Ijumaa, 14 Machi 2025

MAHAKIMU WAPYA WAKABIDHIWA VIPAKATALISHI MBEYA

Na Mwinga Mpoli – Mahakama, Mbeya

Mahakimu waajiriwa wapya mkoani Mbeya wamekabidhiwa vitendea kazi ikiwemo Vipakatalishi (laptops) na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Mbeya Mhe. Joachim Charles Tiganga, makabidhiano hayo yamefanyika leo tarehe 14 Machi, 2025 katika ofisi ya Jaji Mfawidhi wa Kanda hiyo.

Akiongea na Mahakimu hao wakati wa kuwakabidhi vifaa kazi hivyo Mhe. Tiganga amewaasa Mahakimu hao juu ya matumizi sahihi ya vifaa hivyo vya kazi, vilevile aliwakumbusha kwenda kufanya kazi kwa kuzingatia misingi ya maadili, weledi, kujituma na kusimamia viapo vyao vya uhakimu.

“Leo tutawakabidhi komputa mpakato (laptops) mpya za kisasa kama moja ya nyenzo za kazi na Mahakama yetu kwa sasa ni ya kidigitali hivyo mmewezeshwa na mwajiri ili kurahisisha kutenda kazi zenu kidigitali. Tunategemea mtafanya kazi zenu vizuri mkitimiza lengo la umalizaji wa mashauri 260 kwa mwaka kama ilivyo lengo la upimaji utendaji kazi kwa Mahakama za Mwanzo. Nasisistiza mkafanye kazi kwa weledi, kujituma na kuwajibika huku mkisimamia viapo vyenu vya uhakimu,” alisema Jaji Tiganga

Aidha, Mhe. Tiganga akatoa rai kwa Mahakimu hao kuanza kukimbizana na kazi ya kusikiliza na kuamua mashauri ili waende sambamba na Mahakimu wenzao, na pia kuhakikisha  wanaandika  maamuzi ambayo yana hoja zilizojadiliwa kwa kina na kushirikiana na wenzao katika vituo vyao vya kazi na kuheshimu nafasi ya kila mtumishi.

“Tuna matarajio makubwa kutoka kwenu hivyo ninyi kama vijana tumieni nguvu zenu, akili na maarifa kufanya kazi zenu,” aliongeza Mhe. Tiganga

Mahakimu waliokabidhiwa vifaa kazi hivyo ni Mhe. Franco Deogratius Isuja, Mhe. Gift Isack Massawe na Mhe. Joseph George Singano.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Kanda ya Mbeya Mhe. Joachim Charles Tiganga akimkabidhi vitendea kazi Hakimu Mpya Mhe. Franco Deogratius Isuja.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya Mhe. Joachim Charles Tiganga akimkabidhi vitendea kazi Hakimu Mpya Mhe. Joseph George Singano.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya Mhe. Joachim Charles Tiganga akimkabidhi vitendea kazi Hakimu Mpya Mhe. Gift Isack Massawe.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya Mhe. Joachim Charles Tiganga (katikati) akiongea wakati wa makabidhiano ya vitendea kazi hivyo.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Kanda ya Mbeya Mhe. Joachim Charles Tiganga (katikati) akiwa kwenye picha ya pamoja na Mahakimu Wapya waliokabidhiwa Vipakatalishi leo tarehe 14 Machi, 2025 wa pili kutoka kushoto ni Naibu Msajili Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Kanda ya Mbeya Mhe. Aziza Emily Temu.

(Habari Hii Imehaririwa na Innocent Kansha - Mahakama)


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni