Na MAGRETH KINABO- Mahakama, Mwanza
Jumla ya mashauri 244,808 yameamuliwa katika kipindi cha mwaka 2024 ngazi ya Mahakama Kuu na Mahakama zilizopo chini yake, Mkurugenzi wa Menejimenti ya Usimamizi wa Mashauri wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Desdery Kamugisha amekiambia Kikao cha Majaji Wafawidhi wa Mahakama Kuu Kanda na Divisheni kinachoendelea kufanyika jijini Mwanza.
“Kiwango cha jumla cha umalizaji mashauri kimepanda kutoka asilimia 100 mwaka 2023 hadi asilimia 101 kwa kipindi cha mwaka 2024,” na uondoshaji mashauri kimepanda toka asilimia 83 hadi asilimia 84,” amesema Mhe. Kamugisha.
Aidha Mhe. Kamugisha alifafanua kwamba katika Mahakama Kuu (HC,) na Mahakama za Mwanzo (PC) zilikuwa na asilimia101 za umalizaji mashauri na asilimia 85 za uondoshaji wa mashauri.
Mkurugenzi huyo ameongeza kwamba wastani wa jumla wa mzigo wa kazi umepungua kutoka 234 hadi 228 kwa ngazi zote za Mahakama isipokuwa Mahakama Kuu ya Tanzania na Mahakama ya Rufani Tanzania.
Alizitaja sababu za kupungua kwa mzigo huo, kuwa ni kuongezeka kwa Jaji mmoja wa Mahakama ya Rufani Tanzania na Majaji Watano wa Mahakama Kuu ya Tanzania, ikiwemo kuwepo kwa ajira mpya za Mahakimu 92.
Kuhusu idadi ya Wahe. Majaji waliofikisha mashauri 220 amesema imeshuka kutoka 46 mwaka 2023 hadi 17 mwaka 2024., sambamba na Idadi ya Mahakimu wa Mahakama za Hakimu Mkazi na Mahakama za Wilaya (RM & DC) waliofikisha mashauri 250 imezidi kupungua kwa mwaka wa tatu mfululizo kutoka 52 (2022), 50 (2023) hadi 30 (2024).
Hata hivyo ametaja idadi ya Mahakimu 279 wa Mahakama za Mwanzo ambao wamefikisha lengo la mashauri 270 kwa mwaka.
Wakati huohuo, Jaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania, Mhe.Dkt.Benhajj Masoud akitoa mada kuhusu Malezi ya Kitaaluma amesema ili Majaji hao kuweza kuendelea kutekeleza vyema majukumu yao upo umuhimu wa kuendelea na programu ya ushauri kwa watu wanaofanyanao kazi katika Kanda zao.
Ni lazima kuwafahamu watu wako unaofanya nao kazi na kuwasaidia katika utendaji wa kazi na mahitaji yao, ikiwemo kushirikiana nao kwenye masuala mbalimbali.
Katika hatua nyingine, Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano(TEHAMA) wa Mahakama ya Tanzania,Bw. Kalege Enock akitoa mada kuhusu masuala ya teknolojia hiyo amesema Mahakama imeajiri Maofisa TEHAMA wapya wengi, hivyo upo umuhimu wa kuwapatia mafunzo kabla ya kuwakabidhi majukumu yao ya kazi. Kupitia uzoefu wa nchi zilizopiga hatua.
Amesisitiza kwamba iko haja ya kutengeneza sera ya TEHAMA, ikiwemo kuendelea kujenga uwezo watumishi wa Mahakama mbalimbali mfano Majaji, Mahakimu, Wadau wa Sheria, Makarani na Maofisa TEHAMA.Pia kuendelea kushirikiana na taasisi za kimataifa.
“Kwenye eneo hili tunahitaji kuwa na bajeti endelevu, ili kukidhi haja, ” amesema Enock.
Amesema wataendelea kupanua miundombinu ya TEHAMA ili iweze kuendelea kuwa rafiki kwa watumiaji, ikiwemo kushirikiana na sekta binafsi kwa ajili ya kupata mbinu mpya za ubunifu wa masuala ya TEHAMA.
Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Menejimenti ya Mashauri wa Mahakama ya Tanzania, (DCM) Mhe. Desdery Kamugisha alipokuwa akitoa taarifa ya Mashauri kwa Mwaka 2024 kwenye Kikao cha Mwaka cha Majaji Wafawidhi wa Mahakama Kuu, Kanda na Divisheni, kinachofanyika kwa siku tatu katika Hoteli ya Malaika jijini Mwanza.
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe.Dkt. Mustapher Mohamed Siyani akiongoza Kikao hicho.
Jaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania, Mhe. Dkt.Benhajj Masoud akitoa mada kuhusu Malezi ya Kitaaluma.
Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano(TEHAMA), Bw. Kalege Enock akitoa mada kuhusu masuala ya teknolojia hiyo.
\Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma(kushoto) na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza, Mhe.Dkt.Ntemi Kilekamajenga(kulia) wakifuatilia mada ya TEHAMA. Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Shinyanga, Mhe.Frank Mahimbali.
Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Eva Nkya(kulia) na Msajili wa Mahakama ya Rufani Tanzania, Mhe.George Egbert(kushoto) wakizungumza jambo.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Salma Maghimbi akiuliza jambo kuhusu TEHAMA.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kituo cha Usuluhishi, Mhe. Zahra Maruma akichangia mada ya TEHAMA.
Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano(TEHAMA), Bw. Kalege Enock akijibu maswali kuhusu mada ya teknolojia hiyo.
Sekretarieti ikifutilia masuala mbalimbali ya Kikao hicho.
















Hakuna maoni:
Chapisha Maoni