Jumatano, 12 Machi 2025

MAHAKAMA YA RUFANI YAWEKA KAMBI IRINGA

  • Jumla ya mashauri ya mlundikano 26 kushughulikiwa
  • Wadau watakiwa kutoa ushirikiano

Na LUSAKO MWANG’ONDA, Mahakama-Iringa

Jumla ya mashauri ya mlundikano 26 yanatarajiwa kusikilizwa katika  kikao cha Mahakama ya Rufani ya Tanzania kinachofanyika Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Iringa.

Akizungumza tarehe 10 Machi, 2025 katika kikao maalum cha kuwajulisha wadau kuhusu vikao vya Mahakama hiyo vilivyopangwa kusikiliza mashauri Mahakama Kuu Kanda ya Iringa vilivyoanza kuanzia tarehe 10 hadi 28 Machi, 2025, Jaji wa Mahakama ya Rufani na Mwenyekiti wa Jopo la Majaji wa Mahakama ya Rufani wanaosikiliza mashauri hayo, Mhe. Rehema Kerefu alitoa rai kwa wadau wote kutoa ushirikiano wa kutosha katika kipindi chote cha uendeshaji wa vikao hivyo.

“Lengo la kikao hiki ni kufanikisha usikilizwaji wa mashauri yaliyopo mbele yetu ya Rufani na kutoa haki kwa wadaawa kwa wakati ili kupunguza mlundikano wa wafungwa na kuondoa malalamiko ya wadau hivyo ni muhimu kushirikiana wakati wa usikilizaji wa mashauri hayo,” alisema Mhe. Kerefu.

Mhe. Kerefu aliwasisitiza Jeshi la Magereza kuwafikisha wafungwa mapema mahakamani na kwa wengine walio mbali kufika kwa wakati.

Aidha, Mhe. Kerefu aliwakumbusha Mawakili wa Serikali na wa Kujitegemea kusoma vizuri nyaraka za kumbukumbu za mashauri hayo na wakati huo huo kuwasaidia wateja wao wakiwa mahakamani ili kuisaidia Mahakama kuendesha mashauri hayo kwa ufanisi na kutoa uamuzi stahiki na wa haki kwa wadaawa.

Vilevile, Mhe. Kerefu aliwashauri Mawakili wote walioshiriki kikao hicho kujenga utamaduni wa kwenda mahakamani mara kwa mara kusikiliza na kujifunza namna uendeshaji wa mashauri ya aina hiyo ili kuzijua taratibu za uendeshaji wa mashauri na kuijua Mahakama zaidi kwani kwa kufanya hivyo kutawajengea uwezo na kuongeza weledi wao kitaaluma.

Akitoa taarifa ya kikao hicho, Naibu Msajili wa Mahakama ya Raufni Tanzania, Mhe. Joseph Fovo alisema, “kikao hiki kinajumuisha jumla ya mashauri 26 kati ya mashauri hayo ya jinai ni 15, mashauri ya madai yakiwa tisa na hivyo kufanya jumla ya mashauri 26.”

Naye, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Iringa Mhe. Dustan Beda Ndunguru, aliwashukuru Majaji wa Mahakama ya Rufani kwa ujio wao na kuwahakikishia kwamba maandalizi yote ya vikao hivyo yamekamilika na kuahidi kuendelea kutoa ushirikiano wakati wote wa uendeshaji wa vikao hivyo pale utakapohitajika.

Kikao hicho maalum kilichoongozwa na Jaji wa Mahakama ya Rufani ya Tanzania, Mhe. Rehema Kerefu ambaye pia ni Mwenyekiti wa Jopo la Majaji watatu wa Mahakama ya Rufani wanaosikiliza mashauri hayo, Majaji wengine wakiwa ni Mhe. Leila Edith Mgonya na Mhe. Lameck Mlacha.


Jopo la Majaji wa Mahakama ya Rufani wakiwa katika picha ya pamoja wakati wa kikao hicho. Katikati ni Mhe. Rehema Kerefu ambaye ni Mwenyekiti wa Jopo, kulia ni Mhe. Leila Edith Mgonya na kushoto ni Mhe. Lameck Mlacha.

Jaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania na Mwenyekiti wa Jopo wa Jopo la Majaji watatu wanaosikiliza mashauri Kanda ya Iringa, Mhe. Rehema Kerefu  akizungumza wakati wa kikao hicho kilichofanyika tarehe 10 Machi, 2025.

Jaji wa Mahakama ya Rufani ya Tanzania Mhe. L. E. Mgonja akiwa katika kikao hicho kilichofanyika tarehe 10 Machi, 2025. 

Jaji wa Mahakama ya Rufani ya Tanzania, Mhe. Lameck Mlacha akiwa katika kikao hicho.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Iringa, Mhe. Dustan Beda Ndunguru akiwa katika kikao hicho.

Naibu Msajili wa Mahakama ya Rufani Tanzania, Mhe. Joseph Fovo akizungumza wakati wa kikao hicho.

Wajumbe walioshiriki kikao hicho wakifuatilia kwa makini yaliyokuwa yakiendelea katika kikao hicho.

(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma)



Hakuna maoni:

Chapisha Maoni