Na EMMANUEL OGUDA, Mahakama-Shinyanga
Mradi wa Ujenzi wa jengo la Mahakama ya Wilaya Kishapu unatarajia kuanza rasmi mwezi huu Machi, 2025 baada ya Kampuni ya ‘Emirate Builders’ ya jijini Dar es Salaam kukabidhiwa rasmi eneo la ujenzi wa Mahakama hiyo jana tarehe 11 Machi, 2025.
Makabidhiano hayo yalishuhudiwa na Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Shinyanga, Mhe. Gadiel Mariki aliyeambatana na Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Shinyanga, Bw. Bakari Mketo kwa niaba ya Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Shinyanga.
Akizungumza wakati wa makabidhiano ya eneo hilo la ujenzi, Mhe. Mariki alimtaka Mkandarasi kuhakikisha anatekeleza Mradi huo kwa viwango vilivyokubalika na kwa muda sahihi kulingana na Mkataba wa mradi huo.
“Nimtake Mkandarasi kuhakikisha anakamilisha mradi ndani ya muda uliopangwa na kwa viwango vya hali ya juu ili Mahakama yetu ya Wilaya Kishapu ianze kufanya kazi kama ilivyokusudiwa,’’ alisema Naibu Msajili.
Naye, Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Shinyanga, Bw. Bakari Mketo ameahidi ushirikiano kwa Mkandarasi wakati wote wa utekelezaji wa mradi huo ili utekelezaji wake usiwe na changamoto zinazoweza kutatuliwa na uongozi wa Kanda hiyo.
Awali akizungumza katika kikao cha makabidhiano ya Mradi huo, Mtalaamu Mshauri kutoka Kampuni ya MD Consultancy LTD, Mhandisi Evelyn Shirima alisema kuwa, mradi huo utatekelezwa ndani ya kipindi cha miezi nane (8) toka tarehe ya kuanza rasmi kwa ujenzi huo tarehe 26 Machi, 2025 na utagharimu fedha za Kitanzania Shilingi Bilioni 1.5 ikiwa ni fedha za ndani.
Makabidhiano hayo yalishuhudiwa pia na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Kishapu, Mhe. Johanitha Rwehabura ambaye alionesha furaha yake baada ya kuwapokea Wakandarasi wa Mradi huo walioongozwa na Wawakilishi kutoka Idara ya Ujenzi Makao Makuu ambao ni Mhandisi Andrew Weja na Mkadiriaji Majenzi QS Wolfram Mrimi.
Mahakama ya Wilaya ya Kishapu hivi sasa inaendesha shughuli zake katika jengo la Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu tangu mwaka 2015 baada ya kuanzishwa rasmi ambapo awali Mahakama hiyo ilikuwa ikiendesha shughuli za kimahakama katika jengo la Mahakama ya Wilaya Shinyanga.
Ujenzi wa Mahakama hiyo, unatekelezwa ikiwa ni jitihada za Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kushirikiana na Mahakama ya Tanzania katika kuboresha huduma za utoaji haki kwa wananchi wa Wilaya ya Kishapu.
Mkadiriaji Majenzi 'QS' Wolfram Mrimi kutoka Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania (aliyevaa vesti ya njano) akionesha ramani ya ujenzi wa Mahakama ya Wilaya ya Kishapu wakati wa makabidhiano ya eneo la mradi (site) kwa Mkandarasi 'Emirate Builders' tarehe 11 Machi, 2025.
Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Shinyanga, Mhe. Gadiel Mariki akisisitiza jambo wakati wa makabidhiano ya eneo la ujenzi wa Mahakama ya Wilaya Kishapu.
Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Shinyanga, Bw. Bakari Mketo akisisitiza jambo wakati wa makabidhiano ya eneo la ujenzi wa Mahakama ya Wilaya Kishapu tarehe 11 Machi, 2025.
Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Kishapu, Mhe Johanitha Rwehabura akifuatilia kwa makini maelezo ya Mradi wa Ujenzi wa Mahakama ya Wilaya Kishapu.
Mhandisi Evelyn Shirima kutoka MD Consultancy akisisitiza jambo wakati wa makabidhiano ya eneo la ujenzi wa Mahakama ya Wilaya Kishapu jana tarehe 11 Machi, 2025.
Mhandisi Evelyn Shirima (kulia) kutoka MD Consultancy akikabidhi ramani ya ujenzi wa Mahakama ya Wilaya Kishapu kwa Mwakilishi wa Kampuni ya Ujenzi ya 'Emirate Builders' ya jijini Dar es Salaam.
Timu ya Wakandarasi 'Emirate Builders' wakiwa katika picha ya pamoja wakati wa makabidhiano ya eneo la Mradi wa Ujenzi wa Mahakama ya Wilaya Kishapu.
Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Shinyanga, Mhe. Gadiel Mariki katika picha ya pamoja na timu ya Wakandarasi kutoka 'Emirate Builders', Wataalam Washauri kutoka MD Consultancy pamoja na watumishi wa Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania na Mahakama Kanda ya Shinyanga.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni