Jumamosi, 26 Aprili 2025

‘UCHUNGUZI WA MAKOSA YA KIFEDHA NGUZO MUHIMU KATIKA MAPAMBANO YA UHALIFU KIUCHUMI’

Na ASHA JUMA – Mahakama Morogoro

Jaji Mfawidhi wa Mahamaka Kuu ya Tanzania, Kanda ya Morogoro, Mhe. Rose Ebrahim amesema uchunguzi wa makosa ya kifedha ni nguzo muhimu katika mapambano dhidi ya uhalifu wa kiuchumi.

Mhe. Ebrahim ameyasema hayo wakati akifungua mafunzo kwa Wadau wa Haki Jinai kuhusiana na Uchunguzi wa Makosa ya Kifedha na Uchunguzi wa Kisayansi yaliyofanyika kwa siku mbili kuanzia tarehe 25 Aprili, 2025 mkoani hapa.

Alibainisha kuwa Wahalifu wengi wa makosa hayo wamekuwa wakiibua mbinu mbalimbali za kidigitali ikiwemo kuunda mitandao tata isiyofikika kirahisi na kwa mbinu za kawaida.

“Kwenye makosa ya kifedha, wahalifu wengi huwa wanatumia mbinu za kiteknolojia kutenda au kuwezesha utendaji wa makosa hayo, hivyo Wapelelezi na Waendesha Mashtaka lazima wawe na ujuzi wa kutosha kufaa kukusanya ushahidi wa kielektoniki na kufuata sheria zilizowekwa ili kusimama vyema bila kupoteza Ushahidi,”. alisisitiza.

Jaji Mfawidhi alisema ni muhimu  mafunzo hayo kufanyika kwa kila mamlaka ili kuweka utaratibu wa kuwa endelevu na kubaini mbinu zinavyobadilika kila kukicha, kwani itasaidia kupata nafasi ya kubadilishana uzoefu kwa mambo au mbinu na changamoto ambazo wengine wanakutana nazo na namna bora ya kukabiliana nazo.

Mhe. Ebrahim alisisitiza juu ya umuhimu mkubwa wa ushahidi wa kisayansi katika utendaji wa haki ambapo sayansi na teknolojia vimeshika atamu.

“Ni lazima tuwe na maarifa na mbinu za kutosha za kiupelelezi na ukusanyaji ushahidi unaojibu makosa ya kifedha ili kuisaidia Mahakama kutoa maamuzi yaliyosahihi kwa upande wa mashtaka na kuweza kutaifisha mali zinazotokana na makosa husika,’’ alifafanua.

Sambamba na hilo amewahimiza Waendesha Mashtaka na Wapelelezi kufanya kazi kwa ushirikiano ili kuwawezesha kupata ushahidi wa uhakika na uliokamilika.

Alisema mashitaka bila ufuatiliaji wa mali ni ushahidi nusu, ambao bado haujakamilika. Uhalifu wa kifedha sio tu kuwafikisha wahusika mahakamani bali ni kuhusu urejeshaji wa mali, uwajibikaji na kutoa fundisho kwa wengine.

‘Mali yoyote au fedha inayoporwa kutoka kwa umma au Wananchi inapaswa kurejeshwa na kila mhalifu hanabudi kuadhibiwa pamoja na kupokonywa faida ya uhalifu huo,’ Jaji Mfawidhi alisema.

Alieleza kuwa mafunzo hayo yakawe chachu kwao katika kupambana na uhalifu huo wa kifedha na kutumia ushahidi wa kisayansi ili kuhakikisha kuwa hakuna mtu yeyote atakayethubutu kuchezea mali za Taifa, kuzipora au kuzihujumu na kuachwa akafaidika kwa namna yoyote ile.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mashtaka Mkoa wa Morogoro, Bi. Tarsila Gervas alieleza lengo la mafunzo hayo ni kuwaongezea uwezo Wapelelezi na Waendesha Mashtaka katika masuala ya makosa ya kifedha pamoja na makosa mengine yanayohusisha ushahidi wa kisayansi.

Alisema pia kuwa mafunzo hayo ni dhamira ya dhati kwa Mkoa wa Morogoro katika kuhakikisha wanafanya upelelezi na uendeshaji wa mashtaka ambao unakuwa na ufanisi mkubwa na unaolenga kukomesha uhalifu katika mkoa huo.

"Tunataka kuujenga Mkoa salama ambapo Wananchi wake wanaweza kufanya shughuli zao za kiuchumi na kijamii kwa amani pasipo kusumbuliwa wala kuwa uwoga wa vitendo vya kiuhalifu," alifafanua.

Mafunzo hayo yalihusisha Taasisi mbalimbali zinazounda mnyororo wa haki jinai zikiwepo Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, TAKUKURU, TAWA, TANAPA, TFS, Jeshi la Polisi, na Uhamiaji.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Morogoro, Mhe. Rose Ebrahim akitoa hotuba yake wakati wa ufunguzi wa mafunzo kwa Wadau wa Haki Jinai.


 
Mkuu wa Mashtaka Mkoa wa Morogoro, Bi. Tarsila Gervas akiwasilisha mada wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo. 

Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Morogoro, Mhe. Susan Kihawa-wa kwanza kushoto na baadhi ya Viongozi wakifuatilia ufunguzi wa mafunzo hayo.

Wadau wa Haki Jinai wakifuatilia ufunguzi wa mafunzo.


Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dodoma

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni