Jumatano, 19 Machi 2025

JAJI MFAWIDHI MBEYA AFUNGUA MAFUNZO YA UTEKELEZAJI WA HUKUMU MAHAKAMA ZA MWANZO

Na Mwandishi Wetu- Mahakama, Momba

Kamati ya Mafunzo ya kimahakama, Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Mbeya hivi karibuni iliratibu na kuendesha mafunzo maalum ya utekelezaji wa hukumu kwa Mahakimu wa Mahakama za Mwanzo wa Kanda hiyo ambayo inajumuisha Mikoa ya Mbeya na Songwe.

Mafunzo hayo yaliyoendeshwa mnamo tarehe 13 Machi, 2025 yalilenga kuboresha Utekelezaji wa Hukumu katika Mahakama za Mwanzo na yalifanyika kwa njia ya mtandao kupitia jukwaa la Mahakama Mtandao (Virtual Court Platform).

Akifungua Mafunzo hayo, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Mbeya Mhe. Joachim Tiganga aliwasisitiza washiriki wa mafunzo hayo umuhimu wa uelewa wa kina wa taratibu za utekelezaji wa hukumu ili kuhakikisha haki inatendeka kwa ufanisi na weledi na kwa kuzingatia sheria.

Mhe. Tiganga alisema kuwa, utekelezaji wa hukumu ni hatua muhimu katika kuhakikisha haki inapatikana kwa walioshinda mashauri yao, na kwamba kucheleweshwa kwa utekelezaji huo kunaweza kupunguza imani ya wananchi kwa Mahakama lakini pia kufanya ushindi katika kesi kuwa ni kama pambo tu.

Mhe. Tiganga aliwataka washiriki wa mafunzo haya kutumia fursa hiyo kujifunza na kubadilishana uzoefu ili kuboresha utendaji wao wa kazi kila siku.

“Nipongeza mwamko wenu wa ushiriki mkubwa wa Mahakimu wa Mahakama za Mwanzo katika mafunzo haya na kuwataka kuhakikisha kuwa wanatumia maarifa watakayoyapata kuboresha utoaji wa huduma za Mahakama,” alisistiza Jaji Tiganga.

Kwa upande wake, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Songwe, Mhe. Francis Kishenyi akihitimisha mafunzo hayo aliwapongeza washiriki kwa ushiriki mzuri na kujituma katika kujifunza mbinu bora za utekelezaji wa hukumu.

“Utekelezaji wa hukumu ni hatua muhimu inayohakikisha kuwa haki inayotolewa na Mahakama inatekelezwa kwa ufanisi na kwamba kutofuata taratibu sahihi kunaweza kuathiri uaminifu wa Mhimili wa Mahakama kwa wananchi,” alisisitiza Mhe. Kishenyi.

Vilevile, aliwaasa washiriki kuzingatia sheria na taratibu zote za utekelezaji wa hukumu ili kuepuka ucheleweshaji au changamoto zinazoweza kusababisha malalamiko kutoka kwa wadaawa. Aidha, aliwahimiza Wafawidhi wa Vituo vya Mahakama kuhakikisha kuwa utekelezaji wa hukumu unafanyika kwa uadilifu na kuzingatia maadili ya kimahakama.

Aidha, alikumbusha Mahakimu hao kuwa, ukaguzi wa mara kwa mara katika Mahakama unapaswa pia kuelekeza macho katika eneo hilo la utekezaji wa hukumu ili kubaini changamoto zinazoweza kujitokeza na kuzitafutia suluhisho mapema.

Mhe. Kishenyi alisisitiza umuhimu wa kujifunza mara kwa mara na kuendelea kuhamasishana na kushirikiana katika kuongeza ufanisi wa utekelezaji wa hukumu. Aliwahakikishia kuwa mafunzo kwa njia ya mtandao yataendelea kulingana na kadri muda unavyoruhusu, hivyo akawataka washiriki kuwa tayari kujifunza na kushiriki kikamilifu wakati wowote inapojitokeza fursa hiyo.

Mhe. Kishenyi aliwataka washiriki kutekeleza yale yote waliyojifunza, huku akiwahimiza kuendelea kupanua maarifa na kushirikiana kwa lengo la kuboresha utoaji wa haki nchini.

Washiriki wa mafunzo hayo walikuwa ni Mahakimu Wafawidhi wa Mahakama za Mwanzo na pia yalihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Mahakama akiwemo Majaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya Mhe. Mashaka Said Kalunde Mhe. Victoria Nongwa ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Mafunzo Kanda ya Mbeya, Mhe. Mussa Pomo na Naibu Msajili Mfawidhi Mahakama Kuu, Kanda ya Mbeya Mhe. Aziza Temu.

Aidha, katika Mafunzo hayo yaliwezeshwa na Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Hakimu Mkazi Mbeya Mhe. Zawadi Laizer pamoja na Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Wilaya ya Momba Mhe. Raymond Venance Kaswaga

Vilevile, Mafunzo hayo yaliratibiwa na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Mwanzo Uyole Mhe. Ayubu M. Shellimo yalihusisha mada mbalimbali zenye lengo la kuboresha utendaji kazi wa Mahakama za Mwanzo katika kanda hiyo kwenye utekelezaji wa hukumu.

Aidha, mada zilizotolewa zilikuwa kama vile, taratibu sahihi za kukamata na kuuza mali, jukumu la madalali wa Mahakama na watoa huduma za mchakato wa utekelezaji wa hukumu, mbinu bora za uhamishaji wa tuzo za Mahakama, utunzaji wa kumbukumbu za utekelezaji wa hukumu na taratibu za kushughulikia mapingamizi.

Mafunzo hayo ni mwendelezo wa utoaji wa mafunzo endelevu yanayotolewa na Mahakama ya Tanzania kupitia Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto ambacho ni kitovu cha mafunzo na maarifa ya Mahakama ya Tanzania, kwa lengo la kuwajengea uwezo watendaji wa Mahakama katika nyanja mbalimbali za utoaji haki na ni sehemu ya utekelezaji Mpango Mkakati wa Mahakama ya Tanzania na Sera ya Mafunzo ya Kimahakama.

Sehemu ya Mahakimu wa Mahakama Kanda ya Mbeya inajumuisha Mikoa ya Mbeya na Songwe walioshiriki Mafunzo hayo hivi karibuni wakiwa kwenye picha ya pamoja.




(Habari Hii Imehaririwa na Innocent Kansha - Mahakama) 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni