Ijumaa, 28 Machi 2025

JOPO LA MAJAJI WA RUFANI SUMBAWANGA LAFANIKIWA KUSIKILIZA MASHAURI ASILIMIA 100

Na Fredrick Mahava- Mahakama, Sumbawanga

Jaji wa Mahakama ya Rufani ya Tanzania Mhe. Augustine Mwarija ameongoza kikao cha tathmini ya jopo la Mahakama ya Rufani kilichoketi Mahakama Kuu, Kanda ya Sumbawanga. Aidha kwa mujibu wa Kalenda ya Mahakama ya Rufani kikao hicho ni cha kwanza kwa mwaka 2025 kilichoanza tarehe 10 Machi, 2025 na kinatarajiwa kuhitimishwa leo tarehe 28 Machi, 2025.

Katika kikao hicho jumla ya mashauri 28 yalipangwa kusikilizwa na mashauri yote yamefanikiwa kusikilizwa ikipelekea ufanisi wa asilimia 100 ya mashauri yote yaliyopangwa.

Aidha, katika mashauri hayo 28, Mashauri 17 yameshatolewa maamuzi, Mashauri 11 bado yanasubiria  kutolewa maamuzi na hakuna shauri lililohairishwa.

Vilevile, Mhe. Mwarija ambaye alikuwa Mwenyekiti wa jopo la Majaji wa Mahakama ya Rufani waliosikiliza mashauri hayo kwa kushirikiana na Majaji wengine wa Mahakama hiyo ambao ni Mhe. Lilian Mashaka na Mhe. Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi kwa pamoja walisikiliza mashauri ya Jinai 24 na Mashauri ya Madai 2 na maombi ya madai 2.

Pia tumefanikiwa kusajili mashauri yote yalipangwa katika mfumo (eCMS) na mashauri yaliyomalizika tumeweza kuingiza taarifa hizo kwenye mfumo.

Akieleza sababu moja wapo ya mafanikio hayo, Mhe. Mwarija ni ushirikiano walioupata kutoka kwa wadau wote wa mahakama kama vile Jeshi la Magereza mkoa wa Rukwa  kwa kuwawaisha wafungwa mapema Mahakamani na Mawakili kwa ujumla kufika mapema kumewarahisishia wao kufanya kazi kwa urahisi na kumaliza mashauri mapema

Wakati huohuo, Jopo la Majaji wa Mahakama ya Rufani ya Tanzania walioketi Mahakama Kuu, Kanda ya Sumbawanga walieleza changamoto moja kubwa ya mawakili kushindwa kusajili orodha ya mashauri kuegemewa (list of Authority) kwa wakati na hivyo kuomba kutumia mashauri hayo wakati wa usikilizwaji wa mashauri husika mahakamani.

Naye, Naibu Msajili wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Judith.J.Kamala  aliwashukuru, Jeshi la Mageleza, Polisi, Mawakili wa Serikali, Mawakili wa kujitegemea, Ofisi ya Mwendesha Mashtaka wa Serikali kwa ushirikiano waliouonesha na pia alilishukuru Jopo hilo la Majaji wa Mahakama ya Rufani kwa kuendesha mashauri ya Rufaa hayo kwa haki na kuwasaidia maafisa walioshiriki katika kikao hicho kujifunza mambo mengi katika utekelezaji wa sheria na utoaji haki kwa wananchi kwa wakati.

Vilevile, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Sumbawanga Mhe. Fredrick Manyanda, Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Sumbawanga Mhe. Abubakar Mrisha, Naibu Msajili wa Mahakama Kuu, Kanda ya Sumbawanga Mhe. Joseph Luambano, Mtendaji wa Mahakama Kuu, Kanda ya Sumbawanga Bw. Machumu Essaba na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Rukwa Mhe. Kisasila Saguda waliungana na wadau wengine wa haki jinai kushiriki kikao hicho cha tathmini ya kikao cha Mahakama ya Rufani (Session) kilichofanyika katika Kanda ya Sumbawanga.

Jaji wa Mahakama ya Rufani ya Tanzania Mhe. Augustine Mwarija akiongoza kikao cha tathmini ya Kikao (Session) cha Mahakama ya Rufani kilichofanyika Kanda ya Sumbawanga.

Naibu Msajili wa Mahakama ya Rufani Mhe. Judith J.Kamala akizungumza wakati wa kikao cha tathmini ya kikao (Session) cha Mahakama ya Rufani kilichofanyika Kanda ya Sumbawanga.

Majaji wa Mahakama ya Rufani Mhe. Lilian. L. Mashaka na Mhe. Dkt. Eliezer.M.Fereshi wakifuatilia kwa ukaribu yanajiri kwenye kikao cha tathmini ya Kikao (Session) cha Mahakama ya Rufani kilichofanyika Kanda ya Sumbawanga.

Wadau mbalimbali wa Haki Jinai wakisikiliza kwa makini wakati wa kikao cha tathmini ya Kikao (Session) cha Mahakama ya Rufani kilichofanyika Kanda ya Sumbawanga.

(Habari Hii Imehaririwa na Innocent Kansha - Mahakama)






Hakuna maoni:

Chapisha Maoni