- Ahimiza matumizi ya mifumo kwenye utoaji haki
Na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Mwanza
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt.
Mustapher Mohamed Siyani amewahimiza Majaji Wafawidhi kuzidisha matumizi ya
mifumo ili kufikia azma ya Mahakama ya Tanzania ya kuachana na karatasi katika
shughuli zote za kimahama.
Mhe. Dkt. Siyani ametoa wito huo leo tarehe 19 Machi,
2025 alipokuwa anafunga Kikao cha Majaji Wafawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania,
Kanda na Divisheni, kilichokuwa kinafanyika jijini hapa.
‘Uzoefu
tulioupta kutoka Kanda ya Geita ni uthibitisho tosha kwamba matumizi ya
e-judiciary yanawezekana na changamoto chache za kimfumo hazitoshi kuwa sababu za
kuturudisha nyuma kwenye karatasi,’ Jaji Kiongozi amesema.
Amewakumbusha
Majaji Wafawidhi hao kuwa kwenye kikao chao walijadiliana pia kuhusu matumizi
ya mifumo ya e-judiciary katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku. 
Kadhalika,
aliwakumbusha kuwa kwa muda mrefu, Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis
Juma na viongozi wengine wa Mahakama, wamekuwa wakisisitiza kuachana na
matumizi ya karatasi na badala yake kuhakikisha huduma za haki zinatolewa
kisasa kwa njia ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano-TEHEMA. 
‘Katika
hotuba yake ya ufunguzi, Jaji Mkuu alisisitiza matumizi ya TEHEMA na taarifa zilizomo
katika mifumo yetu, hasa takwimu za mashauri mbalimbali kufanya maamuzi… 
‘Bila
shaka, kupitia mifumo yake, Mahakama ina chakata taarifa nyingi ambazo
zikitumika ipasavyo zitasaidia sana kuboresha huduma za haki, ikiwemo kujulisha
maeneo yanayohitaji mitizamo mipya ya sheria, tabia za jamii zinazotuzunguka
katika vituo vyetu vya kazi na nini kifanyike ili kudumisha haki na amani
kwenye maeneo husika,’ Mhe. Dkt. Siyani amesema. 
Jaji
Kiongozi amebainisha kuwa Jaji Mkuu ameelekeza na Watumishi wa TEHAMA
wametekeleza kwa kutengeneza daftari maalumu(ledger) kwa ajili ya kusajili
changamoto zozote za kimfumo ili kuwajulisha wajenzi kuzitafutia ufumbuzi na
hivyo kujenga uwajibikaji. 
Kwa mujibu wa Mhe. Dkt. Siyani, hali
ilivyo kwa sasa bado kuna baadhi ya Kanda zinapokea nyaraka za mashauri kupitia
mfumo na kisha kuitisha nakala ngumu ili kufungua majalada ya mashauri. 
‘Hii
si sahihi. Mbali na kuchelewesha kufikia azma ya kuwa mahakama isiyotumia karatasi,
matumizi ya karatasi yanaiongezea Mahakama gharama ambazo TEHAMA imeshaleta
unafuu wake… 
‘Fedha
zinazotumika kununulia karatasi na majalada zingeliweza kutatua changamoto
zingine kwenye Kanda zenu ikiwemo kuweka mazingira bora ya kazi na kuongeza ari
kwa Watumishi,’ amesema.
Jaji
Kiongozi amebainisha pia kuwa baada ya kuwa wameweza kutumia mifumo kusajili na
kusikiliza mashauri kwa mwaka mzima uliopita, haitarajiwi tena sasa kushuhudia
utaratibu wa zamani wa kutumia karatasi katika utaoaji huduma au kuchanganya
baina ya mifumo sambamba na karatasi. 
‘Tumeona
mifano ya kanda zinazotumia mifumo kwa asilimia100 na hivyo hakuna sababu kwa
nini sote tusifanye hivyo. Ninajua baadhi yenu mnahofia kwamba kuna siku mifumo
itashindwa kufanya kazi,’ amesema. 
Mhe.
Dkt. Siyani amewatoa hofu Majaji Wafawidhi hao kuwa mifumo ya Mahakama
imejengwa na kuhakikiwa na wataalamu wa ndani, ina ulinzi wa kutosha na kuna hifadhi
kubwa, hivyo hakuna kumbukumbu itakayopotea. 
Baadhi ya Viongozi wa Mahakama waliohudhuria Kikao
hicho ni Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Msajili wa Mahakama ya Rufani,
Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mtendaji wa Mahakama Kuu-Kanda, Mtendaji
wa Mahakama Kuu-Divisheni, Msajili Mwandamizi wa Mahakama Kuu, Wakurugenzi
mbalimbali, Naibu Wasajili na wengine.
Mbali na kujadili masuala
mbalimbali yanayohusu utendaji wa Mahakama, Kikao hicho pia kilitoa fursa ya
kujipima na kujitathmini kuhusu utendaji kazi, sambamba na utekelezaji wa
Mpango Mkakati, Dira na Dhima ya Mahakama.
Aidha, Majaji walipata
fursa muhimu ya kubadilishana uzoefu kwenye utendaji wa kazi za Mahakama,
pamoja na kutambua na kujadili changamoto mbalimbali zinazojitokeza katika
Mahakama Kuu na Mahakama za chini yake na hivyo kutafuta majibu kwa changamoto
hizo.
Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Chiganga Tengwa akitoa maelezo ya utangulizi kabla ya kumkaribisha Jaji Kiongozi kufunga Kikao hicho.
 
 
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni