Jumatano, 12 Machi 2025

WATUMISHI, VIONGOZI WA MAHAKAMA KANDA YA MOROGORO WAIPAMBA SIKU YA WANAWAKE DUNIANI

Na ASHA JUMA-Mahakama, Morogoro

Katika kuazimisha Siku ya Wanawake Duniani ambayo hufanyika tarehe 8 Machi kila mwaka, Watumishi na Viongozi Wanawake wa Mahakama ya Tanzania katika Mkoa Morogoro wameungana na Watanzania wengine kusherekea maadhimisho hayo katika matukio ya aina mbalimbali.

Watumishi na Viongozi hao, kwa pamoja walikusanyika katika Halmashauri ya Mji wa  Ifakara iliyo katika Wilaya ya Kilombero kusherekea Siku hiyo iliyopambwa kwa Kauli Mbiu isemayo, “Wanawake na Wasichana 2025 Tuimarishe Haki, Usawa na Uwezeshaji.”

Maadhimisho hayo yaliongozwa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Morogoro, Mhe. Rose Ebrahim yaliambatana na sherehe mbalimbali ikiwemo utalii wa ndani wa kwenda kutembelea Hifadhi ya Taifa Milima Udzungwa.

Katika sherehe hiyo, washiriki pia walipata elimu jinsi ya utoaji haki na namna ya kuhakikisha kama kuna usawa katika jinsia zote mbili, namna ya kujua haki zao na kutoa ushirikiano pindi wanapoleta kesi zao mahakamani.

Akizungumza katika sherehe hiyo, Mhe. Ebrahim alieleza kuwa watu wanapaswa kujua haki zao pamoja na wajibu wao, hivyo jamii inapaswa kujua wajibu wao katika malezi ya Watoto wao ili kuepusha makosa kama ya unyanyasaji wa kijinsia na mimba za utotoni.

Akifungua maadhimisho, Mkuu wa Wilaya ya Kilombero katika Halmashauri ya Mji wa Ifakara, Mhe. Dunstan Kyobya aliwapongeza watumishi Wanawake kwa kushiriki katika hafla hiyo, kwani ni njia mojawapo ya kuwaunganisha watumishi pamoja.

Mkuu wa Wilaya pia alipata wasaa wa kubadilishana mawazo juu ya mambo mbalimbali yanayohusu haki, usawa na uwezeshaji wa Wanawake katika jamii inayomzunguka.

 

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Morogoro, Mhe. Rose Ebrahim akiwa jukwaa kuu katika kuadhimisha sherehe za Siku ya Wanawake duniani.

Watumishi wa Mahakama-juu na chini-walioshiriki katika sherehe za Siku ya Wanawake duniani.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Morogoro, Mhe. Rose Ebrahim akiwa na Watumishi wa Mahakama katika Hifadhi ya Taifa Milima Udzungwa, ikiwa ni mwendelezo wa kusheherekea Siku ya Wanawake duniani.

Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dodoma.

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni