· Asisitiza usimamiaji thabiti wa sheria na kuwachukulia hatua kali wahusika wa Vitendo vya Unyanyasaji wa kijinsi
· Akemea pia matumizi mabaya ya madaraka kwa viongozi wanaume yanayoambatana na rushwa ya ngono
Na MARY GWERA, Mahakama-Cape Town
Rais wa Jamhuri ya Afrika Kusini, Mhe. Matamela Cyril Ramaphosa amesema mapambano dhidi ya vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia na mauaji ya wanawake si jukumu la viongozi wanawake pekee bali pia wanaume wanatakiwa kushiriki kikamilifu kutokomeza vitendo hivyo.
Mhe. Ramaphosa ameyasema hayo leo tarehe 09 Aprili, 2025 wakati akifungua
Mkutano wa 17 wa Chama cha Majaji Wanawake Duniani (IAWJ) unaofanyika katika Kituo
cha Kimataifa cha Mikutano cha Cape Town (CTICC) nchini Afrika Kusini.
“Nimefurahishwa na kaulimbiu ya Mkutano huu wa Majaji Wanawake Duniani
isemayo ‘Wanawake na uongozi katika kushughulikia unyanyasaji wa kijinsia na mauaji
dhidi ya wanawake’ ila naomba niongezee kuwa mapambano haya hayatakiwi kuhusisha
wanawake pekee bali pia yanatakiwa kuhusisha wanaume,” amesema Rais Ramaphosa.
Aidha, Mhe. Ramaphosa amesema kuwa, katika kupambana na vitendo vya unyanyasaji
wa kijinsia na mauaji dhidi ya wanawake ni muhimu Sheria zilizowekwa katika
nchi husika zitekelezwe inavyopaswa sambamba na kuwachukulia sheria kali
wanaobainika kuhusika na vitendo hivyo.
“Katika suala la ushughulikiaji wa watuhumiwa wa vitendo vya unyanyasaji
wa kijinsia na mauaji dhidi ya wanawake ni muhimu sheria ichukue mkondo wake
inavyotakiwa lakini pia haki ionekane kutendeka inavyostahiki,” amesisitiza
Rais Ramaphosa.
Aidha, katika hotuba yake, Mhe. Ramaphosa ametoa rai pia kwa viongozi na
Maafisa wanaume wenye vyeo mbalimbali kutojihusisha na matumizi mabaya ya
madaraka yanayoambatana na rushwa ya ngono hususani wanayofanya hasa kwa wanawake
wenye uhitaji wa kazi.
Amesisitiza pia, wanawake kutoa taarifa kwenye mamlaka husika pindi wanapokumbana na vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia, na kuwakumbusha wawe na udhibiti wa maisha
yao na uhuru wa kiuchumi ili kupungua kutokea kwa vitendo hivyo.
Kwa upande mwingine, Rais Ramaphosa amezungumzia kuhusu usawa wa kijinsia nchini Afrika Kusini, ambapo amesema kuwa, mpaka sasa Nchi hiyo yenye Jaji Mkuu mwanamke na Waziri wa Katiba na Sheria mwanamke ina asilimia 48 ya Majaji wanawake na kueleza kuwa, wamepiga hatua kubwa ikilinganishwa na hali ilivyokuwa awali.
Kwa upande wake Rais wa Chama cha Majaji Wanawake Duniani (IAWJ), Mhe. Binta
Nyako amesema nafasi ya Viongozi wanawake katika sekta ya sheria ni muhimu
katika mapambano dhidi ya vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia sambamba na
mauaji ya wanawake.
“Jamii inahitaji mazingira wezeshi na tulivu, hivyo ni jukumu letu Majaji
na Mahakimu kutoishia tu kwenye vyumba vya Mahakama bali kazi yetu inatakiwa kuwafuata
na kuwaelimisha kuhusu vitendo hivyo,” amesema Mhe. Nyako.
Wanachama wa Chama cha Majaji na Mahakimu Wanawake Tanzania (TAWJA) ni miongoni mwa jumla ya washiriki 903 wanaohudhuria katika mkutano huo wa siku nne.
Mada
mbalimbali zitatolewa lengo likiwa ni kujadili na kuja na maazimio ya pamoja ya namna bora
ya kusimama katika kudhibiti na kukomesha vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia
na mauaji ya wanawake.
Rais wa Jamhuri ya Afrika Kusini, Mhe. Matamela Cyril Ramaphosa akitoa hotuba ya ufunguzi wa Mkutano wa 17 wa Chama cha Majaji Wanawake Duniani (IAWJ) unaofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Cape Town (CTICC) nchini Afrika Kusini.
Vikundi vya burudani vikitoa burudani wakati wa ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa Chama cha Majaji Wanawake Duniani (IAWJ) leo tarehe 09 Aprili, 2025.
Mwenyekiti wa Chama cha Majaji na Mahakimu Wanawake Tanzania (TAWJA), Mhe. Barke Sehel (kulia) akifanya mahojiano na Mwandishi kutoka Shirika la Utangazi la Afrika Kusini (SABC) waliokuwa wakirusha matangazo mubashara ya hafla ya ufunguzi wa Mkutano wa 17 wa Chama cha Majaji Wanawake Duniani leo tarehe 09 Aprili, 2025.
Washiriki wakifuatilia hafla ya ufunguzi wa Mkutano wa Chama cha Majaji Wanawake Duniani (IAWJ) leo tarehe 09 Aprili, 2025.
Rais wa Chama cha Majaji Wanawake Duniani (IAWJ), Mhe. Binta Nyako akizungumza wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa 17 wa Chama cha Majaji Wanawake Duniani (IAWJ) leo tarehe 09 Aprili, 2025 Cape Town nchini Afrika Kusini.
Rais wa Jamhuri ya Afrika Kusini, Mhe. Matamela Cyril Ramaphosa (wa saba kushoto) akiwa katika picha ya pamoja na Washiriki wa Mkutano Mkuu wa 17 wa Chama cha Majaji Wanawake Duniani (IAWJ).
Wanachama wa TAWJA wakiwa katika picha ya pamoja mara baada ya hafla ya ufunguzi wa Mkutano wa 17 wa Chama cha Majaji Wanawake Duniani (IAWJ) leo tarehe 09 Aprili, 2025.
(Picha na MARY GWERA, Mahakama-Cape Town)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni