Ijumaa, 28 Machi 2025

JAJI KIONGOZI AENDELEA NA ZIARA YAKE MAHAKAMA YA WILAYA YA SIKONGE

Na AMANI MTINANGI, Mahakama

Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Mustapher Mohamed Siyani anaendelea na ziara yake ya kikazi Kanda ya Tabora ambapo ametembelea Mahakama ya Wilaya ya Sikonge kukagua hali ya utendaji kazi wa Mahakama hiyo na kujadili changamoto pamoja na mafanikio katika utendaji kazi na wadau katika eneo hilo.

Wakati wa ziara yake jana tarehe 27 Machi, 2025, Mhe. Dkt. Siyani alieleza kwamba Mahakama inaendelea kufanya juhudi kubwa katika kuboresha huduma za Mahakama kwa wananchi ili kuongeza imani ya wananchi kwa Mhimili huo. Alisisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya Mahakama na mamlaka zingine za kiserikali bila kuathiri uhuru wake katika kutoa uamuzi wa mashauri.

Akiwa katika Ofisi ya Mahakama ya Wilaya Sikonge alipokea changamoto ya Wilaya hiyo za kutokuwa na Gereza na Kituo cha Polisi kutokuwa na mazingira rafiki kwa shughuli za Jeshi la Polisi, ambapo katika hilo Jaji Kiongozi alisema analichukua na ataliwasilisha katika mamlaka husika kwa ajili ya hatua zaidi. 

"Mahakama inaendelea kufanya juhudi kubwa katika kuboresha huduma zake kwa wananchi ili kuongeza imani ya wananchi kwa Mahakama. Ushirikiano kati ya Mahakama na mamlaka zingine za kiserikali ni muhimu, lakini ni lazima lifanyike bila kuathiri uhuru wa Mahakama katika kufanya maamuzi ya mashauri yanayofikishwa Mahakamani. Nilipokea changamoto ya Wilaya kutokuwa na Gereza na kituo cha Polisi kutokuwa na mazingira rafiki kwa shughuli za Kipokisi, hii ni changamoto ambayo nitaichukua na kuiwasilisha kwa mamlaka husika ili hatua zaidi zichukuliwe," alisema Mhe. Dkt. Siyani

Aidha, Jaji Kiongozi alitoa taarifa kuhusu mchakato wa kuanzisha Mahakama inayotembea, akieleza kwamba uko katika hatua za mwisho na kwamba hatua hiyo itawapa wananchi wa maeneo ya vijijini na yasiyo na huduma za Mahakama za kawaida fursa ya kupata huduma za kisheria kwa ukaribu zaidi.

Katika kikao huo, Mhe. Dkt. Siyani alisisitiza kuhusu umuhimu wa watumishi wa Mahakama kujitathmini mara kwa mara ili kuboresha utendaji wao huku akitoa wito kwa watumishi kuwa na moyo wa kujitolea na kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi ili kufikia malengo ya Mahakama, na kuwahakikishia wananchi kuwa huduma bora zitatolewa.

Baada ya ziara yake wilayani hapo, Mhe. Dkt. Siyani alifanya Mkutano na Waandishi wa Habari ambapo alifafanua mafanikio yaliyopatikana katika Mahakama ya Tanzania na kuweka wazi kuwa wastani wa muda wa usikilizaji wa mashauri umepungua kwa kiasi kubwa ikilinganishwa na miaka kadhaa iliyopita jambo linaloashiria hayo ni mafanikio ya kujivunia.

“Mafanikio haya ni matokeo ya juhudi za pamoja za Mahakama na wadau wake katika kuhakikisha kwamba haki inapatikana kwa haraka na kwa ufanisi," ameeleza Jaji Kiongozi.

Katika hatua nyingine, alieleza kuwa Miradi ya ujenzi wa Mahakama ya Wilaya Uyui na Mwanzo Kipili imeanza kutekelezwa hivyo ana imani italeta mageuzi chanya katika upatikanaji wa huduma za Mahakama katika maeneo hayo.

Kadhalika, Mhe. Dkt. Siyani amesema kwamba, kiwango cha kuridhika kwa wananchi na huduma za Mahakama kimeongezeka huku akisisitiza kuwa, dhamira ya Mahakama ni kuendelea kufanya kazi kwa bidii ili kuhakikisha haki inapatikana kwa wote na kwa wakati.

Mkuu wa Wilaya ya Sikonge, Mhe. Cornel Magembe  (aliyesimama) akitoa salamu za Wilaya kwa Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Mustapher Mohamed Siyani (aliyeketi kulia) alipotembelea Wilaya hiyo jana tarehe 27 Machi, 2025 kwa lengo la kufanya ukaguzi wa Mahakama. Wengine ni viongozi mbalimbali wa Mahakama na Serikali.

Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Mustapher Mohamed Siyani (kushoto) akisalimiana na watumishi wa Mahakama ya Wilaya Sikonge wakati wa ziara yake jana tarehe 27 Machi, 2025.

Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe.Dkt. Mustapher Mohamed Siyani (katikati) na meza kuu (walioketi) wakiwa katika picha ya pamoja na watumishi wa Mahakama Kuu Kanda ya Tabora.

Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Tabora, Mhe. Pamela Mazengo (aliyesimama) akisoma taarifa ya utendaji kazi wa Mahakama Kuu Kanda ya Tabora mbele ya Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Mustapher Mohamed Siyani (hayupo katika picha) wakati wa ziara yake katika Kanda hiyo.

(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma)



Hakuna maoni:

Chapisha Maoni