Na Christopher Msagati- Mahakama, Manyara
Wadau
wa Mahakama Mkoa wa Manyara wamesisitizwa kuendelea kutoa ushirikiano wa karibu
kwa Mahakama ili kuboresha na kuisaidia Mahakama kumaliza mashauri kwa wakati
kumwezesha mwananchi kupata muda wa kutosha kuzalisha mali na kujenga uchumi
kwa ustawi wa Taifa.
Hayo
yamesemwa jana tarehe 28 Februari, 2025 na Kaimu Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu
Kanda ya Manyara Mhe. Devotha Kamuzora wakati wa kikao kilichofanyika katika
Ukumbi wa Wazi wa Mahakama Kuu Manyara.
Kikao
hicho kiliwashirikisha wadau mbalimbali wa Mahakama Mkoa wa Manyara wakimo Ofisi
ya Mashtaka, TAKUKURU, Ofisi ya Uhamiaji, Ofisi ya Magereza, Ofisi ya Kamanda
wa Polisi, Ofisi ya Ustawi wa Jamii, Madalali wa Mahakama, Ofisi ya Wakili wa
Serikali, Mwenyekiti wa Baraza la Ardhi na Nyumba wa Wilaya ya Babati, Mawakili
wa Kujitegema pamoja na Mahakimu waliopo Wilayani Babati.
Aidha,
kikao hicho kilichoandaliwa mahsusi kwa ajili ya kujadili mafanikio ya mwaka
2024 pamoja na kujiwekea malengo ya Mwaka 2025. Mhe. Kamuzora aliwasisitiza
wajumbe wa kikao kuhakikisha kuwa wanaendelea kutoa ushirikiano wa kutosha ili
kuisaidia Mahakama Kanda ya Manyara kumaliza mashauri mapema ili wananchi
wapate haki zao kwa wakati.
“Tumefanikiwa
kumaliza mwaka 2024 bila ya kuwa na mashauri ya Mlundikano, kwa hili inabidi
tuwashukuru sana wadau wetu kwa kuwa ushirikiano wenu kwetu ndiyo uliofanikisha
haya yote. Kila mmoja humu ndani amekuwa na mchango mkubwa katika suala zima la
kumaliza mashauri, tunaomba pia kwa mwaka huu 2025 muendelee hivyo hivyo na
tena kwa bidii zaidi ili tuweze kuwasaidia wananchi tunaowahudumia wapate haki
zao kwa wakati,” alisema Mhe. Kamuzora.
Katika
taarifa ya Uongozi wa Mahakama Kuu Kanda ya Manyara inayohusu mashauri iliyosomwa
na Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Manyara Mhe. Bernard Mpepo ilisisitiza
wadau kuendeleza kasi ya matumizi ya TEHAMA na mabadiliko yake yanayotokea mara
kwa mara mahakamani.
“Huduma
zetu kwa sasa zinapatikana kwa njia ya mtandao, kuanzia kufungua shauri,
kuliendesha na hadi kulitolea hukumu, wadau wetu tunawasihi muendelee kujifunza
na kuifahamu mifumo hii kwa sababu licha ya kupunguza gharama na matumizi ya karatasi,
pia mifumo hii inasaidia kufikisha huduma haraka na kwa uhakika zaidi kwa
wananchi,” ilinukuliwa sehemu ya taarifa hiyo.
Akichangia
mada katika kikao hicho, Mkuu wa Uhamiaji Mkoa wa Manyara Kamishna Msaidizi wa
Uhamiaji Philon P. Kyetema alisema kuwa, Ofisi yake itaendelea kushirikiana na
Mahakama katika mnyonyoro wa Utoaji Haki na itaendelea kujitahidi kutafuta
mbinu za kukabiliana na changamoto ya wafungwa ambao ni wahamiaji haramu
wanaokaa gerezani kwa muda mrefu na kusababisha changamoto ya kuwa na
mlundikano katika magereza.
“tunajua
kuwa wafungwa wengi wa makosa ya uhamiaji haramu wanakaa katika magereza yetu
kwa muda mrefu bila ya kurudishwa makwao. Hii yote inasababishwa na sababu za
kiuchumi na kibajeti. Tumeanza kubuni mbinu za kuwasiliana na ndugu zao pia ili
nao waweze kufanya taratibu za kuwarudisha makwao,” alisema Kamishna Msaidizi
Kyetema.
Akichangia
katika kikao hicho Mrakibu Mwandamizi wa Magereza Bw. Lisungu. M. Cosmo kwa
niaba ya Jeshi la Magereza wameipongeza Mahakama kwa juhudi wanazozifanya za
kuhakikisha kuwa Nakala za Hukumu na Mienendo ya mashauri zinatoka mapema na
mara nyingi siku hukumu inaposomwa.
“kwa
kuwa jitihada za Mahakama za kutoa nyaraka zimeonekana, sisi Jeshi la Magereza
tutaendelea kuendana na kesi hii ya TEHAMA ili tuweze kuhakikisha mahabusu na
wafungwa wanapata mawasiliano ya mara kwa mara, kuanzia usikilizwaji wa
mashauri na hata Rufaa zao,” alisema Mrakibu Mwandamizi wa Magereza Lisungu. M.
Cosmo.
Mahakama
Kuu Kanda ya Manyara imeweka utaratibu wa kukutana na wadau wake mara kwa mara
na kuweka mikakati mbalimbali ambayo yote ina lengo la kuongeza ushirikiano
miongoni mwa wadau lakini pia kukiwa na lengo la Kumaliza mapema mashauri yanayofunguliwa
Mahakamani ili kuendana na malengo ya Mahakama ambayo yamewekwa Kitaifa na
Kikanda.
Kaimu
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Kanda ya Manyara Mhe. Devotha Kamuzora
akizungumza katika kikao cha Mahakama na Wadau wa Mahakama kilichofanyika
katika Ukumbi wa Mahakama Kuu Manyara jana tarehe 28 Februari, 2025. Kulia ni Naibu Msajili wa Mahakama Kuu, Kanda ya Manyara
Mhe. Bernard Mpepo na kushoto ni Mtendaji wa Mahakama Kuu, Kanda ya Manyara Bi. Nyanzobe Hemedi.
Naibu
Msajili wa Mahakama Kuu, Kanda ya Manyara Mhe. Bernard Mpepo akitoa taarifa yake
katika kikao na wadau wa Mahakama Kuu Kanda ya Manyara.
Mrakibu
Mwandamizi wa Magereza Mkoa wa Manyara Lisungu M. Cosmo akichangia mada katika
kikao cha wadau wa Mahakama Kuu Kanda ya Manyara.
Sehemu ya wajumbe wakifuatilia mada zilizokuwa zikichangiwa katika kikao cha wadau wa
Mahakama Kuu Kanda ya Manyara.
Kamishna
Msaidizi wa Uhamiaji Philon P. Kyetema akichangia mada katika kikao cha wadau wa
Mahakama Kuu Kanda ya Manyara.
Hakimu
Mkazi wa Mahakama ya Mwanzo Magugu Mhe. Kuruthumu Mkundawantu akichangia mada
katika kikao cha wadau wa Mahakama Kuu Kanda ya Manyara.
(Habari Hii Imehaririwa na Innocent Kansha-Mahakama)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni