- Jaji Kiongozi, Mtendaji Mkuu wa Mahakama wawasihi kupanga mikakati mizuri yenye kuleta maboresho
- Ushirikiano na Mihimili mingine sambamba na ushirikishwaji wa watumishi nao wasisitizwa katika safari ya maboresho
Na ARAPHA RUSHEKE, Mahakama-Dodoma
Jumla ya watumishi 33 wa Mahkama Kuu ya Zanzibar wakiongozwa na baadhi ya Majaji wa Mahkama hiyo leo tarehe 17 Februari, 2025 wametembelea Makao Makuu ya Mahakama jijini Dodoma ili kujifunza na kubadilishana uzoefu wa utendaji kazi na maboresho ya huduma ya utoaji haki.
Baada ya kuwasili katika jengo hilo, watumishi hao walipata fursa ya kuonana na kufanya mazungumzo na Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Mustapher Mohamed Siyani.
Akizungumza na watumishi hao ofisini kwake Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma, Mhe. Dkt. Siyani amewashukuru watumishi hao kwa kuitembelea Mahakama ya Tanzania na kuwaeleza kuwa Mahakama nchini ilianza kufanyaa maboresho kwa miaka kadhaa.
"Sisi tumekuwa na miaka kadhaa ya kufanya maboresho kwa kushirikiana na Benki ya Dunia na tulianza mwaka 2015 tunaweza kusema tuna miaka kumi sasa ya kufanya maboresho, yapo maeneo ambayo tumeshuhudia yakiimarika moja wapo ni eneo la ujenzi wa miundombinu ya majengo na kama mnavyofahamu hali ya miundombinu yetu haikuwa mizuri sana hatujamaliza na itachukua muda kumaliza kwa sababu ya ukubwa wa Nchi yetu,” amesema Jaji Kiongozi.
Amesema kuwa, eneo jingine ambalo limepata mafanikio ni katika muda ambao mashauri yanaisha Mahakamani, ambapo amesema kuwa, Mahakama kazi yake kubwa ni kusikiliza mashauri kwa wakati, chochote kinachofanyika kinasababisha maendeleo mazuri kwenye eneo hilo, hivyo ili kuona matokeo kwenye eneo hilo inatakiwa kupunguza muda ambao watu wanatumia kupata haki.
“Ili Mahakama ipate imani ya wananchi hakuna namna yeyote ile sio uzuri wa majengo, sio kitu chochote kile, sio suti zetu ni muda ambao watu watatumia watakapokuja mahakamani, watu wangependa mgogoro unapotokea wasikilizwe maamuzi yatoke kwa wakati, mimi naamini yapo maeneo ambayo hata sisi tunapaswa kujifunza kutoka kwenu na ninaamini tutajifunza pia karibuni sana,” ameeleza Mhe. Dkt. Siyani.
Aidha, baada ya kuonana na kuzungumza na Jaji Kiongozi, wageni hao walipelekwa katika ukumbi wa mikutano uliopo katika jengo hilo na kupata pia fursa ya kuonana na Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel ambaye alifungua kikao cha kubadilisha uzoefu kati ya Mahkama ya Zanzibar na Mahakama ya Tanzania.
Akizungumza na ugeni huo, Prof. Ole Gabriel amesema kuwa, jambo kubwa ambalo limeisaidia Mahakama ya Tanzania katika safari ya maboresho pamoja na mambo mengine ni kuwa na Mpango Mkakati ambao umeipa Mahakama mwongozo mzuri wa nini cha kufanya na namna gani ya kufanya.
“Mpango Mkakati umetupa dira namna gani tufanye nini na kujitathmini pia, Mpango Mkakati wa mwaka (2020/21-2024/25) ambao unaelekea ukingoni na ni jambo kubwa na limetusaidia sana, tunatambua kwamba ni jukumu kubwa la Mahakama ya utoaji haki, mipango yote ambayo tunaifanya inatuwezesha kufikia lengo la utoaji haki,” amesema Mtendaji Mkuu.
Kadhalika ametoa rai kwa ujumbe huo kuwa, suala lingine la kuzingatia katika safari ya maboresho ni pamoja na kujumuisha au kushirikisha mawazo ya watumishi wote kwa kuwa kila mmoja na mchango katika kufanikisha safari hiyo.
“Hakikisheni katika kuimarisha ushirikiano ‘team spirit’ muwe kitu kimoja hii itawafikisha mbali, isitokee mkaanza kutofautiana,” amesema Prof. Ole Gabriel.
Ameongeza kwa kuwataka kuwa na ushirikiano wa karibu na Mihimili mingine ya Dola ikiwemo Serikali na Bunge, ambapo amesema kuwa ni muhimu katika utoaji wa huduma ya haki kwa wananchi.
Wakiwa katika jengo hilo jipya la Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania, watumishi hao wa Mahakama Kuu Zanzibar hao wamepata wasaa wa kupatiwa mawasilisho mbalimbali na kujionea shughuli mbalimbali zinazoendelea katika jengo hilo.
Wameoneshwa kufurahishwa na maboresho hayo ya miundombinu ya Mahakama na kuipongeza Serikali na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na Uongozi wa Mahakama ya Tanzania kwa kufanikisha maboresho hayo.
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe.Dkt.Mustapher Mohamed Siyani akisisitiza jambo wakati alipokuwa akizungumza na ujumbe kutoka Mahkama Kuu ya Zanzibar (hawapo katika picha) walipomtembelea ofisini kwake Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania Dodoma leo tarehe 17 Februari, 2025.
Jaji Kiongozi wa Mahakama ya Tanzania Mhe.Dkt.Mustapher Siyani (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na sehemu ya Majaji wa Mahkama Kuu ya Zanzibar pamoja na watumishi wa Mahkama Kuu Zanzibar leo tarehe 17 Februari, 2025 walipomtembelea ofisini kwake Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni