Na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dodoma
Jaji Mkuu wa Tanzania,
Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma amewakumbusha Watumishi wa Mahakama katazo la
kisheria linalowazuia kujihusisha na masuala ya siasa.
Mhe. Prof. Juma ametoa
angalizo hilo leo tarehe 10 Aprili, 2025 alipokuwa anafungua Kikao cha siku
mbili cha Baraza la Wafanyakazi Taifa kinachofanyika katika Ukumbi wa PSSF jijini
Dodoma.
‘Tukumbushane,
ukijitokeza kuwania nafasi ya kugombea ngazi yoyote katika uchaguzi ujao na
ukakosa, hutarudi katika utumishi wa Mahakama. Tulifanya hivyo katika uchaguzi
Mkuu uliopita,’ Jaji Mkuu ameonya.
Mhe. Prof. Juma amebainisha kuwa katazo la
ushiriki katika shughuli za kisiasa kwa Jaji wa Mahakama ya Rufani, Jaji wa
Mahakama Kuu, Hakimu wa ngazi yoyote; zimefafanuliwa kwa kina na Kanuni za
Maadili ambazo amewaomba wazisome tena na tena.
Amewakumbusha pia
maelekezo ya Ibara ya 113A kuhusu uanachama katika vyama vya siasa, ambayo yanasema,
“Itakuwa ni marufuku kwa Jaji wa Mahakama ya Rufani, Jaji wa Mahakama Kuu,
Hakimu wa ngazi yoyote kujiunga na chama chochote cha siasa, isipokuwa tu
kwamba atakuwa na haki ya kupiga kura iliyotajwa katika Ibara ya 5 ya Katiba
hii.”
Jaji Mkuu amefafanua kuwa
ingawa Kanuni za kimaadili kupiga marufuku ushiriki katika siasa zimejielekeza
kwa Majaji, Wasajili, Mahakimu na Wasaidizi wa Majaji, Watumishi wezeshi wa
Mahakama wamebeba taswira na sura ya Mahakama kutoshiriki katika siasa.
‘Tunapaswa kujiepusha na
siasa kwani kufanya hivyo tukiwa Watumishi inapelekea Wadau na Wananchi
kupoteza imani na Mahakama yao kwa kuamini kuwa haki haiwezi kutendeka kwa
sababu Mahakama inayo itikadi ya chama fulani…
‘…Nafahamu kuwa zipo jitihada kubwa katika
mitandao ya kijamii kujaribu kutuhusisha na siasa, lakini kipimo na nafasi yako
na namna unavyojitokeza, unavyoongea na unavyotoa huduma,’ Mhe. Prof. Juma amesema.
Jaji Mkuu amewataka Watumishi
wote kujizuia kuonesha hisia zao kwa vyama wanavyovipenda au wagombea wanaowapenda
na kwamba lazima wajipange mapema kuwahudumia wateja watakaofika mahakamani
kuhusiana na masuala yanayohusu uchaguzi.
‘Ni vema tukaanza
kujipanga mapema kuzifahamu sheria na kanuni za uchaguzi wa 2025 ili tuweze
kutekeleza kazi zetu kwa ufanisi na ueledi mkubwa. Tukijipanga mapema
tutajiepusha kuwa sehemu ya walalamikiwa katika masuala ya uchaguzi na badala
yake tutabaki kuwa chombo kinachoaminiwa cha kutoa maamuzi katika mashauri ya
uchaguzi endapo yatakuwepo,’ amesema.
Mhe. Prof. Juma ametumia
fursa hiyo kuhimiza Majaji na Mahakimu kusikiliza na kuamua kwa haraka na katika
misingi ya haki mashauri yatokanayo na taratibu mbalimbali za uchaguzi.
Amekumbushia kuwa katika
uchaguzi Mkuu ujao, Majaji, Wasajili, Mahakimu na Watumishi wa Mahakama ni
sehemu muhimu ya utatuzi wa migogoro ya uchaguzi.
Jaji Mkuu amebainisha pia
kuwa kama raia, Watumishi wa Mahakama wanayo haki ya kikatiba kuwachagua Viongozi.
Hivyo ametoa rai kwa Watumishi wa Mahakama kutumia haki hiyo ambayo wamepewa na
Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Katibu wa Baraza hilo, Bw. Hezra Kyando akitoa utambulizho wa Wajumbe wa Baraza ambao wamehudhuria kikao hicho.
Jaji wa Mahakama ya Rufani na Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto, Mhe. Dkt. Paul Kihwelo akifuatilia yaliyokuwa yanajiri wakati wa Kikao hicho.
Sehemu nyingine ya tatu ya Wajumbe wa Baraza-juu na chini- wakifuatilia kinachojiri kwenye Kikao hicho.
Sehemu nyingine ya nne ya Wajumbe wa Baraza-juu na chini- wakifuatilia kinachojiri kwenye Kikao hicho.
Sehemu nyingine ya tano ya Wajumbe wa Baraza-juu na chini- wakifuatilia kinachojiri kwenye Kikao hicho.
Sehemu nyingine ya sita ya Wajumbe wa Baraza-juu na chini- wakifuatilia kinachojiri kwenye Kikao hicho.
Sehemu nyingine ya saba ya Wajumbe wa Baraza-juu na chini- wakifuatilia kinachojiri kwenye Kikao hicho.
Sehemu nyingine ya nane ya Wajumbe wa Baraza-juu na chini- wakifuatilia kinachojiri kwenye Kikao hicho.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni