kweli Kwaya mmefanya mambo yenu. Hongereni sana. Huwa siyo rahisi kuwaburudisha Majaji, lakini Kwaya mmeweza kwa sababu nilikuwa naona sura za Majaji zilivyokuwa.”

Katika kukamilisha maadhimisho hayo ya Siku ya Sheria yanayoashiria mwaka mpya wa shughuli za kimahakama, Jaji Mkuu wa Tanzania alikagua gwaride maalumu lililokuwa limeandaliwa na Jeshi la Polisi kwa heshima yake na kwa ajili ya shughuli hiyo.

Maadhimisho hayo yaliyofanyika Kitaifa katika Viwanja vya Chinangali jijini hapa yamehudhuriwa na Viongozi mbalimbali wa Mahakama, akiwemo Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma na Majaji wa Mahakama ya Rufani.

Alikuwepo pia Jaji Mkuu wa Zanzibar, Mhe. Khamis Ramadhan Abdalla, Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Mustapher Mohamed Siyani, Majaji wa Mahakama Kuu, Mtendaji Mkuu wa Mahakama, Prof. Elisante Ole Gabriel na Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Eva Kiaki Nkya.

Wageni wengine walikuwa Spika wa Bunge la Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Tulia Ackson, Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mhe. Hamza Johari, Katibu Mkuu Kiongozi, Mhe. Dkt. Moses Kusiluka, Makatibu Wakuu, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama, Wakuu wa Wilaya, Viongozi wastaafu wa Mahakama na Serikali, Rais wa Chama cha Mawakili Tanganyika (TLS), Bw. Boniface Mwabukusi na Wananchi kwa ujumla.

Viongozi wengine waliohudhuria maadhimisho hayo ni Makamishna wa Tume ya Utumishi wa Mahakama, Katibu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Baraka Leonard, Rais wa Mahakama ya Afrika Mashariki, Mhe. Nestory Kayobera, Menejimenti ya Mahakama ya Tanzania, Viongozi wa Mahkama Zanzibar, Mkurugenzi wa Mashtaka, Wakili Mkuu wa Serikali, Viongozi wa Dini na Mila na Wakuu wa Taasisi mbalimbali za umma.

 

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akiwasili katika Viwanja vya Chinangali Dodoma kwa ajili ya maadhimisho ya Siku ya Sheria, leo tarehe 3 Februari, 2025.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akiwa katika Jukwaa Kuu baada ya kuwasili kwenye maadhimisho hayo. Picha chini, Meza Kuu ikishiriki kuimba Wimbo wa Taifa na Wimbo wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Majaji wa Mahakama ya Rufani na Mahakama Kuu ya Tanzania wakishiriki kuimba Wimbo wa Taifa.

Sehemu ya Jukwaa Kuu ikishiriki kuimba Wimbo wa Taifa na ule wa Afrika Mashariki.

Sehemu ya Wageni waalikwa wakiimba Wimbo wa Taifa na ule wa Afrika Mashariki.

Brass Band ya Jeshi la Magereza ikiwaongoza Watanzania kuimba Wimbo wa Taifa na ule wa Afrika Mashariki kwenye maadhimisho hayo.



Kwaya ya Mahakama ya Tanzania, Ng'aring'ari, ikiwa katika ubora wake (juu na picha mbili chini).



Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akiwaaga Wananchi wakati anaondoka kwenye Viwanja vya Chinangali baada ya Maadhimisho ya Siku ya Sheria.

Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (juu na chini) akikagua gwaride lililokuwa limeandaliwa na Jeshi la Polisi kwa heshima yake na kiashirio cha kuanza mwaka mpya wa shughuli za kimahakama, 2025.

 

Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akipokea heshima kutoka kwa Kiongozi wa Gwaride hilo baada ya ukaguzi.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni