Na Hilari Herman – Mahakama, Lindi
Watumishi Mahakama ya Hakimu Mkazi na Wilaya ya Lindi
wamefanya kikao cha kawaida cha ndani kikiongozwa Viongozi wa Mahakama hiyo
ambao ni Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Hakimu Mkazi Lindi Mhe. Consolata
Peter Singano na Mtendaji wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Lindi Bi. Quip Godfrey
Mbeyela. Kikao hicho kilifanyika katika ukumbi wa wazi wa Mahakama ya Hakimu
Mkazi Lindi  hivi karibuni.
Akizungumza wakati wa kufungua kikao hicho Mhe. Singano
amewataka watumishi wa Mahakama hizo kuzingatia zaidi suala la nidhamu mahala
pa kazi huku akisisitiza watumishi wa Mahakama kuongeza uwajibikaji, uadilifu
na ueledi katika kutekeleza majukumu yao. 
“Hayati Mwl. Nyerere aliwahi kusema kuwa mtu yeyote
asiye na maadili anaweza kufanya kazi nyingine lakini siyo uhakimu au ujaji na
hii nikutokana na unyeti wa kazi hii. Natambua walizungumziwa Mahakimu na
Majaji lakini watu hao hawafanyi kazi peke yao hivyo niwaombe Mahakimu na
watumishi wenzangu tuwe waadilifu na wenye nidhamu,” alisema Mhe. Singano
 Mhe. Singano
amesisitiza kwa watumishi hao kuwa na mawasiliano mazuri mahali pa kazi miongoni
mwao wenyewe, watumishi kwa viongozi na watumshi kwa wateja, huku akiwataka
watumishi hao kutambua kuwa mawasiliano mazuri huleta afya hasa ya maelewano
mazuri, upendo, utatuzi wa masuala yanayoleta maswahibu, undugu, ushirikiano na
zaidi kufikia mwafaka pasi na mgongano wa aina yoyote.
Kwa upande wake, Mtendaji wa Mahakama ya Hakimu Mkazi
Lindi. Bi. Quip Godfrey Mbeyela amewahimiza watumishi kujali afya zao hasa kwa kufanya
mazoezi kwa kutekeleza agizo aliloto Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Kanda ya
Mtwara Mhe. Edwin Elias Kakolaki. Aidha amewataka watumishi kuchukua hatua
madhubuti kwakufanya uchunguzi wa afya zao (body checkup) kwa lengo
lakujua  afya zao. 
“Nataka
kila mmoja afanye uchunguzi wa afya yake ili ajue yupo imara kiasi gani jambo hii
litaenda sambamba na ushauri wa kitabibu 
kujua ni aina gani ya vyakula unatakiwa kula, mazoezi gani unatakiwa
kufanya na mambo mengine kadha wa kadha kulingana na ushauri wa kitabibu,” alisema
Mtendaji huyo
Viongozi hao vilevile waliwatambulisha watumshi wapya
wa kada mbalimbali akiwemo Mtumishi aliyehamia ambaye ni Hakimu Mkazi
Mwandamizi Mahakama ya Wilaya ya Lindi Mhe. Khalfan Khalfan, Watumishi ajira
mpya akiwemo Afisa Tehama Bw. Furaha Khatibu, Afisa hesabu Bw. Othmani Chimko, Afisa
Ugavi Msaidizi Bw Abeid Omar, Fundi sanifu wa Mifumo ya Maji Bi. Ansila Mziray
na Mlinzi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Lindi Bw. Jackson C. Clialence. 
Zoezi hilo lilienda sambamba na utambulisho Msaidizi
wa Kumbukumbu Mkuu Bw. Selemani Chikumba aliyekuwa masomoni kwa mwaka moja
akisoma Shule ya Sheria kwa vitendo Zanzibar.
Kikao hicho kilihitimishwa kwa watumishi kumjua
mtumishi hodari wa mwezi Februari ambae ni Bi. Mwanate Ally akihudumu kama
Msaidizi wa Ofisi Mkuu. Huu ukiwa ni mwendelezo wa utoaji wa motisha kwa
wafanyakazi wa Mahakama hizo ambao ni wabunifu, wenye bidii ya kazi, wanaofanya
kazi  vizuri kwa mwezi husika.
Mtendaji wa
Mahakama ya Hakimu Mkazi Lindi Bi. Quip Godgrey Mbeyela  akimkabidhi zawadi ya ufanyakazi hodari Bi.
Mwanate Ally (kushoto) anayehudumu kama Msaidizi wa Ofisi Mkuu. 
Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Hakimu Mkazi Lindi Mhe. Consolata Peter Singano (aliyekaa nyoosha mikono) akitoa neno wakati wa ufunguzi wa kikao.
Hakimu Mahakama
ya Wilaya ya Lindi Mhe.Khalfan Khalfan akichangia mada wakati wa kikao
Mtendaji wa
Mahakama ya Hakimu Mkazi Lindi Bi. Quip Godfrey Mbeyela  (aliyesimama ) akielezea moja ya ajenda ya
kikao.






Hakuna maoni:
Chapisha Maoni