Na HUBERT MAANGA-Mahakama, Mtwara
Katika juhudi za
kuimarisha ufanisi wa Mahakama na kuboresha utendaji wa Mahakimu, Mahakama Kuu
ya Tanzania, Kanda ya Mtwara, imekabidhi kompyuta mpakato kwa Mahakimu wapya wa
Mahakama za Mwanzo walioteuliwa hivi karibuni katika Mkoa huo.
Hafla ya makabidhiano
ilifanyika hivi karibuni katika jengo la Mahakama Kuu, ikiendeshwa na Jaji
Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Kanda ya Mtwara, Mhe. Edwin Kakolaki, huku ikiwa
na lengo la kuwawezesha Mahakimu kuendesha mashauri kisasa na kidigitali zaidi
katika shughuli zao kimahakama.
Akizungumza wakati wa
hafla hiyo, Mhe. Kakolaki alisisitiza kutimiza waraka wa Jaji Mkuu wa Tanzania
wa kujikita kwenye TEHAMA kwani katika shughuli za sasa za Mahakama, matumizi
ya mifumo ya kidijitali kama eCM, na Primary Court App ndio mwenendo wa sasa wa
utoaji wa haki wa haraka na uwazi.
"Nyie mmekuja muda
mzuri ambapo Mahakama inaondokana na mfumo wa makaratasi, majalada yote
yanapatikana kwenye mifumo. Hii ni fursa kwenu kuendesha mashauri ndani ya muda
mfupi kwani mabadiliko haya yamerahisisha namna ambavyo Mahakama zetu
zinahudumia Wananchi,’ alisema.
Mahakimu walionufaika na
kompyuta hizo waliishukuru Mahakama kwa kuwapatia nyenzo ambazo zitarahisisha
usimamizi wa mashauri, maandalizi ya hukumu na utoaji wa huduma kwa wananchi.
Waliahidi kujituma katika
kutimiza majukumu yao kwa uadilifu na weledi ili kuimarisha huduma za Mahakama
katika Mkoa wa Mtwara.
Jumla ya Mahakimu wanne walikabidhiwa vitendea kazi hivyo ambao ni Mhe.
Mainda Sengeda wa Mahakama ya Mwanzo Dihimba, Mhe. Caroline Butambala wa
Mahakama ya Mwanzo Lulindi, Mhe. Delphina Charles wa Mahakama ya Mwanzo Nakopi
na Mhe. Magori Nyamwoyo wa Mahakama ya Mwanzo Mnyambe.
Katika makabidhiano hayo,
waliohuduria ni pamoja na Naibu Msajili wa Mahakama Kuu, Kanda ya Mtwara, Mhe.
Seraphine Nsana, Mtendaji wa Mahakama Kuu, Kanda ya Mtwara, Bw. Yussuph
Msawanga na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Mtwara, Mhe.
Charles Mnzava.
Jaji Mfawidhi wa
Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Mtwara, Mhe. Edwin Kakolaki (kulia) akizungumza
kabla ya kukabidhi vitendea kazi kwa Mahakimu wapya wa Mahakama za Mwanzo.
.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni