Na Lydia Churi- Tume ya Utumishi wa Mahakama, Rukwa
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania na Kamishna wa
Tume ya Utumishi wa Mahakama Mhe. Dkt. Mustapher Siyani ametoa wito kwa
Viongozi wa Umma na Wananchi kwa ujumla kujiepusha kuzungumzia au kutoa
misimamo juu ya mashauri yanayoendelea mahakamani.
Akizungumza kwenye Mkutano wa Tume na wadau wa utoaji
haki mkoani Katavi jana tarehe 28 Mei, 2025, Jaji Kiongozi amesema kumekuwa na
mazoea kwa Vongozi wa Umma na wananchi kutoa matamko juu ya mashauri
yanayoendelea mahakamani hali ambayo inawaweka katika wakati mgumu Majaji na
Mahakimu wanaosikiliza mashauri kutoa uamuzi huru.
Alisema mara nyingi jamii imekuwa ikiamini matamko
yanayotolewa na Viongozi na hivyo kutarajia
uamuzi wa shauri husika kuwa kama vile maoni, matamko au misimamo iliyotolewa na
Viongozi.
Jaji Kiongozi alisema Tume ya Utumishi wa Mahakama na
Mahakama ya Tanzania inatarajia kuona Viongozi wote na wananchi kwa ujumla wakijizuia
kutoa matamko, maoni au misimamo kwenye mashauri yanayoendelea mahakamani ili
kulinda uhuru wa Mahakama na kujenga imani ya wananchi kwa Mhilimili huo wenye kauli
ya mwisho juu ya utoaji haki nchini.
Aidha alisema Tume na Mahakama pia inatarajia kuona kuwa wananchi
na viongozi wa Umma wataimarisha ushirikiano na Mahakama katika maboresho ya
huduma za zake yanayoendelea katika maeneo mbalimbali nchini.
Akizungumzia nafasi ya Kamati za Ulinzi na Usalama za
Mikoa na Wilaya, Jaji Kiongozi ametoa wito kwa Kamati hizo kuanza kutazama
visababishi vya uhalifu badala ya kujikita katika ukamataji na upelelezi baada
ya makosa kutokea.
Alifafanua kuwa Kamati hizi zinalo jukumu la kuhakikisha
kunakuwa na amani na utulivu nchini. Kamati hizi pia zina jukumu la kuchunguza
visababishi vya uhalifu unaotishia usalama wa Umma na kuzuia vitendo hivyo.
Alisema matarajio ya Tume na Mahakama ni kuona wadau wa
haki wakihamasisha Umma kutumia huduma za Mahakama katika kutatua migogoro yao
na pia kuona kamati hizi zikihakikisha usalama kwa Maafisa Mahakama na
watumishi wengine kwa ujumla ili kuwawezesha kutekeleza majukumu yao kwa
maslahi ya Umma.
Kuhusu uwepo wa kamati za maadili za Mawakili katika
ngazi za mikoa, Jaji Kiongozi alisema ni muhimu wananchi wakaelimishwa kuhusu
uwepo wa kamati hizo katika mikoa ili wazitumie kuwasilisha malalamiko yao huko
badala ya kuyapeleka Makao Makuu ya Mahakama.
Alisema wananchi hawafahamu kuwa katika maeneo yao kuna
kamati za maadili ambazo zingeweza kusilkiliza changamorto za maadili ya
Mawakili hivyo alikitaka chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) kuhakikisha
inawaelimisha wananchi uwepo wa kamati hizo na pia kushughulikia maadili ya
wanachama wake.
”Tume na Mahakama inatarajia kupungua kwa malalamiko
yanayoletwa moja kwa moja Makao Makuu ya Mahakama na badala yake kamati
zilizopo mikoani zishughulikie malalamiko hayo”, alisisitiza Dkt. Siyani
Kwa upande wa Madalali na Wasambaza Nyaraka wa Mahakama,
Kamishna huyo wa Tume alisema hawa ni wadau muhumu wa Mahakama wanaochakata
hatua ya mwisho ya upatikanaji wa haki mahakamani hususan katika mashauri ya
madai. Alisema Madalali na Wasambaza nyaraka ndiyo wanaotekeleza amri za Mahakama
kwenye mashauri hayo na mipaka yao ya kazi ni mikoa.
Alisema wadau wa utoaji haki hawana budi kuwaelimisha wananchi
kuzitumia nafasi za Madalali ili kurahisisha mchakato wa upatikanaji wa haki na
pia kuwahamasisha wananchi kujitokeza kufanya kazi hii. Mkoa wa Katavi una
Dalali moja tu wakati nchi nzima ina Madalali 118.
Akizungumzia kutenda haki, Jaji Kiongozi amewataka wadau
wa utoaji haki nchini kuongozwa na dhamira ya kutenda haki katika kila hatua ya
mchakato wa uapatikanaji wa haki.
Alisema Tume na Mahakama inatarajia kuwa wadau wote walio
kwenye mnyororo wa utoaji haki wataongozwa na dhamira ya kutenda haki kwa kuwa
dhamira hii ikitawala malalamiko kuhusu kutokutendewa haki kwa wananchi
yataisha na mashauri yenye ushahidi tu ndiyo yatafikishwa mahakamani hivyo kurahisisha
mchakato wa upatikanaji wa haki nchini.
Kamishna alisisitiza kuwa kwa wadau kuongozwa na dhamira
ya kutenda haki katika kila hatua kutaimarisha imani ya wananchi kwa Mhimili wa
Mahakama na kwa vyombo vyote vinavyohusika na upatikanaji wa haki nchini.
Wadau wa Utoaji haki Mkoa wa Katavi wakiwa kwenye Mkutano kati yao na Tume ya Utumishi wa Mahakama jana mjini Mpanda.
Jaji Mkuu wa Tanzania na Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi wa Mahakama Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akiwa katika picha ya pamoja na Wadau wa Utoaji haki Mkoa wa Katavi jana mjini Mpanda.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni