Na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dodoma
Jaji Mkuu wa Tanzania,
Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma amewahimiza Viongozi wa Mahakama kuchukua hatua
stahiki ili kuimarisha huduma ya utoaji haki katika Mahakama za Mwanzo nchini.
Mhe. Prof. Juma ametoa wito
huo leo tarehe 10 Aprili, 2025 alipokuwa anafungua Kikao cha siku mbili cha Baraza
la Wafanyakazi Taifa kinachofanyika katika Ukumbi wa PSSSF jijini Dodoma.
‘Ni ukweli usiopingika
kuwa Mahakama za Mwanzo zinaongoza kuwa na mashauri mengi kwa asilimia zaidi ya
70 ya mashauri yote yanayofunguliwa katika Mahakama zetu. Kwa maana nyingine,
Mahakama za Mwanzo ndizo zinazohudumia Wananchi wengi zaidi ya Mahakama
nyingine hapa nchini,’ amesema.
Jaji Mkuu amebainisha
kuwa katika Mpango Mkakati wa Miaka Mitano ijayo, ni lazima Viongozi na Watumishi
waelekeze nguvu zao katika kuimarisha ubora wa huduma za haki katika ngazi ya
Mahakama za Mwanzo.
Mhe. Prof. Juma amenukuu
hotuba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu
Hassan aliyoitoa katika hafla ya uzinduzi wa jengo la Makao Makuu ya Mahakama hivi
karibuni.
Katika hotuba yake, Rais
Samia, pamoja na kupongeza jitihada za Mahakama katika kutekeleza jukumu lake
la utoaji haki, alisisitiza uongozi wa Mahakama kutupia jicho zaidi katika
Mahakama za Mwanzo ambazo bado zinalalamikiwa na Wananchi.
‘Tunafahamu kuwa Mahakama
za Mwanzo bado zina changamoto nyingi za miundombinu, rasilimali watu na fedha.
Ninawasihi Viongozi wa Mahakama katika Kanda, Mikoa na Wilaya, zingatieni idadi
ya watu katika maeneo mnayopendekeza ujenzi wa Mahakama za Mwanzo,’ amesema.
Jaji Mkuu amewapongeza Watumishi wote wa Mahakama kwa kuendelea kufanya kazi kwa uadilifu, ueledi, uwajibikaji na kwa kulenga matokeo makubwa.
Amebainisha kuwa kwa
mujibu wa Ibara ya 107A ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhimili
wa Mahakama ni Mamlaka yenye Kauli ya Mwisho katika utoaji haki katika Jamhuri
ya Muungano.
Mhe. Prof. Juma amesema
kuwa Ibara ya 107B ya Katiba inatamka kuwa katika kutekeleza
mamlaka ya utoaji haki, Mahakama zote zitakuwa huru na zitalazimika kuzingatia
tu masharti ya Katiba na yale ya Sheria.
‘Ibara hizi zinatarajia Watumishi
kujipanga kimkakati na kuzingatia uadilifu, ueledi, uwajibikaji na kwa kulenga
matokeo makubwa,’ Jaji Mkuu amesema.
Akizungumzia maslahi ya Watumishi,
Mhe. Prof. Juma alibainisha kuwa anafahamu kuwa bado suala hilo linahitaji kufanyiwa
kazi kwa karibu na Viongozi wa Mahakama.
Amekumbushia kuwa wakati
akizindua Jengo la Makao Makuu ya Mahakama, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan aliwakumbusha kuwa bado michakato na
majadiliano ya maboresho ya maslahi kwa Watumishi wa Mahakama inaendelea.
‘Sisi kama Viongozi wa Mahakama
tumekuwa tukijadiliana na Serikali kuhusu maslahi ya Watumishi wa Mahakama na
ndiyo maana baadhi yenu mtakuwa mashuhuda kuwa juhudi hizo zimezaa matunda,’ amesema.
Meza Kuu na wajumbe wa Baraza kutoka Kanda ya Mororogo. Picha chini ni wajumbe kutoka Kanda ya Dar es Salaam.
Meza Kuu na wajumbe wa Baraza kutoka Kanda ya Mtwara. Picha chini ni wajumbe wa Divisheni ya Rushwa na Uhujumu Uchumi.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni