Alhamisi, 10 Aprili 2025

HASSAN RAMADHANI SAID AIBUKA MSHINDI; UTUMISHI HODARI MAHAKAMA KANDA YA IRINGA

  • Ni Msaidizi wa Ofisi Mahakama ya Wilaya Wanging'ombe

Na ABDALLAH SALUM, Mahakama-Njombe

Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Iringa imemchagua mtumishi bora wa Kanda hiyo kuwa ni Bw.Hassan Ramadhan Said ambaye ni Msaidizi wa Ofisi kutoka Mahakama ya Wilaya Wanging’ombe kuiwakilisha Kanda hiyo kama mtumishi bora anayefaa kuigwa na watumishi wengine kwa uchapakazi wake.

Upatikanaji wa Mtumishi huyo ulifanyika wakati wa Kikao cha Baraza la Wafanyakazi kilichofanyika hivi karibuni katika ukumbi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Njombe baada ya kushindanishwa watumishi wawili ambao sifa zao zilisomwa mbele ya wajumbe wa kikao hicho na kupigiwa kura.

Akielezea sifa zake katika kikao hicho, kilichoongozwa na Mwenyekiti ambaye ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Iringa, Mhe. Dunstan Ndunguru, Afisa Utumishi wa Mahakama ya Wilaya Wanging’ombe, Riziki Sanga alisema, Bw.Hassan amejifunza na anaweza kutumia vifaa vya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) katika mifumo ya Mahakama.

“Mtumishi huyu ameshiriki kikamilifu katika zoezi la ku ‘scan’ mafaili ya mashauri ya zamani yaliyoisha kwa ajili ya kuyasajili kwenye mfumo unaosimamia mashauri  mahakamani (e-CMS),” alisema Bw. Sanga.

Alieleza kuwa, Bw. Said ameshiriki kwa kiasi kikubwa katika kuanzisha na kusimamia bustani ya matunda aina ya parachichi yenye miche zaidi ya 40 iliyopo katika kiwanja cha Mahakama na ni mtumishi hodari anayetekeleza kazi zake za kila siku akiwa mtumishi pekee yake wa kutegemewa katika kada yake kwenye Mahakama hiyo.

Alieleza zaidi kuwa, Bw.Hassan ameweza kutunza jengo pamoja na viunga vyake vya  Mahakama ya Wilaya Wanging’ombe ambalo lipo katika hali ya usafi na nzuri kwa takribani miaka minne mpaka sasa.

“Mtumishi huyo amekuwa akimudu kufanya usafi peke yake katika ukubwa wa eneo zima la Mahakama hiyo ambalo lina takribani ukubwa wa mita za mraba 4,560 na kutekeleza maelekezo anayopatiwa na viongozi wake,” alisema.

Kadhalika aliongeza kwamba, Bw. Hassan amekuwa ni mtiifu, mwaminifu anayejituma na anapenda kujifunza mambo mapya pamoja na kujifunza kuhusu shughuli na taratibu za kuingia mahakamani na sasa anaingia na kutekeleza  majukumu hayo pasipo shaka

Alisema pia, mtumishi huyo ana nia ya kujiendeleza kielimu katika kozi za TEHAMA hili aweze kuongeza ujuzi  katika kusaidia Taasisi katika ujenzi wa taifa.


    Picha ya juu na chini ni Bw. Hassani Said, Mtumishi wa Mahakama ya Wilaya Wanging'ombe iliyopo Kanda ya Iringa akiwa anatimiza majukumu yake ya kufanya usafi kwenye viunga vya  nje ya jengo la Mahakama hiyo.

Mtumishi wa Mahakama ya wilaya Wangingombe kanda ya Iringa, Bw.Hassani Said akiwa anapanda na kuhudumia miti ya matunda aina ya parachichi katika eneo la Mahakama hiyo.


Bw. Hassan Said akiwa na kompyuta mpakato akifanya shughuli za kiTEHAMA nje ya majukumu yake ya kiofisi.

(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama)

 

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni