Ijumaa, 14 Machi 2025

JAJI MKUU AONGOZA JOPO LA MAJAJI KUSIKILIZA MASHAURI YA RUFAA 34 MUSOMA


 

Na KANDANA  LUCAS -Mahakama, Musoma

 

Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma ameongoza jopo la Majaji wa Mahakama ya Rufani kusikiliza mashauri katika Masjala ndogo ya Mahakama hiyo ilipo kwenye jengo la Mahakama   Kuu ya Tanzania Kanda ya Musoma, akiwa ni Mwenyeti wa jopo hilo.  

 

Katika kikao  cha ufunguzi (pre-session meeting) ambacho kilihusisha wadau mbalimbali kilichofanyika hivi karibuni,ambapo awali  Jaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania, Mhe. Dkt. Mary Caroline Levira aliimwakilisha Jaji Mkuu alitoa rai kwa wadau wote wanaohusika kuonesha ushirikiano ili kuhakikisha mashauri yote yaliyopangwa yanasikilizwa na kuamuliwa bila kukwama.

 

“Tumekutana katika kikao hiki cha pre-session kwa lengo la kuweka maandalizi yetu vizuri ili usikilizaji wa mashauri ufanyike kwa urahisi na kusiwe na mkwamo. Pia kupitia kikao hiki, niwaombe ushirikiano wadau wote wanaohusika ili kwa pamoja tufikie malengo kwa asilimia mia ya kikao chetu cha kusikiliza na kuamua mashauri,” alisema Jaji Dkt. Levira.

 

Naye Naibu Msajili Mwandamizi wa Mahakama ya Rufani (SDR) Mhe. Emmanuel Gasper Mrangu, kwa upande wake alieleza kuwa jumla ya mashauri 34 yamepangwa kusikilizwa na jopo la Majaji  hao wanne, wakiongozwa na Mwenyekiti ambaye pia ni Jaji Mkuu kuanzia tarehe 10 Machi, 2025 hadi 28 Machi,2025. 

 

Vilevile Mhe. Mrangu alifafanua kuwa kikao hicho ni cha pili kwa mwaka 2025 kufanyika Kanda ya Musoma pamoja na Kanda za Mahakama nyingine.

 

“Mahakama ya Rufani  Tanzania itaendesha kikao (session) hapa Musoma, ikiwa ni utekelezaji wa mpango maalumu wa kumaliza mashauri. Katika kikao hiki, jumla ya mashauri yaliyopangwa kusikilizwa ni thelathini na nne (34) ikiwa rufaa za Jinai ni 25, Rufaa za Madai moja na maombi ya Madai nane,” alisema Mhe. Mrangu.


Majaji wengine wa Mahakama ya Rufani Tanzania  wanaounda jopo hilo liliopiga kambi Musoma, ni Mhe. Dkt. Mary Caroline Levira, Mhe. Dkt.Benhajj Shaban Masoud na Mhe. Dkt. Deo John Nangela.  

 

Jaji Mkuu ya Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (mwenye tai nyekundu) akisalimiana na watumishi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Musoma na Mahakama ya Hakimu Mkazi Musoma. (Kulia kwake ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Musoma, Mhe. Fahamu H. Mtulya (mwenye tai nyeusi).

 

Jaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania, Mhe. Dkt. Mary Caroline Levira (katikati) akiongoza kikao cha awali cha usikilizaji wa mashauri (pre-session meeting) kilichofanyika hivi karibuni kilichohusisha wadau mbalimbali (hawapo pichani).

Naibu Msajili Mwandamizi wa Mahakama ya Rufani Tanzania, Mhe. Emmanuel Gasper Mrangu (aliyesimama) akitoa taarifa ya Msajili katika kikao cha awali cha usikilizaji wa mashauri (pre-session meeting).

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (katikati mstari wa mbele) akiwa  kwenye  picha ya pamoja na Wahe. Majaji wa Mahakama hiyo(walioko Kulia), na wakiwemo Majaji wa Kanda hiyo na viongozi wengine wa Mahakama.

Jaji Mkuu Mhe. Prof Ibrahim Hamis Juma(katikati mstari wa mbele) akiwa katika picha ya pamoja na Wahe.  Majaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania(kushoto) na  Wahe. Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania(ulia), viongozi wa Mahakama na  baadhi ya watumishi wa Kanda hiyo.


(Habari hii imehaririwa na MAGRETH  KINABO-Mahakama, Dodoma)

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni