Jumanne, 18 Februari 2025

MAFUNZO HAYA YAWAFIKIE WADAU WOTE WA HAKI JINAI; JAJI TIGANGA

Na Mwandishi Wetu - Mahakama, Momba

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Mbeya, Mhe. Joachim Charles Tiganga, tarehe 14 Februari 2025 amefungua mafunzo maalum ya wadau wa haki jinai katika Wilaya ya Momba yaliyolenga kuboresha utoaji wa haki kwa kuepusha kutonesha majeraha ya kisaikolojia kwa wahanga wa ukatili wa kingono pamoja na matumizi ya adhabu mbadala katika mfumo wa haki jinai ili kupunguza mlundikano wa wafungwa katika magereza.

Mhe. Tiganga amesisitiza umuhimu wa mafunzo hayo kwa wadau wa sekta ya sheria na kuelekeza kuwa ni muhimu yakawafikia wadau wote wa mkoa wa Songwe ili kuongeza ufanisi katika utoaji haki.

Aidha, aliwapongeza wadau wa Mahakama Momba kwa kushiriki kwa pamoja katika mafunzo hayo na kwa kujadiliana kuhusu changamoto na mbinu bora za kuboresha utendaji kazi katika eneo hilo muhimu. Alisisitiza kuwa ujuzi walioupata hauna budi kusambazwa kwa wengine ambao hawakupata fursa ya kushiriki, ili kuhakikisha maarifa haya yanawanufaisha wadau wote wa haki.

Pia, Mhe. Tiganga aliwahimiza washiriki kuyatumia ipasavyo mafunzo hayo katika kutekeleza majukumu yao kwa weledi katika kutenda haki.

Mafunzo hayo yamefanyika katika ukumbi wa Mahakama ya Wilaya Momba na kuhudhuriwa na mahakimu wa ngazi mbalimbali pamoja na wadau wa haki jinai ndani ya wilaya hiyo, Mkuu wa Mashtaka wa Wilaya, waendesha mashitaka, Kaimu Mganga Mkuu wa Mji, Afisa Ustawi wa Jamii na wasaidizi wa kumbukumbu wa Mahakama.

Mafunzo hayo yaliyopewa jina la Enhancing Justice Delivery: Integrating Trauma-Informed Approaches and Community-Based Rehabilitation’’ yalifanyika kwa lengo la kuwajengea uwezo washiriki katika kushughulikia wahanga wa ukatili wa kingono na kuhakikisha kuwa mfumo wa haki jinai unatoa suluhisho mbadala kwa wahalifu wa makosa madogo kupitia huduma kwa jamii badala ya vifungo vya kawaida.

Aidha, Mafunzo hayo ni mwendelezo wa mafunzo ya kuzuia kutonesha majeraha kwa wahanga wa ukatili wa kingono yaliyoendeshwa na Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto kwa ushirikiano na Taasisi ya Irish Rule of Law International (IRLI) jijini Dodoma kuanzia tarehe 4 hadi 6 Februari, 2025.  

Katika mafunzo hayo, mada mbalimbali ziliwasilishwa na kujadiliwa kwa kina, ikiwa ni pamoja na Mikakati ya Kuzuia Kutonesha Majeraha ya Kisaikolojia kwa Wahanga wa Ukatili wa Kingono iliyowezeshwa na Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Wilaya Momba Mhe. Raymond V. Kaswaga, ambapo washiriki walijifunza namna ya kutambua na kuwalinda mashahidi na wahanga wa ukatili wa kijinsia na kingono.

Aidha, ilielezwa umuhimu wa mbinu za kuzingatiwa na wadau wa haki jinai katika kuhakikisha mashahidi na wahanga wa ukatili hawapati madhara zaidi wanapotoa ushahidi mahakamani.

Naye, Afisa Huduma za Uangalizi kwa Jamii Bw. Nelson Duba, aliwaongoza washiriki kubadilishana uzoefu wa namna ya kutoa adhabu ya huduma kwa jamii kwa makosa yanayostahili adhabu mbadala ambayo ni ya kifungo cha chini ya miaka mitatu. Washiriki walijifunza jinsi huduma kwa jamii inavyosaidia katika urekebishaji wa wahalifu na kupunguza gharama kwa Serikali za uendeshaji wa magereza.

Washiriki hao, walipata nafasi ya kujifunza tofauti kati ya wafungwa wa huduma kwa jamii na wale wa uangalizi maalum (probation) ambapo pamoja na mambo mengine ilielezwa kuwa wafungwa hufuatiliwa na maafisa maalum wa uangalizi badala ya kutumikia vifungo gerezani.

Kwa upande wake, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Songwe, Mhe. Francis Kishenyi, alisisitiza kuwa mafunzo hayo yana umuhimu mkubwa katika kuleta mabadiliko chanya katika utoaji wa haki kwa njia mbadala na kwa kuzingatia athari za kihisia  na kisaikolojia kwa wahanga wa matukio ya ukatili wa kingono na kueleza kuwa Mafunzo hayo yataacha msingi imara wa maboresho katika sekta ya haki wilayani humo.

Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Wilaya Momba Mhe. Raymond V. Kaswaga (Katika) akiwa kwenye picha ya pamoja na washiriki wa mafunzo hayo yaliyofanyika Mahakama ya Wilaya Momba.



Washiriki wa mafunzo hayo yaliyofanyika Mahakama ya Wilaya Momba wakifuatilia mafunzo hayo.

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni