Alhamisi, 15 Mei 2025

JAJI MKUU AZINDUA JUKWAA LA KUFUNDISHIA KWA NJIA YA MASAFA

Na INNOCENT KANSHA - Mahakama

Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma leo tarehe 15 Mei, 2025 amezindua rasmi Mfumo wa Mafunzo kwa Njia ya Mtandao (e-Learning Platform) pamoja na kukabidhi jengo la kisasa la Media Studio itakayotumika kuandaa mitaala ya kufundishia katika Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA).

Uzinduzi huo umefanyika kwa njia ya mkutano mtandao wakati Mhe. Prof. Juma akiwa ofisini kwake jijini Dar es Salaam huku akiambatana na Msajili Mkuu wa Mahakama Mhe. Eva Nkya pamoja na Mtendaji Mkuu wa Mahakama Prof. Elisante Ole Gabriel, huku Viongozi na Maafisa wengine waandamizi wa Mahakama wakifuatilia kwa njia hiyo ya mkutano mtandao kutokea Dar es salaam, Dodoma na Lushoto.

“Ni faraja kubwa kwamba uzinduzi huu unafanyika kwa njia ya mtandao, jambo linaloendana kikamilifu na dhamira ya Mahakama ya Tanzania kutumia teknolojia katika nyanja zote za utoaji huduma na kuonesha kwa vitendo kuwa Mahakama yetu ni taasisi inayoendana na mabadiliko ya kidijitali,” amesema Jaji Mkuu.

Katika hotuba yake, Mhe. Prof. Juma amesema kuwa mfumo huo unakwenda kuwezesha watumishi wengi wa Mahakama kupata mafunzo mbalimbali bila kikwazo cha kifedha, gharama na muda. Mfumo unampa msomaji uhuru wa kupanga muda unaomfaa kwa kusoma pamoja na kuchagua mazingira rafiki ya kusoma.

Aidha, Mhe. Prof. Juma amebainisha faida nyingi za Mfumo wa Mafunzo kwa Njia ya Mtandao (e-Learning Platform) kama vile, urahisi wa kufikisha mafunzo kwa wasomaji wengi na kwa muda mfupi na kuwa mada zote zinapakiwa kwenye mfumo na zinapatikana muda wowote kwa njia ya mtandao, inapotokea kunakuwa na uhitaji wa mafunzo ya aina yeyote ni rahisi sana kuwafanya wasomaji wengi waweze kusoma na kumaliza mada zao ndani ya muda mfupi tofauti na mafunzo yanayotolewa ana kwa ana ambapo ingewalazimu  wakufunzi kuwazungukia    wasomaji/wanafunzi maeneo walipo au kuwakusanya sehemu moja na kuwapatia mafunzo.

Vilevile, faida nyingine ni urahisi wa kufanya mabadiliko ya mtaala Inapotokea kunakuwa na mabadiliko yeyote ya mtaala au sheria au chochote katika mada, inakuwa rahisi kufanya mabadiliko kwenye mfumo,na mbadiliko hayo kuwafikia walengwa papo hapo.

“Ni dhahiri shahiri kuwa kutakuwa na unafuu wa gharama za utoaji mafunzo Mafunzo haya yanapunguza gharama kwa upande wa rasilimali fedha, muda na nafasi,” ameongeza Jaji Mkuu.

Jaji Mkuu amesema, sambamba na ujenzi wa Mfumo huo, pia umefanyika ukarabati mkubwa wa jengo lililopo Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA) kwa kulifanya kuwa Media studio ya kisasa yenye vifaa vya TEHAMA. Studio hiyo ni maalum kwa ajili ya uzalishaji wa mada mbalimbali za kujifunzia, zitakazobadilishwa kuwa katika mfumo wa kieletroniki na kupakiwa kwenye Mfumo wa mafunzo kwa njia ya mtandao kwa ajili ya matumizi ya wanufaika wa mafunzo yatakayotolewa kwa njia hiyo ya masafa.

Aidha, Mhe. Prof. Juma ameongeza kuwa, Mahakama imejipanga kikamilifu kuutumia mfumo huu ili uweze kuleta tija katika kubadili utendaji kazi wa Watumishi. Hivyo, uwekezaji wa Mfumo huu utaboresha huduma za Mahakama, kwa kuwa watumishi wengi watafikiwa na mafunzo kwa wakati pasipo kujali utofauti wa kijiografia na hivyo kupunguza mlundikano wa mashauri, kuongeza uwazi katika utoaji wa haki, na kuimarisha imani ya wananchi.

“Nitoe rai kwa Mtendaji Mkuu na Msajili Mkuu wa Mahakama kuwa, ushirikiano baina ya Mahakama na Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA) uendelee ili kuhakikisha matumizi ya Mfumo yanakuwa endelevu kwa kufanya kazi kwa pamoja na kazi ya kujenga umahiri wa watumishi na wadau inakuwa endelevu,” amesisitiza Jaji Mkuu.

Vilevile, Mhe. Prof. Juma amesema kwamba, hali ya Watumishi kukosa mafunzo kutokana na changamoto ya ufinyu wa bajeti itaondolewa na jukwaa hilo na kuhakikisha uwezo, ujuzi na umahiri wa Watumishi na wadau wa Mahakama unaimarika.

“Sote tunajua kuwa Mahakama ilikuwa inaandaa Mipango ya Mafunzo ya kila mwaka, lakini kwa sababu za ufinyu wa bajeti, mipango hiyo ilikuwa inatekelezwa kwa kiwango kidogo sana. Hili linakwenda kumalizwa na uwepo wa mfumo huu kwa kuwafikia watumishi wengi kwa wakati mmoja na kuwa, hakutakuwa na vizuizi vya kijiografia, muda au rasilimali. Hivyo, kuendelea kufanya kazi kwa pamoja kutawezesha lengo la ujenzi wa Mfumo kufikiwa kwa haraka,” amesema Jaji Mkuu huyo.

Vilevile Mhe. Prof. Juma amesema kuwa mfumo huo utaiwezesha IJA kutoa mafunzo ya muda mrefu ya ngazi ya Stashahada (Diploma) na Astashahada (Cheti) ya Sheria na hivyo kuwarahisishia  watu kujifunza elimu ya sheria popote walipo.

Aidha Jaji Mkuu ametoa wito kwa Uongozi wa Mahakama na wa IJA kuhakikisha wana usimamia vizuri mfumo huo uwe endelevu ikizingatiwa kuwa umegharimu kiasi cha shilingi bilioni 1.36 za Kitanzania.

Wakati huo huo, Jaji Mkuu amezindua mafunzo ya kundi la kwanza la Washiriki 25 ambao ni Naibu Wasajili 5, Mahakimu Wakazi Wafawidhi wa mikoa 5 na Mahakimu Wakazi Wafawidhi wa Mahakama za Wilaya 15 wanaochukua mafunzo ya kiuongozi kupitia mada ya "Enhancing Leadership and Practical Skills for Registrars, Deputy Registrars, and Magistrates in-charge.

Awali, Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA) ambaye pia ni Jaji wa Mahakama ya Rufani Mhe. Dkt. Paul F. Kihwelo akitoa taarifa fupi ya ujenzi wa mradi huo, ameuelezea mfumo huo ulijengwa kwa kusema kuwa umejengwa ili kutatua changamoto ya watumishi wengi wa Mahakama kukosa mafunzo kwa sababu za kifedha, umbali na muda.

Pia amesema kuwa mfumo huo ambao tayari una mada tatu, unamuwezesha mwanafunzi kujisomea mwenyewe ndani ya mwezi mmoja na unasahihisha wenyewe mitihani na majaribio.

Aidha, Mhe. Dkt. Kihwelo amesema kuwa, mfumo huo pamoja na studio ni sehemu ya utekelezaji wa Mpango mkakati wa Mahakama katika awamu ya pili ya Maboresho ya Mahakama na umefadhiliwa na Serikali ya Tanzania kupitia Benki ya Dunia.

Jukwaa hilo la kufundishia mtandaoni lilijengwa na wataalamu wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) kutoka Mahakama ya Tanzania, IJA, Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT) na Chuo cha Serikali za Mitaa (Hombolo).

Ni imani kuwa mfumo huu utakuwa chachu ya mabadiliko ya kiutendaji, kwa kusaidia kuimarisha weledi wa watumishi wetu na kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa kazi za Mahakama kwa kuwa Watumishi watapata fursa ya kupatiwa mafunzo mbalimbali kwa gharama nafuu na kuwafikia wengi kwa wakati mmoja,” ameongeza Jaji Kihwelo.

Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akitoa hotuba wakati wa  uzindua rasmi wa Mfumo wa Mafunzo kwa Njia ya Mtandao (e-Learning Platform) pamoja na kukabidhi jengo la kisasa la Media Studio itakayotumika kuandaa mitaala ya kufundishia katika Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto 
(IJA) leo tarehe 15 Mei, 2025 ofisini kwake jijini Dar es salaam.


Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akitoa hotuba wakati wa  uzindua rasmi Mfumo wa Mafunzo kwa Njia ya Mtandao (e-Learning Platform) pamoja na kukabidhi jengo la kisasa la Media Studio itakayotumika kuandaa mitaala ya kufundishia katika Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA) leo tarehe 15 Mei, 2025 ofisini kwake jijini Dar es salaam.


Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA) ambaye pia ni Jaji wa Mahakama ya Rufani Mhe. Dkt. Paul F. Kihwelo akifuatilia mkutano mtandao huo

Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Mhe. Eva Nkya akifuatilia mkutano mtandao huo

Msajili wa Mahakama ya Rufani ya Tanzania Mhe. George Helbert akifuatilia mkutano mtandao huo

Timu ya ufundi ikiwa inaratibu shughuli ya Uzinduzi huo uliofanyika kwa njia ya mkutano mtandao 


Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akitoa hotuba wakati wa  uzindua rasmi Mfumo akiwa ameambatana na Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Mhe. Eva Nkya (kulia)  pamoja na Mtendaji Mkuu wa Mahakama Prof. Elisante Ole Gabriel (kushoto) wakifuatilia mkutano mtandao huo


Viongozi na Maafisa wengine waandamizi wa Mahakama wakifuatilia kwa njia hiyo ya mkutano mtandao kutokea Dar es salaam.
Viongozi na Maafisa wengine waandamizi wa Mahakama wakifuatilia kwa njia hiyo ya mkutano mtandao kutokea Dar es Salaam.

(Picha na Innocent Kansha - Mahakama)






Hakuna maoni:

Chapisha Maoni