Ijumaa, 28 Machi 2025

MAGEREZA WAZIPA TANO MAHAKAMA KANDA YA SHINYANGA NA GEITA KASI YA USIKILIZAJI MASHAURI

TEHAMA yatajwa kuchochea kasi hiyo

Na EMMANUEL OGUDA, Mahakama-Shinyanga

Kasi ya usikilizaji wa mashauri Kanda za Shinyangana Geita, yatajwa kuwa chanzo kikuu cha kupungua kwa mlundikano wa wafungwa na Mahabusu katika Gereza kuu la Wilaya ya Kahama.

Akitoa taarifa ya wafungwa na mahabusu wakati wa ukaguzi wa kawaida uliofanywa katika Gereza hilo na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Shinyanga, Mhe. Frank Mahimbali na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Geita, Mhe. Kevin Mhina leo tarehe 28 Machi, 2025, Mkuu wa Magereza Wilaya ya Kahama Mrakibu Mwandamizi wa Magereza, SSP Hamza Abdallah amesema, awali idadi ya mahabusu na wafungwa ilikuwa kati ya 200 hadi 300.

SSP Abdallah amesema, kutokana na kasi ya usikilizwaji wa mashauri iliyochangiwa kwa kiasi kikubwa na matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), idadi ya wafungwa na mahabusu imepungua hadi 181 ikiwa ni ziada ya wafungwa wanne (4) tu tofauti na idadi halisi inayohitajika ya washikiliwa 177.

"Natumia nafasi hii kuzipongeza Mahakama Kuu Kanda za Shinyanga na Geita kwa kuwa Gereza letu la Kahama, linashikilia Mahabusu kutoka katika Kanda hizi mbili, ikilinganishwa na mwaka jana mwezi Desemba, malalamiko ya wafungwa na mahabusu yalikuwa mengi, lakini leo mlipofika mkiwa Majaji Wafawidhi wawili, hatuna msongamano wa wafungwa na mahabusu isipokuwa tuna ziada ya washikiliwa wanne (4) tu,’’ amesema Mkuu huyo wa Magereza  Wilaya ya Kahama.

SSP Abdallah ameipongeza Mahakama Kuu Kanda ya Shinyanga kwa utaratibu wa kufanya ukaguzi katika Gereza hilo kwa pamoja na Kanda ya Geita ili kutatua changamoto zinazowakabili wafungwa na mahabusu katika Gereza hilo huku akiongeza kuwa utaratibu unaofanywa na Mahakama wa kutembelea Magereza kila robo, unaendelea kutatua changamoto nyingi zitokanazo na usikilizwaji wa mashauri ya wafungwa na mahabusu katika gereza hilo.

Wakisoma taarifa kwa Majaji Wafawidhi hao, Mahabusu na wafungwa katika Gereza la Wilaya ya Shinyanga, wameiomba Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka kuharakisha upelelezi katika mashauri yanayowakabili ili kuendana na kasi ya Mahakama ya usikilizwaji wa mashauri kwa haraka.

Aidha, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Shinyanga, Mhe Frank Mahimbali amesema, "Desemba, 2024 nilifika hapa kufanya ukaguzi na kukuta malalamiko mengi ya Wilaya za Mbogwe na Bukombe, nilifanya mawasiliano na Jaji Mfawidhi Kanda ya Geita, changamoto nyingi zimetatuliwa, na leo tumeambatana na Jaji Mfawidhi kutoka Kanda ya Geita akiwa ameambatana na Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Geita, Mhe. Griffin Mwakapeje, Naibu Msajili, Mtendaji wa Mahakama pamoja na Mahakimu wa Wilaya za Bukombe na Mbogwe ili kuona kama kuna changamoto zingine ziweze kutatuliwa leo.’’

Kwa upande wake, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Geita, Mhe. Kevin Mhina amesema, matumizi ya TEHAMA katika Kanda ya Geita yamerahisiha kwa kiasi kikubwa upatikanaji wa haki kwa wakati, na kwamba hakuna tena malalamiko ya nakala za hukumu ambazo kwa sasa hutolewa kila shauri linapomalizika Mahakamani.

Ukaguzi katika Gereza la Wilaya ya Kahama umefanyika kwa pamoja ukihusisha Kanda za Shinyanga na Geita, ukiwa na lengo la kusikiliza na kutatua changamoto zinazowakabili wafungwa na mahabusu katika gereza hilo, ukaguzi huo umehusisha Majaji kutoka Kanda za Shinyanga na Geita, Naibu Wasajili, Watendaji wa Mahakama, Mahakimu wa Wilaya za Kahama, Bukombe na Mbogwe.


Mkuu wa Magereza Wilaya ya Kahama, Mrakibu Mwandamizi wa Magereza, SSP Hamza Abdallah (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Majaji Wafawidhi wa Kanda za Shinyanga na Geita wakati walipofanya ukaguzi katika gereza la Kahama leo tarehe 28 Machi, 2025. Kushoto ni Mhe. Frank Mahimbali na kulia ni Mhe. Kevin Mhina.


Mkuu wa Magereza Wilaya ya Kahama, Mrakibu Mwandamizi wa Magereza, SSP Hamza Abdallah (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Majaji Wafawidhi wa Mahakama Kuu Shinyanga na Geita, Mhe. Frank Mahimbali (wa tatu kushoto) na Mhe. Kevin Mhina (wa tatu kulia).  Wa pili kulia ni Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Geita, Mhe. Griffin Mwakapeje, wa kwanza kushoto ni Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Shinyanga, Mhe. Gadiel Mariki, wa pili kushoto ni Naibu Msajili Mahakama Kuu ya Shinyanga, Mhe. Asha Mwetindwa  na wa kwanza kulia ni  Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Geita,  Mhe. Fredrick Lukuna.

(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma)


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni