Na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema kuwa ana matumaini makubwa na Mahakama ya Tanzania pamoja na wadau wake katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 hususani katika eneo la uboreshaji wa huduma ya utoaji haki kwa wananchi.
Mhe. Dkt. Samia ametoa rai hiyo leo tarehe 03 Februari, 2025 wakati akihutubia wananchi katika hafla ya Maadhimisho ya Siku ya Sheria nchini iliyofanyika Kitaifa kwenye viwanja vya Chinangali jijini Dodoma ambapo amesema kuwa, Kaulimbiu ya Wiki na Siku ya Sheria ya mwaka huu inaashiria dhamira ya dhati ya Mahakama na Wadau wake katika utekelezaji wa Dira hiyo.
“Nimefurahishwa sana na kaulimbiu hii isemayo; ‘Tanzania ya 2050: Nafasi ya Taasisi Zinzosimamia Haki Madai katika Kufikia Malengo Makuu ya Dira ya Taifa ya Maendeleo’, kaulimbiu hii ni muafaka na inaridhisha na kudhihirisha dhamira ya kuifanya Dira ijayo kuwa ya mipango ya kukuza haki nchini kwenda kufanikiwa,” amesema Rais Samia.
Aidha, Mhe. Dkt. Samia ametoa rai kwa Wadau wengine wa Mihimili ya Serikali na Bunge kujipanga vizuri na mapema kwenye utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2050.
Amesema kuwa, utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo inayoishia mwishoni mwa mwaka huu 2025 umekuwa na matokeo chanya katika maisha ya wananchi ambapo ameeleza kwamba hali ilivyokuwa kwa mwaka 2000 sivyo ilivyo kwa sasa.
Mhe. Dkt. Samia amebainisha kuwa, utekelezaji wa Dira hiyo umekuwa na mabadiliko katika Sekta za kiuchumi, maendeleo ya jamii, Sekta ya Kifedha na katika sekta ya utoaji haki ambapo yameshuhudiwa maendeleo makubwa kwenye miundombinu, vifaa na watumishi.
Akizungumzia maboresho kwa upande wa Sekta ya utoaji haki, Rais Samia amesema kwa sasa, Mahakama ya Tanzania ni miongoni vya Taasisi zenye majengo mazuri yanayopendezesha miji mbalimbali, usikilizwaji wa mashauri kwa njia ya mtandao nao umekuwa jambo la kawaida na umerahisisha na kupungua aza ya wananchi kusafiri umbali mrefu kufuata huduma ya haki.
“Mageuzi na maboresho katika Mahakama zetu hayajatokea kwa sadifa, hatukusadifu tu bali ni mipango madhubuti na hatua za makusudi, kwenye Mpango wa tatu wa Maendeleo ya miaka mitano unaoishia mwaka 2025, msingi mmojawapo wa mpango huo ni kuendelea kuimarisha miundombinu ya mifumo ya kidijitali kuwezesha wananchi kupata manufaa ya mapinduzi ya ili ya kidijitali au TEHAMA kwenye Sekta mbalimbali ikiwemo elimu, Utawala wa Umma na Mahakama,” amesema Mhe. Dkt. Samia.
Ameongeza kuwa, katika juhudi za kuendeleza utawala wa sheria Kifungu namba 120 (h) cha Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) kwa mwaka 2020-2025 kilielekeza Serikali kujenga mifumo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) na kuendelea kuhimiza matumizi yake katika utoaji wa haki.
Ameeleza kwamba, mafanikio ya Mahakama ya Tanzania yaliyoainishwa katika hotuba ya Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma ni matokeo ya utekelezaji wa mipango ya Serikali katika kutekeleza maelekezo ya Ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM).
Kadhalika, Mhe. Dkt. amesema kuwa ni wakati sasa wa kuangalia upande wa haki Madai, ambapo ametoa rai kwa Majaji na Mahakama kuendelea kutoa haki kwa wakati na kutokuwa kikwazo katika suala la utoaji haki kwa wananchi.
Amebainisha kwamba, katika Dira ijayo ya miaka 25, Watanzania wengi wanatamani Tanzania iwe Taifa jumuishi, lenye ustawi, haki na linalojitegemea, ambapo ameeleza kuwa, “katika kufikia matamanio hayo ya wananchi Mhimili wa Mahakam ana Tasnia ya Sheria kwa ujumla utakuwa na mchango mkubwa na tunategemea mtatimiza wajibu wenu ipasavyo.”
Ameongeza kuwa, Dira ijayo itaweka lengo la kuongeza pato la Taifa hadi kufikia Dola bilioni 700 ifikapo 2050, hivyo ili kufikia hapo Serikali italazimia kuchukua hatua za kukuza sekta za kiuchumi, ikiwemo kuvutia uwekezaji na biashara, kuvutia mitaji nchini na kukuza njia za ukusanyaji wa mapato nchini.
“Mambo hayo yote yatalazimu sekta zinazohusika na haki madai kujiandaa vyema katika kutoa huduma za haki, kuongezeka kwa shughuli nyingi za uwekezaji na biashara zitazusha migogoro ya kisheria na uhitaji mkubwa wa huduma za utoaji wa haki, haitarajiwi kwa Mahakam ana Wadau wake kuchelewesha utoaji haki na badala yake tunatarajia Mahakama iwe mwezeshaji wa ukuaji wa uchumi kwa kutenda haki kwa wakati,” amesisitiza Rais Samia.
Kuhusu maslahi ya watumishi wa Mahakama, Mhe. Dkt. Samia ameahidi kuendelea kuboresha kadri bajeti ya Serikali itakavyoruhusu.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akihutubia wananchi katika hafla ya Maadhimisho ya Siku ya Sheria nchini iliyofanyika Kitaifa kwenye viwanja vya Chinangali jijini Dodoma leo tarehe 03 Februari, 2025.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni