· Ni wakati akifungua kikao kazi cha Divisheni hiyo kilichohusisha Majaji Wafawidhi, Wade
· Awataka Majaji wengine kuendeleza na kuimarisha ushirikiano na wadau kuongeza ufanisi katika utoaji haki
Na
MARY GWERA, Mahakama-Arusha
Jaji
Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Mustapher Mohamed Siyani ameipongeza
Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi kwa kuendelea kuwa mfano katika utekelezaji wa
nguzo nambari tatu ya Mpango Mkakati wa Mahakama ya Tanzania inayohusu Imani
kwa Wananchi na ushirikishwaji wa wadau.
Akizungumza
leo tarehe 15 Mei, 2025 wakati akifungua Kikao cha Haki Kazi baina ya Shirika
la Kazi Duniani (ILO) na Majaji Wafawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania na wadau wa haki kazi wa Mahakama kinachofanyika
katika ukumbi wa Hoteli ya ‘Corridor Springs’ jijini Arusha, Mhe. Siyani amesema jambo hili la
kuwakutanisha wadau wa haki na kujadili masuala mbalimbali ni muhimu kwa mustakabali wa utendaji kazi wa Mahakama.
“Ninawapongeza Mahakama Kuu Divisheni ya
kazi kwa kuendelea kuwa mfano wa utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Mahakama
kwenye eneo hili la ushirikishwaji wa wadau, kipekee nimpongeze Mhe. Dkt Yose
Mlyambina, Jaji Mfawidhi wa Divisheni hii na wenzake wamekuwa mfano bora wa
ubunifu unaowezesha Mahakama na wadau wake kukutana mara kwa mara na kujengeana
uwezo katika maeneo mbalimbali kwa lengo la kuboresha utendaji kazi,” amesema
Jaji Kiongozi.
Aidha,
Mhe. Siyani amesema kupitia Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi, Mahakama imeweza
kuwashirikisha wadau mbalimbali kama vile Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF),
Wakala wa Usalama na Afya Mahala pa Kazi (OSHA) na Shirika la Kazi Duniani
(ILO).
“Hatua hii ya wadau wa Mahakama kuja pamoja kwa lengo moja ni muhimu kwa mafanikio ya taasisi yoyote na kwa Mahakama ni muhimu zaidi kwani majadiliano na uzoefu unaopatikana, unasaidia sana kuimarisha mifumo ya utoaji haki kazi nchini. Kwa hiyo, kwa dhati kabisa, ninawashukuru wadau wetu wote,” amesisitiza.
Aidha, Jaji Kiongozi ametoa wito kwa Majaji Wafawidhi na Majaji wote wa Mahakama Kuu nchini kuendelea kuimarisha ushirikiano na Wadau ili kuboresha ufanisi sambamba na kujenga Mahakama inayoshirikiana na jamii.
Ameongeza kuwa, suala la kuboresha ufanisi katika utoaji wa haki kupitia vikao kazi na mafunzo, ni jukumu endelevu kwakuwa kupitia vikao kama hivyo wanapata fursa ya kubadilishana uzoefu, kutathmini changamoto zilizopo, kuainisha maeneo yanayohitaji maboresho na hatimaye kuandaa mikakati madhubuti itakayoimarisha kasi ya utoaji haki.
Amesema
kuwa, fursa hiyo ya kukutana na wadau ni muhimu kwani inalenga kuboresha mifumo
ya utoaji haki na hatimaye kuwezesha watu kupata haki kwa wakati lakini katika
mazingira ya uwazi na yanayoaminika.
“Ni muhimu kukumbuka kuwa, Taifa lolote lisilo na mifumo bora ya kutoa haki, inaweza kutumbukia kwenye machafuko yasiyo ya lazima. Kwa hiyo, kwa sisi tuliopata fursa ya kuwatumikia wenzetu katika vyombo hivi, ni lazima tukumbuke wajibu wetu ambao hauwezi kukamilika kama fursa hizi muhimu za kuongeza maarifa hazitapatikana,” ameeleza.
Amesisitiza pia juu ya umuhimu wa Majaji kuendana na kasi ya mabadiliko duniani na kwamba vikao kazi kama hicho ni njia moja wapo ya kufanya hivyo.
Kadhalika, Mhe. Siyani amesema kwamba, eneo la haki kazi ni muhimu kwani migogoro ya kazi sio tu inaathiri wafanyakazi na waajiri, bali maendeleo ya uchumi wa taifa kwa ujumla ambapo ameeleza kuwa, migogoro isiyoshughulikiwa kwa haraka husababisha uzalishaji kushuka, wawekezaji kupoteza imani na wakati mwingine hata kusababisha athari za kijamii kama vile migomo na hali ya kutoelewana mahala pa kazi.
Ameseisitiza kuwa, “ili kufanikisha utoaji wa haki kazi kwa wakati na kwa ufanisi, ni muhimu kwa wadau wote ikiwemo Mahakama, Ofisi ya Kamishna wa Kazi, Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA), waajiri, wafanyakazi, OSHA, mifuko ya hifadhi ya jamii na mashirika ya kimataifa kama ILO kushirikiana kwa ukamilifu.”
Hali kadhalika amesema kuwa, Mahakama lazima iendelee kujipanga na kuboresha mifumo yake ya usikilizaji wa mashauri ya kazi, ikiwemo matumizi ya TEHAMA kwa lengo la kuwezesha haki kazi kutendekea kwa wakati na gharama nafuu.
Katika neno lake la ufunguzi, Jaji Kiongozi amewasisitiza Majaji hao kuongeza uwazi na uwajibikaji katika kushughulikia mashauri yote ikiwemo yale ya kazi, kuhakikisha matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) yanaimarishwa ili kuboresha huduma za Mahakama, kuimarisha mafunzo ya viongozi wa Mahakama kuhusu haki kazi, sheria za kimataifa na utatuzi wa migogoro ya kazi kwa kutumia akili unde (AI).
Kwa
upande wake Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Divisheni ya Kazi, Mhe.
Dkt. Yose Mlyambina amesema kuwa Kikao Kazi kimebeba Kaulimbiu isemayo ‘Uboreshaji
wa Uongozi kwa Ufanisi na Tija katika Utoaji wa Haki Kazi’ na kutoa rai kwa Majaji wenzake kuwa Viongozi wa maono na kuwa Taasisi
inayosimamia haki.
Mhe.
Mlyambina amesema kuwa, kikao kazi hicho kitakuwa na mada mbalimbali ambazo ni pamoja
na Akili ya kihisia na udhibiti wa mafadhaiko, motisha kwa watumishi na kujenga
ujasiri, uongozi na usimamizi wa mabadiliko, kanuni za maadili za uongozi na
uadilifu na nyingine.
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Mustapher Mohamed Siyani akifungua Kikao cha Haki Kazi leo tarehe 15 Mei, 2025 kilichoshirikisha Shirika la Kazi Duniani (ILO) na Majaji Wafawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania na wadau wa haki kazi wa Mahakama kinachofanyika katika ukumbi wa ‘Corridor Springs Hotel’.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni