Na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Mwanza
Jaji Mkuu wa Tanzania,
Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma amewahimiza Majaji Wafawidhi wa Mahakama Kuu ya
Tanzania kuendeleza mabadiliko ya kifikira na kimtazamo ili uwekezaji mkubwa wa
kimaboresho ambao umefanyika mahakamani ulete matokeo chanya kwenye mchakato mzima wa
utoaji haki kwa Wananchi.
Mhe. Prof. Juma ametoa
wito huo leo tarehe 17 Machi, 2025 alipokuwa anafungua Kikao cha Mwaka cha Majaji
Wafawidhi wa Mahakama Kuu, Kanda na Divisheni, kinachofanyika kwa siku tatu
katika Hoteli ya Malaika jijini hapa.
‘Maboresho hayawezekani
bila mabadiliko makubwa ya kifikra na mitazamo. Msukumo wa kimaboresho ambao
unaendelea lazima tuuendeleze. Kasi na uendelevu lazima tuuendeleze,’ Jaji Mkuu
amewaambia Majaji hao na Viongozi wengine Waandamizi wa Mahakama ya Tanzania
wanaohudhuria Kikao hicho.
Amebainisha kuwa tayari
uwekezaji mkubwa umefanywa katika Mfumo wa Tafsiri na Unukuzi, katika Mfumo wa
Usimamizi wa Mashauri na usikilizaji wa mashauri kwa njia ya mtandao, hivyo hayo
yote hayatadumu kama hawatayaendeleza na wenye uwezo wa kuyaendelea ni wao wenyewe.
Jaji Mkuu alitoa mfano wa
mpango mkubwa wa kudijiti nyaraka zote ambazo wanazitumia, ambao mwaka jana au
mwaka juzi ulipoanza kwa mara ya kwanza kulikuwepo na msisimko mkubwa.
‘Uwekezaji mkubwa ambao
tumeufanya ni lazima tuhakikishe unakuwa endelevu, vinginevyo tutashindwa
kuonesha kiasi kikubwa cha uwekezaji tuliofanya umeleta faida gani kubwa,’ Mhe.
Prof. Juma amesema.
Amewakumbusha Majaji hao
kuwa wanapozungumzia maboresho wanatakiwa kuhakikisha kwamba badala ya kutaja tu
uwekezaji mkubwa ambao wameufanya, waeleze pia faida kubwa ambazo wamevuna
kutokana uwekezaji huo.
‘Kuna faida nyingi sana
ambazo Mwananchi wa kawaida anapata baada ya sisi kuanza kutumia vifaa hivyo
vya kisasa katika utoaji haki. Mwananchi hapendi kusikiliza uwekezaji, bali
kuona matunda au matokeo ya uwekezaji huo mkubwa,’ Jaji Mkuu amesema.
Awali, akimkaribisha Jaji
Mkuu kufungua Mkutano huo, Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt.
Mustapher Mohamed Siyani, amewapongeza Majaji Wafawidhi hao kwa mafanikio
makubwa ambayo yamepatikana kwani takwimu zinaonesha kuongezeka kwa kasi ya utoaji haki nchini.
‘Bila shaka, kuongezeka kwa kasi ya umalizaji wa
mashauri na kupungua kwa idadi ya mshauri ya mlundikano ni jambo la kupongezwa.
Nichukue fursa hii kuwapongeza Majaji Wafawidhi kwa niaba ya Watumishi na Wadau wote wa Mahakama kwa mafanikio haya,’
amesma.
Jaji Kiongozi amebainisha
kuwa takwimu za mashauri zinaonyesha kwa
Mahakama Kuu, wastani wa kukamilika kwa shauri umeendelea kupungua, kutoka siku
381 kwa mwaka 2021 hadi siku 249
mwaka 2024, Mahakama za Hakimu Mkazi siku 187, Mahakama za Wilaya siku 131 na Mahakama za Mwanzo 37.
‘Hii inaleta hoja ya
kutafakari upya iwapo muda uliopo wa kutambua mashauri ya mlundikano unapaswa
kurekebishwa ili uendane na hali halisi ya mwenendo wa mashauri mahakamani,’
Mhe. Dkt. Siyani amesema.
Aidha, Jaji Kiongozi amebainisha kuwa kuwepo kwa
viwango maalum vya mashauri ambavyo Majaji na Mahakimu wanapaswa kumaliza kila
mwaka kumechangia kuhakikisha haki inapatikana kwa wakati.
Kadhalika, ameeleza kuwa
kwa mwaka 2024, wastani wa muda uliotumika tangu shauri kufunguliwa hadi
kukamilika ulikuwa ni siku 78, pungufu ya siku sita kutoka siku 84,
ukilinganisha na mwaka 2023.
Aidha, Mhe. Dkt. Siyani amesema
idadi ya mashauri ya mlundikano mbele ya Mahakama Kuu na Mahakama za chini yake
kwa mwaka 2024 imeendelea kupungua, kwani ni mashauri 451 pekee, sawa na asilimia 1.2 ya mashauri
37,674
yaliyobakia Disemba 2024, ndiyo yalikuwa
ya mrundikano.
‘Hii inaonyesha upungufu
wa asilimia 2 kutoka 3 kwa mwaka 2023. Mahakama za Watoto na za Mwanzo zilirekodi
asilimia 0 ya mashauri yaliyokuwa na mlundikano mwaka 2024,’ Jaji Kiongozi
amewaeleza washiriki wa Kikao hicho.
Mbali na kujadili masuala
mbalimbali yanayohusu utendaji wa Mahakama, Kikao hicho pia kinatoa fursa ya kujipima na
kujitathmini kuhusu utendaji kazi,
sambamba na utekelezaji wa Mpango Mkakati, Dira na Dhima ya Mahakama.
Aidha, Majaji wanapata fursa
muhimu ya kubadilishana uzoefu kwenye utendaji wa kazi za Mahakama, pamoja na
kutambua na kujadili changamoto mbalimbali zinazojitokeza katika Mahakama Kuu
na Mahakama za chini yake na hivyo kutafuta
majibu kwa changamoto hizo.
Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Chiganga Tengwa akitoa maelezo ya utangulizi kuhusu Kikao hicho.
Meza Kuu inayoongozwa na Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma-katikati. Wengine ni Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Mustapher Mohamed Siyani-wa pili kushoto, Rais wa Mahakama ya Afrika na Haki za Binadamu, Mhe. Iman Aboud-wa pili kulia, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Mwanza, Mhe. Dkt. Kilekamajenga-wa kwanza kushoto na Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Eva Nkya-wa kwanza kulia.
Meza Kuu ikionmgozwa na Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma-katikati waliokaa-ikiwa katika picha ya pamoja na Majaji Wafawidhi-juu na chini-wanaohudhuria Kikao hicho.
Meza Kuu ikionmgozwa na Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma-katikati waliokaa-ikiwa katika picha ya pamoja na Majaji wengine wa Mahakama Kuu ya Tanzania ambao wamealikwa kuhudhuria Kikao hicho.
Meza Kuu ikionmgozwa na Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma-katikati waliokaa-ikiwa katika picha ya pamoja na Wajumbe wa Menejimenti ya Mahakama ya Tanzania wanaohudhuria Kikao hicho. Picha chini ni Wajumbe wa Sekretarieti ya maandalizi ya Kikao hicho.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni