Na INNOCENT KANSHA- Mahakama, Dodoma
Rais
wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) Wakili Msomi Boniface Anyesile
Kajujumele Mwabukusi leo tarehe 03 Februari, 2025 amesema, Chama hicho kinatambua
na kupongeza jitihada kubwa zilizokwisha fanyika na zinazoendelea kufanywa na
Mahakama ya Tanzania za ujenzi wa miundombinu ya kisasa pamoja na uwekezaji
mkubwa katika Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) ili kurahisisha uratibu,
usimamizi, uendeshaji na usikilizwaji wa mashauri na Uwekezaji huo Chama kimeuona
kwa macho na kimetembelea maeneo hayo.
Akizungumza
wakati wa sherehe za kilele cha kuadhimisha siku ya sheria nchini zikiashiria
kuanza kwa mwaka wa kimahakama, zilizofanyika kitaifa katika viwanja vya
Chinangali jijini Dodoma, Wakili Mwabukusi amesema, “Uwekezaji huo ni wa
kipekee na wa kujivunia, ambao hautii shaka hata kidogo ukiwa na nia thabiti ya
kuimarisha mfumo wa utoaji haki nchini. Miundombinu hii inaifanya Mahakama
ifikiwe na watu wote bila kujali umbali au mahali popote alipo mtu,” amesema
Rais wa TLS.
“Chama
kinatoa rai kwamba, wakati Mahakama ikiendelea na maboresho haya tusiwasahau
wanaohusika kule ndani hususani Mahakimu, Mahakimu wanafanya kazi chini kabisa
kule kwa wananchi. Kwa kweli majengo yanavutia sana na teknolojia ni nzuri na ya
kisasa lakini ni vema tuhakikishe tunaboresha maslahi na mazingira yao ya
utendaji kazi. Kwa sababu ni hatari sana mwananchi mwenye shida kukutana na
wakili mwenye msongo wa kipato na Hakimu mwenye msongo wa kipato hapo
anayeshughulikiwa ni mwananchi. Kwa hiyo kuboresha mazingira yao itakuwa zaidi ni
kuwasaidia wananchi,” amesisitiza Wakili Mwabukusi.
Aidha,
akizungumzia Kauli mbiu ya wiki ya sheria na siku ya sheria nchini 2025 inayosema,
‘Tanzania
2050: Nafasi ya Taasisi Zinazosimamia Haki Madai katika Kufikia Malengo Makuu ya
Dira ya Taifa ya Maendeleo’.
Rais
huyo amesema, nampongeza Jaji Mkuu na Mahakama kwa kauli mbiu hiyo imeletwa
muda muafaka, kama ilivyo mwelekeo wa Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2025
ni kuwa na Taifa Jumuishi lenye ustawi, haki na linalo jitegemea pamoja na
mambo mengine dira hiyo inajenga kukuza mfumo wa utawala wa haki na uliyojumuishi.
Msingi
wa dira ni utawala, amani, usalama na utulivu ambapo lengo ni kuwa na mfumo
imara wa kisheria na kitaasisi katika utelekelezaji endelevu wa maendeleo ya
watu na wenye ufanisi.
“Mhe.
Mgeni Rasmi nijaribu kuangalia Dira ya Taifa ya Maendeleo na hali ilivyo ya
kisheria, ni matarajio ya Chama kuwa, wakati tukiendelea kuboresha na kujipanga
tuhakikishe kwamba, tunaweka utaratibu wa kisheria wa kuhakikisha kuwa, sheria
na sera zinazotungwa ziwe katika namna ya ushirikishaji wa kutosha wa wananchi
katika ngazi zote,” amesema Rais Mwabukusi.
Aidha,
Wakili Mwabukusi amesema pia dira ilenge katika kuongeza uwezo wa Taasisi
katika utoaji wa huduma za kisheria kwa wananchi hasa kwa makundi yaliyo pembezoni
na kuondoa mambo yote ya kiufundi na kuweka mkazo katika kutatua migogoro
inayofikishwa mbele ya vyombo vya maamuzi. Kwani mambo ya kiufundi
yanawagharimu sana wananchi na kuchelewesha haki. Hivyo tulenge kuelekea kwenye
utaratibu huo unalenga nafuu ya kisheria kwa wananchi.
Vilevile,
kujenga na kuimarisha ushirikiano wa Serikali na Sekta binafsi kama ambavyo TLS
na Serikali wanavyofanya kazi kwa pamoja kwenye kampeni ya Mama Samia ya msaada
wa kisheria. Kwa hiyo Chama kinaposhirikiana na Serikali siyo kweli kwamba
Chama kinalamba asali. Chama kinapata changamoto wananchi wanapoona
kinashirikiana na Serikali. TLS si kikundi cha magaidi ni chama kilichoanzishwa
kisheria na moja ya kazi yake ni kuwahudumia wananchi kwa kushauri masuala ya
kisheria na kuwawakilisha kwenye vyombo vya kutoa haki.
“Hivyo
TLS itaendelea kutimiza wajibu wake wa kisheria kama kuna sehemu ya kuonya
itaonya kwa haki, kama kuna sehemu ya kupongeza itafanya hivyo kwa haki pia, na
sehemu ya kushiriki kufanya kazi tutashiriki pamoja kulijenga Taifa letu na
kumuhudumia mtanzania,” amefafanua Rais huyo.
Wakati
huo huo Wakili Mwabukusi ameongeza kuwa, dira itilie mkazo katika sheria za
nchi zinazolinda rasilimali, kila taifa lina rasilimali za kulinda kwa Tanzania
kuna ardhi, Mbunga za wanyama, Bahari, mito, maziwa na madini. Sheria, kanuni,
sera na taratibu zinazotungwa zihakikishe zinalinda maeneo hayo kwa wivu mkubwa
kwa sababu ndiyo urithi utako achwa kwa kizazi kijacho kitakacho weza
kushindana na mataifa mengine kiuchumi.
Vilevile,
akifafanua kazi mahususi ya Chama hicho Rais huyo amesema, “Sisi Chama cha
Wanasheria Tanganyika (TLS) tunaongozwa na kifungu cha nne cha sheria ya
Mawakili na mambo yetu ya msingi tunayofanya ni kuimarisha ustawi wa tasnia ya
sheria, kuhamasisha utawala bora na utawala wa sheria, kulinda na kusaidia umma
wa watanzania katika masuala yote yanayohusiana na sheria,” amefafanua.
Wakili
Mwabukusi amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia
Suluhu Hassan, kwa kubuni na kuanzisha kampeni ya msaada wa kisheria yenye
lengo la kuwasaidia wananchi na Chama hicho kimekuwa kikishiriki katika kampeni
hiyo mikoa yote kuwafikia wananchi. Hivyo kupitia programu kama hizo Serikali
inakuwa inakisaidia Chama moja kwa moja, kwani wengi wanaokuwa na matatizo ya
kisheria ni wananchi ambao hawana namna yoyote ile ya kupata huduma ya mawakili
kulingana na uwezo wao wa kiuchumi na maeneo waliko, wengi wao wamekuwa
wakisaidiwa na kufikiwa.
“Kwa hiyo huduma hii ya Mama Samia ya msaada wa kisheria iwe endelevu na tuone namna ya kuiboresha zaidi iwe endelevu na ya kudumu,” ameongeza Wakili Mwabukusi.
Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) Wakili Msomi Boniface Anyesile Kajujumele Mwabukusi leo tarehe 03 Februari, 2025 akitoa hotuba kwa niaba ya chama hicho wakati wa sherehe za kilele cha kuadhimisha siku ya sheria nchini zikiashiria kuanza kwa mwaka wa kimahakama, zilizofanyika kitaifa katika viwanja vya Chinangali jijini Dodoma.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni