Na ARAPHA RUSHEKE na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dodoma
Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan leo tarehe 26 Aprili, 2025
amemtunuku Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma, Nishani ya Kumbukumbu
ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar Daraja la Pili.
Hafla ya kutunuku nishani
hizo imefanyika katika Ikulu ya Chamwino jijini hapa na kuhudhuriwa na Viongozi
mbalimbali wa kitaifa wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali
ya Mapinduzi Zanzibar.
Walikuwepo pia Viongozi Wakuu
wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Baraza la Wawakilishi Zanzibar na
Mahakama ya Tanzania na Mahkama ya Zanzibar, Majaji wa Mahakama ya Rufani, Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania na Majaji wengine pamoja na Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania.
Akimtunuku nishani hiyo
Jaji Mkuu, Rais Samia amesema, ‘Kwa kutambua mchango wako katika Taifa la Tanzania
na utumishi wako, mimi Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania nakutunuku Nishani ya Kumbukumbu ya Muungano Daraja la Pili.’
Viongozi wengine
waliotunukiwa nishani kwenye hafla hiyo ni Makamu wa Rais Mstaafu wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Ali Mohamed Shein na Makamu wa Pili wa Rais wa
Zanzibar, Mhe. Balozi Seif Ali Iddi.
Wengine ni Waziri Mkuu Mstaafu
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Hayati Edward Ngoyai Lowassa, Waziri Mkuu Mstaafu
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Mizengo Kayanza Peter Pinda na Spika Mstaafu
wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar, Mhe. Pandu Ameir Kificho.
Viongozi wengine waliotunukiwa
nishani hizo ni Katibu Mkuu Kiongozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Hayati
Balozi John William Kijazi na Makamu wa Mwenyekiti Mstaafu wa Chama cha
Mapinduzi, Mhe. Phillip Mangura, ambaye alitunukiwa Nishani ya Kumbukumbu ya
Muungano Daraja la Tatu.
Wasifu wa Mhe. Prof. Juma
uliosomwa kwenye hafla hiyo unaonesha kuwa amepata elimu ya Msingi, Sekondani na
Vyuo Vikuu katika Nchi mbalimbali, ikiwemo Tanzania, Uingereza, Sweeden na Uberigiji.
Amekuwa Mwanachama wa
Chama cha Mawakili Tanganyika, Wakili wa Serikali, Kaimu Mkurugenzi wa Kituo
cha Sheria na Haki za Binadamu na Mjumbe wa Kamati mbalimbali, ikiwemo
iliyochunguza mauaji ya Wafanyabiasha wa Madini Mahenge, Morogoro-maarufu Tume
ya Jaji Kipenka, Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania na Tume ya Utumishi wa Mahakama.
Kadhalika, Mhe. Prof.
Juma amekuwa Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Jaji wa Mahakama ya Rufani
Tanzania, Kaimu Jaji Mkuu na baadaye kuwa Jaji Mkuu wa Tanzania, nafasi
anayoihudumu hadi sasa.
Mhe. Prof. Juma ameandika
vitabu 18 vyenye maudhuri tofauti ya kisheria, amekuwa Mhadhiri katika Chuo Kikuu
cha Dar es Salaam, Kitivo cha Sheria kwa miaka mingi na kwa nyakati tofauti amewahi
kufanya kazi za ushauri elekezi-consultancy- kwenye maeneo tofauti nane chini
ya Wizara mbalimbali.
Utoaji wa nishani hizo kwa Viongozi mbalimbali ni sehemu ya Maadhimisho ya Miaka 61 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar uliozaa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Picha na Arapha Rusheke-Mahakama, Dodoma
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni