Na ASHA JUMA-Mahakama, Morogoro
Watumishi wa
Mahakama wanaotarajia kustaafu kutoka katika Mikoa na Kada mbalimbali wamepata
semina maalum kuhusu namna ya kuweza kukabili maisha baada ya kustaafu.
Mafunzo hayo yanafanyika
kwa mujibu wa sera ya mafunzo ya Mahakama ya 2019. Sera hiyo inaelekeza Watumishi
wa Mahakama wajengewe uwezo wa kujiandaa kustaafu ili waweze kukabili maisha
baada ya kustaafu.
Mafunzo hayo ya
siku sita yanayofanyika katika Ukumbi wa Mikutano kwenye Kituo Jumuishi cha
Utoaji Haki-IJC- Morogoro yalifunguliwa jana tarehe 17 Machi, 2025 na Kaimu
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Morogoro, Mhe. Stephen Magoiga.
Washiriki wa
mafunzo hayo ni Watumishi wa Mahakama kutoka Makao Makuu, Mahakama ya RufanI, Kanda
na Divisheni za Mahakama Kuu.
Mafunzo hayo yanaratibiwa
na Mahakama na yanatolewa kwa kushirikiana na Wataalam kutoka Taasisi
mbalimbali kama PSSSF, NSSSF, UTT-AMIS, Viongozi wa Dini na Wataalam wa Afya
kutoka Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.
Miongoni mwa mada
zitakazowasilishwa ni pamoja na masuala muhimu ya kiafya, taratibu za kisheria za
maandalizi ya kustaafu, stahiki na haki za mtumishi kabla na baada ya kustaafu,
bima ya afya, ujasiliamali, mafao ya kustaafu, mirathi ya Watumishi, mifuko ya uwekezaji
na masuala ya kiroho.
Akizungumza wakati
wa ufunguzi wa mafunzo hayo, Mhe. Magoiga aliwaeleza wastaafu kuwa mafunzo hayo
yatawapa mbinu za kukabiliana na changamoto mbalimbali, kuwapa maisha yenye
tija, furaha na ustawi hata baada ya kustaafu.
“Mafunzo haya ni
kwa ajili ya kuwatoa hofu kwani hofu inaua, kustaafu ni kuanza upya na
kutafakari juu ya utumishi wenu,” alisema.
Mhe Magoiga aliwashukuru
Watumishi hao kwa utendaji wao wa kazi akisema, “Nyinyi mna mchango mkubwa sana
na tunautambua, katika mchakato mzima wa utafutaji haki, nyinyi pia mlikua na
mchango mkubwa bila kujali kada zenu.”
Kaimu Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Morogoro, Mhe. Stephen Magoiga na Naibu Msajili, Mhe. Susan Kihawa-kushoto na kulia ni Mkurugenzi Msaidizi wa Mafunzo, Bi. Patricia Ngungulu wakifuatilia yaliyokuwa yanajiri wakatinwa ufunguzi wa mafunzo hayo.
Watumishi kutoka sehemu mbalimbali wakifuatilia mafunzo.
Kaimu Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya
Tanzania, Kanda ya Morogoro, Mhe. Stephen Magoiga akiwa na Watumishi mbalimbali
na Wawezeshaji wa mafunzo.
Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Mwanza.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni