Jumanne, 18 Februari 2025

MFUMO WA eJOPRAS UNAWAKUMBUSHA MAHAKIMU KUWAJIBIKA

Na DANIEL SICHULA – Mahakama, Mbeya

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Mbeya Mhe. Joachim Tiganga tarehe 12 Februari, 2025 ahitimisha mafunzo ya mfumo wa upimaji na kutathmini utendaji kazi kwa Mahakimu wa Mahakama Mkoa wa Mbeya.

Katika maboresho ya utendaji kazi kwa watumishi wa Mahakama, Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya iliendesha mafunzo maalum kwa Mahakimu wa Mkoa wa Mbeya katika matumizi mbalimbali ya Mifumo ya kielektroniki ikiwa ni jitihada za kuongeza ufanisi wa utendaji kazi kwa watumishi hao.

Wataalam wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHEMA) wa Mahakama Kuu Mbeya na Songwe, Bw. Sadati Kalungwana na Bi. Rosemary Mwandambo, walitoa elimu ya mifumo ya kielektroniki namna ya utumiaji wa mifumo kama eJOPRAS, eCMS na Data Hub kwa Mahakimu na umuhimu wa mifumo hiyo katika utendaji wao wa kazi za kila siku.

Aidha, washiriki walipata kujua namna ya kutumia mfumo wa eJOPRAS katika majukumu yao ya kila siku na namna ya kujaza taarifa zao kwani mfumo huo ni muhimu katika kutathmini utendaji wao wa kazi na kupata mrejesho wa kile wanafanyia kazi kila siku.

Umuhimu wa mfumo eJOPRAS ulionekana pale Mahakimu walipojaribu kufanya kwa vitendo na kuona ni namna gani mfumo huo utakua na msaada katika kazi zao za kila siku.

Mafunzo hayo yaliwapa Mahakimu uelewa wa kina wa namna ya kutumia mfumo huo kwa ufanisi, ikiwa ni pamoja na mbinu za kuhakikisha tathmini zao zinasaidia kuimarisha huduma kwa Wananchi.

Na katika Mfumo wa eCMS washiriki waliweza patiwa ujuzi zaidi kwani wamekuwa wakiutumia mara kwa mara katika usajili wa mashauri, usikilizwaji wa mashauri na kutolea maamuzi kwa wakati na kupunguza ucheleweshaji wa mashauri.

Na pia, Mahakimu hao walishukuru uongozi wa Mahakama Kuu Mbeya kwa kuendesha mafunzo ya mifumo ya kielectroniki, kwani imewakumbusha uwajibikaji katika majukumu yao ya kila siku katika kuwahudumia wananchi kwa haki na kwa ufanisi.

Afisa TEHAMA Bw. Sadati Kalungwanasadati akifafanua namna mfumo wa ejopras unavyofanyakazi.

Afisa TEHAMA Bi.  Rosemary Mwandambo akifafanua namna mfumo wa ejopras unavyofanyakazi.

Mahakimu wakiwa kwenye mafunzo ya mifumo ya kieletroniki.



Hakuna maoni:

Chapisha Maoni