Jumatatu, 3 Februari 2025

JAJI MKUU: MABADILIKO YAHITAJIKA KUFIKIA MALENGO YA DIRA YA TAIFA YA MAENDELEO YA MWAKA 2050

 Na MAGRETH KINABO, Mahakama-Dodoma

 

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma amesema ili kuweza kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo ya Mwaka 2050 ni muhimu kwa taasisi zote za utoaji haki na wananchi kwa ujumla kufanya mabadiliko makubwa ya ndani ya taasisi ambayo ni ya kifikra, kimtazamo, kubadili mazoea, kiteknolojia na matumizi ya akili mnemba.

 

Aidha Jaji Mkuu amesema mabadiliko hayo  ni hatua ya kuisaidia Tanzania kuweza kufikia  kiwango cha uchumi wa nchi ya kati ngazi ya juu au juu zaidi. Hivyo  Dira ya Taifa ya Mwaka 2050 ni safari inayohitaji matayarisho ya kina miongoni mwa taasisi zote za umma zinazotarajiwa kufanya mabadiliko makubwa.

 

Jaji Mkuu, Mhe. Prof. Juma amesema hayo leo tarehe 03 Februari, 2025 wakati wa hafla ya kilele cha  Maadhimisho ya Siku ya Sheria nchini  kilichofanyika kwenye Viwanja vya Chinangali jijini Dodoma.

 

Akitoa hotuba yake, Jaji Mkuu  amesema Dira ya Taifa ya Maendeleo ya Mwaka 2050 ni safari inayohitaji matayarisho ya kina miongoni mwa taasisi zote za umma zinazotarajiwa.

 

“Tanzania ya Dira ya Taifa ya Maendeleo ya Mwaka 2050 haiwezi kukabiliana na changamoto ya mabadiliko ya tabianchi na ongezeko la idadi ya watu bila taasisi husika na maeneo hayo kubadilika kutoka mazoea ya sasa. Aidha, Dira ya  Taifa ya  Maendeleo ya Mwaka 2050 haiwezi kufaidi matunda ya matumizi ya Teknolojia za Habari na Mawasiliano hususani akili mnemba bila kufanya mabadiliko makubwa katika taasisi husika na kuziweka kwenye utayari,” amesema Jaji Mkuu Prof.  Juma.

 

Aidha Jaji Mkuu ameongeza kwamba kutokana na uzoefu wake katika kutumia Dira ya Mwaka 2025 kufanya maboresho yake, Mahakama ya Tanzania itaipokea Dira ya Taifa ya Maendeleo ya Mwaka 2050 kama kielelezo cha utashi wa kisiasa kwa taasisi zinazosimamia haki madai na zile zinazosimamia haki jinai kuwa zinatakiwa kufanya mabadiliko makubwa ili zifanikishe Taifa kufikia malengo na matarajio ya Dira hiyo.

Prof. Juma amefafanua kuwa kufikiwa kwa Malengo ya Dira ya  Taifa ya Maendeleo ya Mwaka 2050, kwa kiasi kikubwa, kutategemea mabadiliko makubwa yatakayofanywa ndani ya taasisi zinazosimamia haki madai ili ziwezeshe Tanzania kufikia maono na dhamira ya kuwa nchi ya uchumi wa kipato cha kati ngazi ya juu au juu zaidi. Taasisi zinazosimamia haki madai ndizo zinategemewa kuwa watekelezaji wakubwa wa ramani ya mabadiliko yataifa itakayowekwa na Dira hiyo.

“Katika kukuza utajiri ili kuongeza viwango vya ubora wa maisha na kutokomeza umaskini hakuwezi kufanikiwa endapo taasisi za umma zitashindwa kufanya mabadiliko ya ndani ya taasisi. Ndoto ya jamii ya Watanzania kuwa yenye ustawi, usawa, na kujitosheleza haiwezekani bila ya taasisi za umma kufanya mabadiliko makubwa ya ndani na kuwa na mwelekeo wa kutekeleza Dira ya  Taifa ya Maendeleo ya Mwaka 2050,” amesisitiza.

Amezitaja taasisi zingine ambazo huduma zao zinagusa haki madai za wananchi kila siku na zinahitaji kufanyiwa mabadiliko makubwa ili ziweze kuifikisha Tanzania katika uchumi wa kati ngazi ya juu.

Mifano ya taasisi hizo ni pamoja zile zinazosimamia ardhi, maji, misitu, hifadhi, madini, leseni, na vibali mbalimbali ambazo kila siku zinagusa haki za wananchi.

“Mathalani, taasisi zinazohusika na ardhi zikifanya usimamizi endelevu wa ardhi, migogoro mingi ya ardhi itaishia kwenye usuluhishi bila kufikishwa mahakamani,” amesema huku akitoa mfano kuwa usimamizi endelevu wa ardhi ni mtaji muhimu wa kufikia malengo na matarajio ya Dira ya Taifa ya Maendeleo ya Mwaka 2050.

Halikadhalika ameseme  katika aya ya 4,3.4 ya rasimu ya Dira ya Taifa  ya    Maendeleo ya Mwaka 2050 inahusu  usimamizi wa ardhi eneo ambalo linasimamiwa na taasisi tofauti tofauti na sheria mbalimbali  zinazogusa haki mbalimbali za wananchi.

 

“Taasisi hizi zilizopewa majukumu ya usimamizi endelevu wa ardhi zinatakiwa kujipanga sasa nasi kesho, ili ziwe na utayari wa kukabiliana na kasi ya ongezeko la idadi ya watu, ukuaji wa miji, upanuzi wa shughuli za kilimo, uchimbaji madini, na maendeleo ya viwanda yatakayoongeza uhitaji mkubwa wa rasilimali za ardhi, hivyo kuleta uwezekano wa kuibuka kwa migogoro itakayohitaji utatuzi wa haraka,”amesema.

Amesema taasisi zinazohusika na usimamizi endelevu wa ardhi zisipojipanga, badala ya kuchochea ukuaji wa uchumi endelevu, zitakuwa vyanzo vya migogoro ya ardhi itakayolundikana katika ngazi mbalimbali za mahakama.

Akizungumzia kuhusu kauli mbiu ya Wiki na Siku ya Sheria Tanzania kwa mwaka huu, 2025 isemayo ‘Tanzania ya 2050: Nafasi ya Taasisi zinazosimamia haki madai katika kufikia Malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo’. Inaakisi dirá hiyo na kuhimiza taasisi za hakimadai nchini kushiriki kikmilifu kuwezesha kufikiwa kwa malengo yake.

Amesema Maadhimisho ya Siku ya ya Sheria hutanguliwa na Wiki ya Sheria, ambayo hutumika kutoa elimu kwa umma ikiwemo kuwasikiliza wananchi ambao hutoa mrejesho na maoni kuhusu utoaji haki nchini.  Hivyo kwa mwaka huu, wiki hiyo ya utoaji elimu ilizinduliwa na Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne, Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, tarehe 25 Januari, 2025 kwenye Viwanja vya Mwalimu Nyerere, jijini Dodoma.

Kuhusu wiki hiyo ya Jaji Mkuu  amesema wananchi waliopata elimu wametoa maoni mbalimbali ambayo kwa Mahakama ni mtaji wa kusaidia kujipima na kuweka mikakati thabiti ya kuboresha huduma za utoaji haki nchini.

Huku akiwataka wananchi kutosubiri wiki hiyo,  ili waipate elimu ya sheria , bali watumie nafasi ya mara mbili kwa wiki inayotolewa na mahakama mbalimbali  nchini kabla ya kuanza kwa shughuli za  kimahakama.

Hata hivyo amesema Mahakama inaendelea kuboresha huduma za utoaji haki ikiamini kuwa huduma bora huchangia utulivu, amani, na umoja unaowezesha kufikiwa kwa mipango mbalimbali ya maendeleo kwa mtu mmojammoja, familia, na taifa kwa ujumla.

Maadhimisho ya Siku ya Sheria Tanzania, mbali na kuashiria kuanza kwa mwaka mpya wa kazi wa Mahakama, yamekuwa yakitumika kufikisha maombi kwa Mwenyezi Mungu na kuwaombea watoaji haki na kuwakumbusha kuwa kazi ya utoaji haki ni ya Mwenyezi Mungu, hivyo Majaji na Mahakimu  ni mawakala wa kutimiza wajibu huo.

Kuhusu maslahi ya watumishi wa Mahakama, Jaji Mkuu amemshukuru Rais Samia,    kwa kuboresha maboresho ya baadhi ya posho.

Wakati huohuo, Jaji Mkuu akizungumza kuhusu hali ya mashauri  amesema kipindi cha  mwaka 2024, jumla ya mashauri 242,284 yalifunguliwa kwenye  ngazi zote za mahakamaikilinganishwa na mashauri 249,846 yaliyofunguliwa mwaka 2023. Hivyo inaonesha punguzo la asilimia tatu.

Katika kipindi cha mwaka 2024, mashauri 245,310 yalisikilizwa na kumalizika, ambayo ni sawa na asilimia 101 ya mashauri yaliyofunguliwa kwa mwaka 2024 na asilimia 84 ya mashauri yote yaliyokuwa mahakamani mwaka huo (yaliyofunguliwa mwaka 2024 na yaliyobaki 2023).

Pia amesema viwango vya umalizaji na uondoshaji wa mashauri navyo vimeongezeka kwa asilimia moja  ikilinganishwa na mwaka 2023.Hivyo takwimu hizo zinaashiria ongezeko la ufanisi wa usikilizaji wa mashauri.

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma, akitoa hotuba yakeya  Maadhimisho ya  Kilele cha Siku ya Sheria  yaliyofanyika  leo tarehe 3 Februari, 2025 kwenye Viwanja vya Chinangali, jijini Dodoma.  

Baadhi ya Majaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania Mahakama Kuu ya Tanzania wakiwa katika  picha ya pamoja wakati wa Maadhimisho ya  Kilele cha Siku ya Sheria  yaliyofanyika  leo tarehe 3 Februari, 2025 kwenye Viwanja vya Chinangali, jijini Dodoma. 

Baadhi ya viongozi wa dini, Majaji wastaafu, Makamishna wa Tume ya Utumishi wa Mahakama wakiwa katika siku hiyo.

Meza kuu ikiwa katika picha ya pamoja  na wawakilishi kutoka Ubalozi wa Ireland.

Wageni na wanataaluma ya sheria waliohudhuria maadhimisho hayo.

Kwaya ya Mahakama ya Tanzania ikitumbuiza.

Brass Band  ikitumbuiza.

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma,(aliyeinama) akikagua gwaride maalumu.

Gwaride.

(Picha na  INNOCENT KANSHA - Mahakama, Dodoma)

 

 

 

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni