Jumatano, 9 Aprili 2025

WATUMISHI WASTAAFU MASJALA KUU WAAGWA

Na ARAPHA RUSHEKE-Mahakama Kuu, Dodoma

Watumishi watatu wa Mahakama ya Tanzania, Masjala Kuu Dodoma, ambao wamestaafu kazi kwa mujibu wa sheria, wameagwa rasmi.

Hafla ya kuwaaga Watumishi wao ilifanyika jana tarehe 8 Aprili, 2025 katika ukumbi uliopo Rafiki Hoteli jijini Dodoma na kuhudhuriwa na Viongozi pamoja na Watumishi wakiongozwa na Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu Tanzania, Mhe. Dkt. Mustapher Mohamed Siyani.

Katika hafla hiyo, Watumishi hao walipatiwa zawadi mbalimbali ikiwa ni ishara ya kuenzi mchango wao katika kuitumikia Mahakama ya Tanzania kwa uadilifu na uchapakazi uliotukuka.

Wastaafu hao ni Bi. Scholastica Njiwa ambaye ni Mwandishi Mwendesha Ofisi, Bw. Hemed Hemed na Bw. Issa Rajab Kabandika.  

Watumishi hao walipata fursa ya kushiriki katika shughuli mbalimbali ikiwemo tukio la kukata keki pamoja na burudani, hali iliyoleta furaha na kumbukumbu nzuri, huku wakikumbushana mambo ya zamani waliyokutana nayo pamoja na chamngamoto katika utumishi wao.

Walitumia hao pia walipata nafasi ya kueleza jinsi walivyoweza kuvuka vikwazo na kufanya kazi kwa ushirikiano ili kufanikisha malengo ya Mahakama na kuwasihi wanaobaki waendelee kufanya kazi kwa bidii pamoja na kujituma.

Akitoa neno la shukrani kwa niaba ya wenzake, Bi. Scholastika Njiwa aliwashukuru Viongozi na Watumishi kwa kuwafanyia sherehe pamoja na kuwapatia zawadi.

 

Watumishi wastaafu wa Masjala Kuu wakiwa katika picha ya pamoja wakati wa hafla hiyo iliyofanyika Rafiki Hoteli jijini Dodoma.

Picha ya Keki iliyokuwa imeandaliwa katika sherehe hiyo.

Sehemu ya Watumishi wa Masjala Kuu waliohudhuria hafla hiyo.

Bi. Scholastica Njiwa, mmoja ya Watumishi Wastaafu akitoa neno la shukrani kwa niaba ya wenzake.

Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Mustapher Mohamed Siyani (wapili kutoka kulia) akiwa katika picha ya pamoja na Watumishi waliostaafu wakati wa hafla ya kuwaaga.

Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Morogoro.

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni