- Lengo ni kurahisisha utendaji kazi na utoaji haki kwa wakati
- Jaji Mfawidhi asisitiza matumizi ya TEHAMA kuwa ni ya lazima
Na LUSAKO MWANG’ONDA, Mahakama-Iringa
Jumla ya Mahakimu wapya sita waliopangwa katika Mahakama za Mwanzo zilizopo mkoani Iringa wamekabidhiwa Kompyuta Mpakato (laptop) kwa ajili ya kusaidia utendaji kazi wao.
Makabidhiano hayo yalifanyika tarehe 10 Machi, 2025 katika ukumbi wa Mahakama Kuu Kanda ya Iringa ambapo Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Iringa Mhe. Dustan Ndunguru ndiye aliyeongoza zoezi hilo.
Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo, Mhe. Ndunguru aliwakumbusha Mahakimu hao kuwa, matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) mahakamani kwa sasa yamekuwa ni ya lazima, hivyo wanapaswa kuitumia vema wanapotekeleza majukumu yao.
“Kwa sasa Mahakama mtandao imeshika kasi tofauti na zamani wakati sisi ndio tunaingia humu, nyie mmekuja kipindi ambacho kila kitu kipo kwenye TEHAMA, hivyo ni wajibu wetu sote kuitumia TEHAMA ipasavyo,” alisema Jaji Ndunguru.
Aidha, Jaji Mfawidhi huyo alieleza kuwa, anaamini kuna wakati unakuja ambapo hata Mahakama za Mwanzo watafanya kila kitu katika mtandao kama ambavyo Mahakama za Wilaya na nyingine zinavyofanya, hivyo Mahakimu hao wanatakiwa kujizoesha kuishi kwenye ulimwengu wa sasa.
Kadhalika, Mhe. Ndunguru alitumia fursa hiyo kuwahimiza Mahakimu hao kuzingatia ubora wa maamuzi yao na kuhakikisha wanafanya rejea ya sheria ili waweze kutoa hukumu zilizo bora na kuongeza kwamba anaamini kuwa watatumia kompyuta hizo katika kufanya tafiti mbalimbali za kisheria.
Akizungmza kwa niaba ya Mahakimu wenzake waliokabidhiwa kompyuta hizo, Mhe. Emmy Mwamgiga alitoa shukrani kwa uongozi wa Mahakama kwa kuzingatia haja ya kuboresha mazingira ya kazi, na kueleza kuwa, vifaa hivyo vitawawezesha kufanya kazi zao kwa haraka zaidi na kuwezesha haki kutolewa kwa wakati.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Iringa, Mhe. Dustan Beda Ndunguru (kushoto) akikabidhi kompyuta mpakato kwa Mhe. Hekima Nyalusi ambaye ni Hakimu wa Mahakama ya Mwanzo Iringa Mjini. Katikati ni Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Iringa, Bi. Melea Richard Mkongwa. Zoezi ya makabidhiano ya kompyuta hizo lilifanyika tarehe 10 Machi, 2025.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Iringa, Mhe. Dustan Beda Ndunguru akikabidhi kompyuta kwa Mhe. Nives Mahui ambaye ni Hakimu wa Mahakama ya Mwanzo Iringa Mjini. Katikati ni Mtendaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Iringa, Bi. Melea Richard Mkongwa.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Iringa, Mhe. Dustan Beda Ndunguru akikabidhi kompyuta kwa Mhe. Emmy Mwangiga ambaye kwa sasa ni Hakimu wa Mahakama ya Mwanzo ya Iringa Mjini. Katikati ni Mtendaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Iringa, Bi. Melea Richard Mkongwa.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Iringa, Mhe. Dustan Beda Ndunguru akikabidhi kompyuta kwa Mhe. Deograsias Kibasa ambaye kwa sasa ni Hakimu wa Mahakama ya Mwanzo ya Bomani. Katikati ni Mtendaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Iringa, Bi. Melea Richard Mkongwa.








Hakuna maoni:
Chapisha Maoni