· Majaji Wafawidhi, Wadau wakumbushwa kuhusu kudhibiti mafadhaiko
kuboresha utendaji kazi
· Washauriwa pia kusawazisha kati ya Taaluma na Utu
Na MARY GWERA, Mahakama-Arusha
Kikao cha Haki Kazi baina
ya Shirika la Kazi Duniani (ILO) na Majaji Wafawidhi wa Mahakama Kuu ya
Tanzania na wadau wa haki kazi kinachofanyika jijini Arusha kinaendelea
huku washiriki wa kikao hicho wakiendelea kupatiwa mada mbalimbali zenye lengo la kuboresha utendaji kazi.
Akitoa mada kuhusu Akili ya kihisia na udhibiti wa mafadhaiko (Emotional Intelligence and Stress Management) jana tarehe 15 Mei, 2025, Mwezeshaji wa Mafunzo, Bi. Zuhura Muro alitoa rai kwa viongozi wanaoshiriki katika kikao kazi hicho kudhibiti mafadhaiko ili waweze kufanya kazi ipasavyo.
“Kimsingi uongozi ni kuwezesha utendaji wa juu, kuwahamasisha wengine kufanya mambo kwa ufanisi, akili ya kihisia ni sifa muhimu ambayo husaidia viongozi kufanikisha kazi hii,” alisema Bi. Muro.
Mwezeshaji huyo alisema kuwa, Utu wa mtu una nafasi kubwa katika kutokea kwa mafadhaiko, ambapo amebainisha mambo muhimu ya kuzingatia ili kudhibiti kutokea kwa mafadhaiko na kukuza ustawi wa akili ni pamoja na kuzingatia ulaji sahihi, kufanya mazoezi, kunywa maji, kupumzika na mengine.
Kadhalika, Bi. Muro aliongeza kuwa, akili ya kihisia akili ya kihisia (emotional intelligence) ni muhimu katika utendaji na inahusisha seti ya ujuzi ambao hutusaidia kutambua, kuelewa, kueleza, sababu na kudhibiti hisia, ndani yetu na wengine.
Kwa upande wake, Prof. Samuel Wangwe mmoja kati ya Wawezeshaji wa Kikao hicho, akiwasilisha mada kuhusu Kusawazisha Taaluma na Utu (Balancing Professionalism and Personality) amesema kunahusisha kudumisha mwenendo wa kitaaluma huku ukiruhusu ubinafsi wako kung'aa kwa njia ambayo ni ya heshima na ya kweli.
Prof. Wangwe amesema kuwa, Kiongozi anatakiwa pia kuheshimu, kusikiliza kwa subira wakati wa mikutano na timu yake huku akithamini mchango wa kila mshiriki, kuwa muadilifu katika vitendo, kutoa majibu ya matatizo yenye kuzingatia usawa na haki, kutoa maoni yenye kujenga bila upendeleo na anaheshimu usiri wa mfanyakazi, kudumisha viwango vya maadili.
Ameongeza pia kuwa, ni muhimu kwa kiongozi kuwa na chapa yake binafsi (Personal Brand) ambayo inakuwa na mchanganyiko wa ujuzi, uzoefu na sifa za kibinafsi ambazo mtu angependa kujulikana kwazo.
Mada nyingine zinaendelea kutolewa katika kikao kazi hicho cha siku mbili chenye kaulimbiu isemayo: ‘Uboreshaji wa Uongozi kwa Ufanisi na Tija katika Utoaji wa Haki Kazi’.
Mwezeshaji wa Mafunzo, Prof. Samuel Wangwe akiwasilisha mada kuhusu Kusawazisha Taaluma na Utu (Balancing Professionalism and Personality) katika Kikao cha Haki Kazi baina ya Shirika la Kazi Duniani (ILO).
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni