Jumatano, 19 Machi 2025

KIKAO CHA MAJAJI WAFAWIDHI MWANZA CHAHITIMISHWA

  • Watoka na maazimio kadhaa kuboresha utendaji

Na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Mwanza

Kikao cha Majaji Wafawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda na Divisheni, kilichokuwa kinafanyika jijini hapa kimehitimishwa leo tarehe 19 Machi, 2025, huku Viongozi hao wakitoka na maazimio kadhaa yanayolenga kuboresha huduma za utoaji haki kwa Wananchi.

Kabla ya Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Dkt. Mustapher Mohamed Siyani, ambaye alikuwa Mwenyekiti, kuhitimisha Kikao hicho, Majaji Wafawidhi walipokea mada tatu zilizowasilishwa na wataalam wa ndani ya Mahakama.

Mada ya kwanza iliwasilishwa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Manyara, Mhe. John Kahyoza kuhusu matumizi ya Mifumo katika kutekeleza majukumu ya Jaji Mfawidhi.

Mkurugenzi wa Usimamizi na Ukaguzi wa Huduma za Kimahakama, Mrejesho kwa Umma na Maadili wa Mahakama ya Tanzania, ambaye pia ni Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Maira Kasonde, aliwasilisha taarifa ya ukaguzi wa Mahakama.

Kadhalika, Jaji Mfawidhi wa Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia, Mhe. Mwanabaraka Mnyukwa alitoa uzoefu kuhusu usimamizi wa mashauri ya mirathi baada ya uteuzi wa msimamizi.

Katika maazimio hayo, Majaji hao wamehimiza changamoto zinazozitokeza kwenye matumizi ya Mfumo wa Tafsiri na Unukuzi Pamoja na Mifumo mingine ziendelee kuibuliwa na kutafutiwa ufumbuzi ili kuboresha ufanizi.

Majaji hao pia wameazimia kuwa Maafisa wote wa Mahakama wapatiwe kompyuta mpakato kama sehemu ya kitendea kazi, kwa kuwa sasa Mahakama hatumii karatasi.

Kadhalika, Majaji Wafawidhi wameazimia kuwa kuwepo na progamu za unasihi kwa Maafisa wa Mahakama katika kila Kanda na Divisheni za Mahakama Kuu kama inavyoelekezwa katika Mwongozo wa Malezi ya Kitaalam ya Maofisa wa Mahakam awa mwaka 2025.

Baadhi ya Viongozi wa Mahakama wanaohudhuria Kikao hicho ni Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Msajili wa Mahakama ya Rufani, Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mtendaji wa Mahakama Kuu-Kanda, Mtendaji wa Mahakama Kuu-Divisheni, Msajili Mwandamizi wa Mahakama Kuu, Wakurugenzi mbalimbali, Naibu Wasajili na wengine.

Mbali na kujadili masuala mbalimbali yanayohusu utendaji wa Mahakama, Kikao hicho pia kilitoa fursa ya kujipima na kujitathmini kuhusu utendaji kazi, sambamba na utekelezaji wa Mpango Mkakati, Dira na Dhima ya Mahakama.

Aidha, Majaji walipata fursa muhimu ya kubadilishana uzoefu kwenye utendaji wa kazi za Mahakama, pamoja na kutambua na kujadili changamoto mbalimbali zinazojitokeza katika Mahakama Kuu na Mahakama za chini yake na hivyo kutafuta majibu kwa changamoto hizo.

Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Mustapher Mohamed Siyani akiendesha Kikao cha Majaji Wafawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda na Divisheni katika siku ya tatu leo tarehe 19 Machi, 2025 jijini Mwanza. Katika siku ya tatu ya Kikao hicho, mada mbalimbali ziliwasilishwa na kujadiliwa.

Jaji John Kahyoza akiwasilisha mada kuhusu matumizi ya mifumo katika kutekeleza majukumu ya Jaji Mfawidhi.

Mkurugenzi wa Usimamizi na Ukaguzi wa Huduma za Kimahakama, Mrejesho kwa Umma na Maadili wa Mahakama ya Tanzania, ambaye pia ni Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Maira Kasonde, akiwasilisha taarifa ya ukaguzi wa Mahakama.

Jaji Mfawidhi wa Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia, Mhe. Mwanabaraka Mnyukwa alitoa uzoefu kuhusu usimamizi wa mashauri ya mirathi baada ya uteuzi wa msimamizi.


Jaji Mfawidhi wa Majakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Kigoma, Mhe. Augustine Rwizile akichangia mada kwenye Kikao hicho.


Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kituo cha Usuluhishi, Mhe. Zahra Maruma naye hakuwa nyuma kuchangia mada zilizowasilishwa.


Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Mwanza, Mhe. Dkt. Ntemi Kilekamajenga akichangia mada hizo.


Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Tabora, Mhe. Dkt. Adam Mambi akichangia mada zilizowasilishwa.


Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Shinyanga, Mhe. Frank Mahimbali naye hakubaki nyuma.


Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Mbeya, Mhe. Joachim Tiganga akichangia mada hizo.


Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Arusha, Mhe. Ilvin Mugeta akichangia mada zilizowasilishwa.


Rais wa Mahaama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu, Mhe. Iman Aboud naye hakubaki nyuma kuchangia mada hizo.




Hakuna maoni:

Chapisha Maoni