Alhamisi, 15 Mei 2025

JOPO LA MAJAJI MAHAKAMA YA RUFANI KUSHUGHULIKIA MASHAURI 26 KIGOMA

Na AIDAN ROBERT-Mahakama, Kigoma

Mahakama ya Rufani Tanzania imepanga kusikiliza mashauri 26 kwenye kikao kitakachofanyika katika masjala ndogo kwenye jengo la Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Kigoma, kuanzia tarehe 12 hadi 30, Mei 2025.

Kikao hicho kitakuwa chini ya jopo la Majaji watatu watakaoongozwa na Mhe. Stella Mugasha, ambaye ni Mwenyekiti. Majaji wengine wanaounda jopo hilo ni Mhe. Lucia Kairo na Mhe. Mustafa Ismail.

Akizungumza wakati anafungua kikao cha awali cha maandalizi (pre-session), Mhe. Mugasha alisisitiza Wadau wote wanaohusika kwenye kikao hicho kukamilisha mapema maandalizi na kuzingatia muda wa kuanza shughuli za Mahakama.

‘Mawakili mnaowasimamia Washitakiwa waliopo gerezani mjitahidi kuwaona mapema na kusoma vyema vitabu vya mashauri. Mfanye hivyo kwa makini ili tutakapoanza kusikiliza mashauri haya tusiwe na mkwamo ambao unagusa maeneo  ambayo tunapaswa kujiandaa mapema,’ alisema.

Akitoa taarifa ya usikilizaji wa mashauri hayo, Naibu Msajili, Mhe. Dyness Lyimo alisema kuwa kikao hicho cha Mahakama ya Rufani ni cha kwanza kufanyika katika Kanda ya Kigoma kwa mwaka 2025.

Mhe. Lyimo alitanabaisha kwamba jumla ya mashauri ya jinai 20 na mashauri ya madai sita, yanayoleta idadi ya mashauri 26 ndio yaliyopangwa kusikilizwa na kutolewa uamuzi na jopo hilo.

Baada ya kikao hicho cha maandalizi, Majaji wa Mahakama ya Rufani na wale wa Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma walipata fursa ya kupanda miti ya matunda na kivuli eneo la Mahakama hiyo, ikiwa ni sehemu ya kutekeleza mpango mkakati wa Mahakama wa kutunza mazingira.

Awali, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Kigoma, Mhe. Augustine Rwizile aliwaongoza Watumishi kuwapokea Majaji hao wa Mahakama ya Rufani waliowasili Kigoma tarehe 8 Mei 2025.


Jaji wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Stella Mugasha, akitia saini kitabu cha wageni mara baada ya kuwasili katika jengo la Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Kigoma.

Jopo la Majaji watatu wa Mahakama ya Rufani-juu na chini-likiwa katika kikao cha awali kutathimini maandalizi ya kusikiliza mashauri.

Majaji wa Mahakama ya Rufani, Majaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma pamoja na  wajumbe wa kikao cha maandalizi wakitembelea mazingira ya nje ya jengo la Mahakama Kuu Kigoma.

Jaji wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Stella Mugasha akipanda mti wa matunda katika eneo la Mahakama Kuu Kigoma.

Jaji wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Lucia Kairo akipanda mti wa matunda katika eneo la Mahakama Kuu Kigoma.

Jaji wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Mustafa Ismail akipanda mti wa matunda eneo la Mahakama Kuu Kigoma.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Kigoma, Mhe. Augustine Rwizile akipanda mti wa matunda eneo la Mahakama Kuu Kigoma.

Majaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma, Mhe. John Nkwabi-juu-na Mhe. Projestus Kahyoza-chini-wakipanda miti ya matunda eneo la Mahakama Kuu Kigoma.

Naibu Msajili wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Dyness Lyimo akipanda mti wa matunda eneo la Mahakama Kuu Kigoma.

Majaji wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Stella Mugasha (Katikati waliokaa), Mhe. Lucia Kairo, (wa tatu kushoto), Mhe. Mustafa Ismail (watatu kulia), wakiwa katika picha ya Pamoja na Majaji wa Mahakama Kuu Kigoma na wajumbe wa kikao cha maandalizi ya awali(pre-session).

Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dodoma

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni