Na ASHA JUMA –Mahakama, Morogoro
Katika juhudi za kuimarisha utoaji wa haki kwenye kesi za Watoto nchini,
Mahakama ya Tanzania imeandaa kikao kazi maalum kupitia na kuboresha mwongozo
wa usimamizi na ukaguzi wa Mahakama za Watoto.
Lengo la maboresho hay oni kuhakikisha kuwa haki za Watoto zinalindwa
kwa mujibu wa viwango vya kitaifa na kimataifa.
Aidha, kikao cha siku tano kinachofanyika kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Kituo
Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) Morogoro kimekusudia kutathmini ufanisi wa
uendeshaji wa Mahakama hizo, pamoja na kuandaa orodha ya vipengele muhimu
vitakavyotumika katika ukaguzi wa Mahakama za Watoto kote nchini.
Kikao hicho kinahudhuriwa na Jaji wa Mahakama Kuu Tanzania, Kanda ya
Arusha, Mhe. Nyigulila Mwaseba ambaye ni Mwenyekiti na Maofisa wengine kutoka
maeneo mbalimbali nchini. Kikao hicho pia kinahusisha Maofisa wa ndani wa
Mahakama, wakiwemo Majaji na Mahakimu.
Ushirikiano huu unalenga kuhakikisha kuwa Mahakama za Watoto zinakuwa na
mazingira rafiki na kwamba mashauri yanayowahusu Watoto yanashughulikiwa kwa
weledi na kwa kuzingatia haki zao za msingi.
Muongozo wa awali wa usimamizi na ukaguzi wa uendeshaji wa Mahakama za
Watoto ulifanyiwa marekebisho mwaka 2019 na sasa unafanyiwa mapitio ili
kujumuisha vipengele mahususi vinavyohitajika kuzingatiwa katika ukaguzi wa
Mahakama za Watoto.
Hii ni sehemu ya juhudi za Mahakama ya Tanzania kuhakikisha kuwa mfumo
wa utoaji haki kwa Watoto unakuwa wa haki, wa haraka na unaozingatia maslahi
bora ya Mtoto.
Mahakama ya Tanzania imekuwa ikichukua hatua mbalimbali za kuimarisha
haki za Watoto, ikiwemo kuanzisha Mahakama za Watoto katika Mikoa mbalimbali na
kutoa mafunzo kwa Majaji na Mahakimu kuhusu usikilizaji wa mashauri ya Watoto.
Kupitia kikao kazi hicho, Mahakama ya Tanzania inaendelea kuonesha dhamira yake ya dhati ya kuhakikisha kuwa haki za Watoto zinalindwa na kuendelezwa na kuimarisha mifumo ya usimamizi na ukaguzi wa Mahakama za Watoto nchini.
Maofisa wa kikao kazi-juu na picha mbili chini- wakiwa wanajadili masuala mbalimbali.
Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Arusha, Mhe. Nyigulila Mwaseba (katikati) ambaye ni Mwenyekiti wa kikao kazi, Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Usimamizi, Ukaguzi wa Huduma za Kimahakama, Mrejesho kwa Umma na Maadili, Mhe. Karol Mashauri (kushoto) na Naibu Msajili Mahakama Kuu, Masjala Kuu anayeshughulika Masuala ya Watoto, Mhe. Mwajabu Mvungi (kulia) wakiwa pamoja na Maofisa wa kikao kazi-juu na chini.
Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dodoma.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni