Jumanne, 13 Mei 2025

JAJI MKUU WA TANZANIA AMLILIA CLEOPA DAVID MSUYA

  • Asema alikuwa Kiongozi jasiri, shupavu, mstahimilivu

Na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dodoma

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma, leo tarehe 13 Mei, 2025 ameungana na Watanzania katika maziko ya Makamu wa Kwanza wa Rais na Waziri Mkuu Mastaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Marehemu Cleopa David Msuya, aliyefariki dunia tarehe 7 Mei, 2025.

Mhe. Msuya amezikwa katika Kijiji cha Chomvu, Kata ya Chomvu Wilaya ya Mwanga, Mkoa wa Kilimanjaro, tukio ambalo limeongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan na kuhudhuriwa na Viongozi mbalimbali wa kitaifa wa Serikali, Bunge na Mahakama, Wastaafu, Viongozi wa Dini na Wananchi wengi.

Akiwasilisha salamu za faraja kwa niaba ya Mahakama ya Tanzania, Jaji Mkuu amemwelezea Mhe. Msuya kama Kiongozi jasiri, shupavu na mstahimilivu kwenye nafsi yake ambayo aliitumia katika kuleta maendeleo makubwa katika Taifa.

‘Ushupavu na ustahimilivu wake huo ndiyo uliofanya apewe kazi ngumu, zenye joto. Kati ya mwaka 1978 na 1979 kulikuwa na moto wa Vita vya Kagera na mwaka 1980 akapewa kazi ya Uwaziri Mkuu, siyo kazi nyepesi, hasa ukizingatia hali ya uchumi. Kwa hiyo, unahitaji mtu wa aina fulani kuweza kuhimili kazi hiyo,’ Mhe. Prof. Juma amesema.

Jaji Mkuu ameeleza kuwa Tanzania ilipitia katika changamoto kubwa za kiuchumi, hasa baada ya bei ya bidhaa za mazao kama kahawa kushuka, bei ya mafuta kupanda na hali mbaya ya uchumi iliyotokana na vita, lakini Mzee Msuya akapewa Uwaziri wa Fedha.

Mhe. Prof. Juma ameeleza kuwa Mzee Msuya alitegemewa na Baba wa Taifa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Awamu ya Kwanza, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere pamoja na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Awamu ya Pili, Mzee Ali Hassan Mwinyi kwa sababu hakuwa mtu jeuri na mkali, bali mtumishi mwadilifu na mchapakazi hodari.

‘Wale wazee wa zamani mtakumbuka msimamo wa Baba wa Taifa dhidi ya kukubali masharti ya Shirika la Fedha duniani na Benki ya Dunia. Tunaambiwa kulikuwa na mvutano mkali kama Serikali ikubali kujadiliana na Shirika la Fedha. Majadiliano yalichukua zaidi ya miaka minne, wakati huo huo uchumi unadorora,’ amesema.

Jaji Mkuu amemsifia Mzee Msuya kutokana na uwezo mkubwa aliokuwa nao wa kuweza kumsoma Mwalimu Nyerere kwa urahisi zaidi kuliko watu wengi kuwa alikuwa amekubali kwamba wakati umefika wa majadiliano na Benki ya Dunia ingawa wengi katika Serikali na Chama walikuwa na mawazo tofauti.

Hivyo amewaomba Wananchi kuendelea kudadisi maisha ya Marehemu Msuya, kwani kuna mambo mengi ambayo wanaweza kujifunza kwa sasabu yeye ameona siasa ya ujamaa na kujitegemea, mabadiliko ya kiuchumi na hali ya sasa ambayo inazungumzia teknolojia.

Cleopa David Msuya alifariki tarehe 7 Mei, 2025 katika Hospitali ya Mzena Jijini Dar es Salaam alipokuwa amelazwa akipatiwa matibabu ya ugonjwa wa moyo.  Kufuatia kifo hicho, Rais Samia alitangaza siku saba za maombolezo hadi tarehe 13 Mei, 2025 na kuwapa pole ndugu, jamaa na Watanzania wote kwa msiba huo mzito kwa Taifa.

Mhe. Cleopa David Msuya alizaliwa tarehe 4 Januari 1931 katika kijiji cha Chomvu, Usangi, wilayani Mwanga, mkoani Kilimanjaro. Alisoma katika Chuo Kikuu cha Makerere kuanzia mwaka 1952 hadi 1955. Baada ya hapo, alijihusisha na kazi za maendeleo ya jamii na huduma kwa Wananchi vijijini kuanzia mwaka 1956 hadi 1964.

Kuanzia mwaka 1964, Msuya alihudumu kama Katibu Mkuu katika Wizara mbalimbali: Wizara ya Maendeleo ya Jamii na Utamaduni (1964–1965), Wizara ya Ardhi, Makazi na Maendeleo ya Maji (1965–1967), Wizara ya Mambo ya Uchumi na Mipango (1967–1970) na Wizara ya Fedha (1970–1972).

Mnamo tarehe 18 Februari 1972, Mhe. Msuya aliteuliwa kuwa Waziri wa Fedha na alihudumu hadi alipohamishiwa kuwa Waziri wa Viwanda mnamo tarehe 3 Novemba 1975.

Baada ya kuhudumu kwa miaka mitano kama Waziri wa Viwanda, aliteuliwa kuwa Waziri Mkuu mnamo Novemba 1980, nafasi aliyoshikilia hadi Februari 1983. Baadaye, alirudi tena kuwa Waziri wa Fedha kutoka Februari 1983 hadi Novemba 1985.

Tarehe 6 Novemba 1985, Mhe. Msuya alipewa jukumu jipya akiwa Waziri wa Fedha, Mambo ya Uchumi na Mipango hadi Machi 1989, kisha alirudi kuwa Waziri wa Fedha tena kuanzia Machi 1989 hadi Desemba 1990, na baadaye kuwa Waziri wa Viwanda na Biashara kutoka Machi 1990 hadi Desemba 1994.

Mwaka 1994, aliteuliwa tena kuwa Waziri Mkuu kwa mara ya pili, na pia kuhudumu kama Makamu wa Kwanza wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hadi Novemba 1995.

Katika uchaguzi wa Bunge wa mwaka 1995, Mhe. Msuya alichaguliwa tena kuwa Mbunge na alihudumu hadi alipostaafu rasmi tarehe 29 Oktoba 2000.

Baada ya kustaafu, Msuya aliendelea kuwa mwanachama hai wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), na kufikia mwaka 2006 alikuwa bado ni mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM. Pia alikuwa Mwenyekiti wa Jukwaa la Maendeleo la Kilimanjaro.

Mnamo Oktoba 23, 2019, akiwa na umri wa miaka 88, Mhe. Msuya aliteuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Awamu ya Tano, Hayati John Pombe Magufuli kuwa Mkuu wa Chuo cha Ardhi.


Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akizungumza katika ibaada maalum ya mazishi ya Makamu wa Kwanza wa Rais na Waziri Mkuu Mastaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Marehemu Cleopa David Msuya iliyofanyika leo tarehe 13 Mei, 2025 mkoani Kilimanjaro. Picha chini ikionesha mwili wa Marehemu Msuya wakati wa ibaada hiyo.

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni