Na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Mwanza
Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan atazindua rasmi jengo la
Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania lililopo katika eneo la Tambuka Reli jijini
Dodoma tarehe 8 Aprili, 2025.
Hayo yamebainishwa leo
tarehe 17 Machi, 2025 na Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma alipokuwa
anafungua Kikao cha Mwaka cha Majaji Wafawidhi wa Mahakama Kuu, Kanda na
Divisheni, kinachofanyika kwa siku tatu katika Hoteli ya Malaika jijini hapa.
‘Tarehe 8 Aprili, 2025 ni
siku muhimu sana kwa Mahakama. Hilo ni jengo la kisasa. Tunawaomba wale
watakaolitumia jengo hili wahakikishe kwamba linakuwa kweli la kisasa hata kwa
huduma, siyo kwa muonekano tu,’ amesema.
Mhe. Prof. Juma ameeleza
kuwa jengo hilo limejengwa kwa asilimia 100 na kodi za Wananchi na halikutokana
na mradi wa Benki ya Dunia na kwamba jumla ya kiasi cha Shilingi za Kitanzania bilioni
129.7 zimetumika kwenye mradi huo.
‘Kwa hiyo, jengo hili ni mali
ya Wananchi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Tuhakikishe kwamba jengo hili linakuwa
la kisasa kweli, vyumba vyake vinakuwa na teknolojia. Lazima iwe tofauti na
Mahakama zingine unapoingia kwenye Mahakama ya karne ya 21,’ Jaji Mkuu amesema.
Mhe. Prof. Ibrahim Juma
amesisitiza matumizi ya mkutano mtandao wakati wa kusikiliza mashauri kwenye
jengo hilo, hatua itakayochochea kupunguza mlundikano mahakamani.
Hivyo amewahimiza Majaji
Wafawidhi kuwasaidia Magereza ili wawe na vyumba vizuri wezeshi vitakavyotumia
teknolojia hiyo kutokana na changamoto inayowakabili ya kuwasafirisha Wafungwa
wanaokata rufaa kutoka Magereza ya mbali na kuwaleta mahakamani.
‘Kuwasafirisha Wafungwa
pengine kuwaleta Arusha, kutoka Songea kwenda Moshi ni gharama kubwa na kiusalama
siyo salama. Magereza wametuomba tuongeze matumizi ya teknolojia katika kusikiliza
mashauri,’ amesema.
Kazi za ujenzi katika mradi huo zilianza Julai 2020 na Jaji Mkuu wa Tanzania aliweka jiwe la msingi wa jengo hilo tarehe 26 Januari, 2022. Jengo hilo lipo kwenye eneo la ukubwa wa hekta 18.9, takribani hekali 45.
Akiwasilisha taarifa ya
ujenzi katika hafla ya kuweka jiwe la msingi, Mtedaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole
Gabriel aliishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kutoa fedha za utekelezaji wa mradi huo kwa
wakati.
Kwa mujibu wa Mtendaji
Mkuu, kwa miaka mingi Mhimili wa Mahakama haukuwa na jengo la Makao Makuu,
hivyo jitihada zilizanza mwaka 2013. Jengo hilo ilikuwa lijengwe katika eneo la
Chimala jijni Dar es Salaam, karibu na jengo refu lile linalochungulia Ikulu ya
Magogoni.
Alisema kuwa baada ya
mipango ya Serikali kuwa Makao Makuu ya Nchi yanahamia Dodoma, mchakato huo
uligeuza mwelekeo na ikaonekana jengo hilo lijengwe jijini Dodoma.
Prof. Ole Gabriel alisema
kuwa mwaka 2017 mchakato huo ulipata msukumo pale ambapo Jaji Mkuu mwenyewe
ulipoongea na Rais wa Awamu ya Tano, Hayati Dkt John Pombe Magufuli ili kuweza
kupata eneo jijini Dodoma.
“Baada ya hapo kasi
iliongezeka ambapo majadiliano yaliendelea na iliyokuwa Mamlaka ya Ustawishaji
Makao Makuu (CDA) na baadaye Mamlaka ya Jiji la Dodoma na eneo hili likapatikana,’
alisema.
Mtendaji Mkuu aliwataja
wanaosimamia ujenzi ni CRJE, Kampuni ya Kichina ambao wamefanya kazi kubwa na
kazi yao ni ya viwango vya hali ya juu, huku akibainisha Wasanifu wa jengo hilo
wakiwa ni Acquise Achtectural Design ambao ni wazalendo.
Alibainisha pia kuwa
jengo hilo lina matawi matatu ambayo ni Mahakama ya Upeo (Supreme Court),
Mahakama ya Rufani na Mahakama Kuu. Prof. Ole Gabriel alieleza kuwa matawi hayo
yanatengeneza jengo katikati litakalokuwa linatumika kama ofisi za utawala.

Hakuna maoni:
Chapisha Maoni